MALI ZA MAMA’KE…MTOTO WA AMINA CHIFUPA AFUNGUKA

DAR ES SALAAM: IKIWA ni miaka 11 sasa tangu mama yake mzazi ambaye alikuwa mwanasiasa maarufu nchini, Amina Chifupa afariki dunia, mwanaye Abdurahman Mohamed Mpakanjia (18) (pichani) ameibuka na kufungukia mali alizoachiwa na marehemu mama yake.

Akizungumza na Amani mtoto huyo ambaye amehitimu kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Yemeni, alianza kwa kusema anamshukuru Mungu anaendelea vizuri na wakati anasoma hakupata shida kwani familia ilikuwa ikimuhudumia vizuri na kuona kama wazazi wake wapo hai.

Kuhusu mali ambazo aliziacha mama yake, alisema ziko mikono salama japo mpaka sasa bado hajazijua zote kwa kuwa muda mwingi alikuwa shule na alikuwa mdogo bado ila kwa sasa anamiliki gari la mama yake aina ya Toyota Prado na nyumba ambayo anaisimamia mjomba wake.

“Mali alizoacha mama yangu ziko kwenye mikono salama ambapo anazisimamia mjomba wangu anayeitwa Rich Maina na ndiye aliyekuwa akinilipia ada kwa hiyo sina shaka nazo. “Kuhusu kuhudumiwa nahudumiwa vizuri na familia zote mbili yaani ya marehemu baba na mama na nimekuwa nikiwaombea dua wazazi wangu huko walipo wawe mahali salama,” alisema Abdurahman.

ATAKA KUWA KAMA MAMA’KE

Pamoja na kufungukia mali hizo, mtoto huyo alieleza kuwa anataka kuwa mwanasiasa kama alivyokuwa marehemu mama yake ili aweze kuwatumikia wananchi kwa weledi. “Huwa nawaombea dua wazazi wangu na natamani sana niweze kuja kufanya vizuri kama mama yangu kwa kuwa sijawahi kusikia mambo mabaya kutoka kwake, kwa hiyo huwa najiona naishi na mama yangu yaani yupo pembeni yangu,” alisema.

Amina ambaye alikuwa Mbunge wa Viti Maalumu kupitia Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), alifariki dunia mwaka 2007 katika Hospitali ya Lugalo jijini Dar huku mumewe, Mohamed Mpakanjia akifariki mwaka 2009 katika hospitali hiyohiyo

Stori: Neema Adrian na Memorise Richard, Amani

Loading...

Toa comment