The House of Favourite Newspapers

Aliyetelekezwa na Mimba Amuua, Kumzika Mtoto Wake

0

 

MWANAMKE aliyejulikana kwa jina la Lucia Lukenya Mahizi (42) mkazi wa Kitongoji cha Wizunza kijiji cha Seke Ididi kata ya Sekebugoro wilayani Kishapu mkoani Shinyanga anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumuua kisha kumzika mtoto wake mwenye umri wa siku mbili kwa madai kuwa ni ugumu wa maisha baada ya kutelekezwa na aliyempa mimba.

 

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari, leo Alhamis Mei 28,2020 Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba amesema mtuhumiwa amekamatwa Mei 26,2020 baada ya wananchi kubaini kuwa mwanamke huyo hana mtoto aliyejifungua.

 

“Tunamshikilia Lucia Lukenya Mahizi (42) mkazi wa kitongoji cha Wizunza kijiji cha Seke Ididi kwa kosa la mauaji ya mtoto wake mchanga, jinsia ya kiume anayekadiriwa kuwa na umri wa siku mbili baada ya kuzaliwa kwake kisha kumzika mwenyewe pekee yake wakati mvua kubwa ikiendelea kunyesha ili watu wasimuone,” amesema Magiligimba.

 

Ameongeza kwamba Mei 26, 2020 majira ya saa kumi na mbili jioni (12:00) katika maeneo ya kitongoji cha Wizunza kijiji cha Seke Ididi wananchi wa maeneo hayo walibaini kuwa mtuhumiwa Lucia Lukenya Mahizi hana mtoto aliyejifungua tarehe Aprili  17, 2020.

 

“Baada ya wananchi kubaini kuwa Lucia hana mtoto ndipo wananchi hao waliamua kutoa taarifa kwa jeshi la polisi na mtuhumiwa huyo alikamatwa siku  ya Aprili 26, 2020,” ameeleza Magilimba na kueleza kwamba chanzo cha mauaji hayo kilidaiwa kuwa ni ugumu wa maisha baada ya kutelekezwa na aliyempa mimba.

 

“Mabaki ya mwili wa marehemu yalipatikana Mei 26, 2020 majira saa tisa alasiri katika kaburi alilozikwa na mtuhumiwa huyo na kukabidhiwa kwa ndugu kwa taratibu za mazishi,” aliongeza na  kutoa wito kwa wananchi hususani wanawake kuacha kukatisha uhai wa watoto kwa sababu tu ya kutelekezwa na wenza wao bali wafike katika madawati jinsia na watoto yaliyopo vituo vya polisi na ofisi za ustawi wa jamii ili kupata ufumbuzi wa matatizo yanayowakabili.

Leave A Reply