The House of Favourite Newspapers

Mama aua mwanaye kwa kipigo

0

INASIKITISHA! Mama mzazi wa Salome Pius Kahela (13) ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Iyela, Mbeya; Anipha Zambi mkazi wa Mtaa wa Iyela 0ne Kata ya Iyela, anadaiwa kumuua mwanaye huyo kwa kipigo.

Habari zilieleza kuwa tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki iliyopita ambapo mama Salome kwa kushirikiana na shemeji yake walimshushia kipigo mtoto huyo kwa madai kuwa alimnyang’anya mdogo wake shilingi 1000 za mama yake mdogo alizokuwa ametumwa sokoni.

Kutokana na kitendo hicho mama mzazi wa Salome alimpigia simu shemeji yake (jina halijafahamika) anayeishi Mtaa wa Maendeleo ili amsaidie kumwadhibu mwanaye kwani alichoshwa na tabia za udokozi ambazo zimetolewa taarifa mara kwa mara kwa balozi wa mtaa huo, Eliah William.

Shemeji alipofika nyumbani hapo kwa kushirikiana na mama huyo, pia mdogo wake na watoto wawili walianza kumpiga hadi kumsababishia umauti.

Akizungumza na Risasi Mchanganyiko, balozi wa eneo hilo, Eliah alisema alisikia watoto wakilia kutoka nyumbani kwa Anipha na baada ya kufika alikuta mtoto Salome amepoteza maisha.

Eliah alisema baada ya kushuhudia tukio hilo alilazimika kumpigia simu Mwenyekiti wa Mtaa wa Iyela One, Sadi Njechele ambaye alitoa taarifa Polisi ambao walifika na kuuchukua mwili wa marehemu hadi Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya kwa uchunguzi zaidi.

Mmoja wa mashuhuda, Hamad Tulyanje alisema kitendo kilichofanywa na wazazi kwa kushirikiana na watoto wawili si cha kiungwana kwani hatua waliyoichukua ni kubwa mno.

Uchunguzi ulibaini kuwa marehemu alikuwa akiadhibiwa mara kwa mara ambapo enzi za uhai mwenyewe aliwahi kusema huwa hajitambui wakati akifanya vitendo vibaya na kuonya asiwe anapigwa kwani watakuja kumuua.

Joseph Malaso ni jirani wa marehemu ambaye alieleza kuwa mara kadhaa wamekuwa wakipewa elimu kuachana na tabia za kujichukulia sheria mkononi. Walimu Kanyika Taabu na Lameck Hussein alikokuwa akisoma mtoto huyo, walisema mahudhurio ya marehemu Salome shuleni hayakuwa mazuri.

Kwa upande wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei alithibitisha kukamatwa kwa watu wanne kwa tuhuma za kusababisha kifo na kwamba uchunguzi ukikamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani.

Mwili wa marehemu ulisafirishwa kwenda Kitongoji cha Mwenzo Kijiji cha Itepula Kata ya Igamba wilayani Mbozi, Mkoa wa Songwe kwa ajili ya maziko.

Stori: EZEKIEL KAMANDA, MBEYA

Leave A Reply