The House of Favourite Newspapers

Mama Ambipu Sirro! Amfanyia Unyama Mwanaye

0

SIKU chache baada ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Nyakoro Sirro kuzindua dawati la jinsia na watoto katika vituo vya polisi vya Butiama na Kiabakari wilayani Butiama mkoani Mara na kuwataka wanawake wawalinde watoto wao dhidi ya vitendo vya kikatili, Maria Nyakisirya (26), amembipu kiongozi huyo kwa kudaiwa kumfanyia unyama mwanaye, Risasi Jumamosi linakupakulia.

 

Mama huyo mkazi wa Kijiji cha Kiabakari, wilayani Butiama, anadaiwa kumfanyia unyama wa kutisha mtoto wake wa kumzaa kwa kumuunguza mikono kwa chai baada ya kumkuta amevaa bangili yake mkononi bila ya ridhaa yake.

 

Mashuhuda walioshuhudia tukio hilo la ukatili alilofanyiwa mtoto huyo lililotokea Desemba 10, mwaka huu wamesema, mama huyo alitoka katika shughuli zake muda wa saa 11:00 jioni na mara baada ya kufika nyumbani kwake alimkuta mwanaye huyo akiwa amevaa mkononi bangili yake moja, ndipo alipomshika na kuanza kumpa kipigo kikali kwa fimbo kisha akachukua chupa ya chai na kumuunguza mtoto huyo katika mikono yake.

 

“Baada ya kumfanyia unyama huo, alimfungia ndani ya nyumba na kuondoka na kumuacha akiugulia maumivu makali bila ya msaada wowote,” alisema shuhuda mmoja kwa sharti la kutotaja jina lake gazetini.

 

Aidha, shuhuda huyo alifafanua kuwa, mara baada ya mtoto huyo kufungiwa ndani ya nyumba na mama yake kutoweka, alijitahidi kujiokoa huku mikono yake ikiwa imevimba ambapo alifanikiwa kuvunja mlango na kutoroka kwenda kwa bibi yake aitwaye Skola ambaye ni mama mzazi wa mama yake.

 

Baada ya kufika kwa bibi yake ambaye pia anaishi Kiabakari, mtoto huyo alimsimulia kisa chote na bibi yake akaenda kutoa taarifa katika Kituo cha Polisi cha Kiabakari kisha akapewa PF 3 baada ya hapo polisi wakaenda kumkamata mama yake, huku mtoto akipelekwa kituo cha afya kutibiwa.

 

IGP ALIVYOONYA

Tukio hilo limejiri siku chache baada IGP Sirro kutembelea Kiabakari na kuonya wananchi kuacha vitendo vya kikatili kwa wanawake na watoto.

IGP Sirro alionya kwamba yeyote atakayefanya ukatili huo, jeshi la polisi litamshughulikia kwa kumkamata na kumfikisha mahakamani.

 

RPC ANENA

Kamanda wa Polisi mkoani Mara, Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Daniel Shilla amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.

 

“Ni kweli mama huyo Maria Nyakisirya (26) jeshi la polisi linamshikilia kwa kumuunguza mwanaye kwa maji ya moto na kwamba atafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria,” alisema Kamanda Shilla.

 

Aliwaonya wale wote wanaojaribu kupinga maagizo ya Kamanda Sirro aliyoyatoa alipofanya ziara mkoani kwake ya kuzuia ukatili kwa wanawake na watoto kwamba atakayekiuka atakumbana na mkono wa sheria.

Stori: Gregory Nyankaira, Mara

Leave A Reply