The House of Favourite Newspapers

MAMBO 12 USIYOYAJUA Kuhusu Moi

0

Stori: GABRIEL MUSHI NA AMINA SAID, Ijumaa

WAKATI Wakenya na dunia kwa jumla wakiomboleza kifo cha aliyekuwa Rais wa Pili wa Taifa hilo, Daniel Arap Moi, IJUMAA tumekuchambulia mambo 12 usiyoyajua kuhusu kiongozi huyo aliyeitawala Kenya kwa miaka 24 kuanzia mwaka 1978 hadi 2002.

Kiongozi huyo alizaliwa Septemba 2, mwaka 1924 na kufariki dunia Februari 4, 2020. Yafuatayo ni baadhi ya mambo yaliyojificha katika kipindi cha uongozi wake.

FIMBO YAKE

Rais Moi alikuwa akipenda kifimbo chake na alikuwa nacho popote alipokuwa akienda. Thamani ya kifimbo hicho haikufahamika hadi baada ya kisa kilichotokea 1991 wakati kifimbo hicho kilichotengenezwa kwa pembe ya ndovu, kilipoanguka na kuvunjika vipande. Wakati huo Moi alikuwa jijini Los Angeles, Marekani baada ya mkutano wa Umoja wa Mataifa uliofanyika New York.

Kifimbo hicho kilivunjika wakati alipokuwa akijiandaa kuondoka Los Angeles kwenda Melbourne, Australia na kwa sababu ya umuhimu na thamani ya kifimbo hicho, Moi asingeweza kwenda mbali bila ya fimbo hiyo.

Kwa mujibu wa katibu wake; Lee Njiru, Ikulu ya Nairobi ilifahamishwa na kutakiwa kusafirisha kwa ndege kifimbo kingine hadi Australia. Ilibidi mfanyakazi mmoja wa ikulu apande ndege moja kwa moja na kifimbo cha Moi hadi Australia.

KUTUNZA KUMBUKUMBU

Wakati watu wakikaribia kuzeeka huweza kupunguza uwezo wa kutunza kumbukumbu. Lakini hali ni tofauti kwa Moi kwani alikuwa na uwezo mzuri wa kukumbuka na aliweza kumpigia mtu simu bila ya kuangalia daftari la anwani.

KUSAIDIA WATU

Baadhi ya watu wakipata umaarufu huweza kuwasahau watu wengine walio chini yake. Lakini hali imekuwa tofauti kwa mzee Moi, ambaye alikuwa akitumia karibia shilingi milioni 10 za Kenya kila mwaka kwa ajili ya kuwasaidia wasiojiweza.

HAKUWAHI KUBADILISHA FUNDI

Kutokana na umaarufu na cheo chake, hakuweza kumtupa fundi aliyekuwa akimshonea nguo kama ilivyo kwa watu wengine wenye nyadhifa fulani serikalini. Fundi wake wa nguo alikuwa ni yule yule kabla ya kuwa rais na baada ya kupata cheo hicho, na wala hakuwahi kumbadilisha.

MSAMAHA GUMZO

Moja kati ya hotuba zake za mwisho alipokuwa akiondoka madarakani mwaka 2002 ambayo iligeuka kuwa bora zaidi ni pale alipoomba msamaha kwa wote aliowakosea.

“Wale wanaotaka kuongoza, msiweke Kenya chini, msiweke msingi wa siasa zenu kwa chuki. Kama yuko mtu amenitukana namsamehe na kama kuna mtu ambaye nimesema chochote kikaumiza roho yake anisamehe,” alisema mzee Moi.

AMEISHI MIAKA 46 BILA MKE

Ni jambo la kushtusha kwa kiongozi mkubwa kama Moi, lakini ndivyo ilivyokuwa. Moi ameishi peke yake tangu mwaka 1974 baada ya kutengana na mkewe Lena kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kutokuwa mwaminifu.

Lena ambaye alizaa watoto nane na Moi, alikuwa mama wa taifa ambaye hakuwa akijulikana na watu wengi, akilinganishwa na wake wengine wa marais nchini Kenya.

Lena aliaga dunia 2004 na kuzikwa nyumbani kwa Moi Kabarak – Moi alisema angependa kuzikwa karibu na kaburi lake akifa na atazikwa huko.

UTATA UMRI WAKE

Vyombo vya habari nchini humo pamoja na duniani vinataarifu kuwa Moi alikuwa na umri wa miaka 95, lakini Msemaji wake; Lee Njiru amefichua kwamba rais huyo mstaafu ana umri wa kati ya miaka 102 hadi 103.

“Nimekuwa karibu naye na nimeshuhudia hali yake ya afya ikidorora kila miaka inapozidi kusonga. Ningependa kusema kwamba mzee Moi ana umri wa kati ya miaka 102 hadi 103, na wala sio 95 kama ambavyo wengi wanavyosema,” Njiru alifichua.

MAPINDUZI YAMGEUZA DIKTETA

Licha ya kupewa jina la ‘Profesa wa siasa’ kutokana na Taifa hilo kutokuwa na wafungwa wengi wakiwamo wa kisiasa. Agosti 1982 kulitokea jaribio la mapinduzi ambalo lilizimwa na wanajeshi waaminifu kwake.

Baadaye mwezi huo Rais alivunja kikosi cha jeshi la wanaanga, ambao wengi wao waliongoza jaribio hilo la mapinduzi.

Hata hivyo, kuanzia hapo Moi alianza kuwashughulikia vilivyo wapinzani wake, kwa kuwatesa katika vyumba maalumu na wengine hata kudaiwa kuuawa wakiwemo marubani wawili.

WASIOMPENDA ‘WALIMUUA MARA 14’

Msemaji wake; Lee Njiru pia amedai kwamba “Watu wasiompenda Moi walimuua mara 14” tangu 1983 kabla ya kifo chake Jumanne wiki hii.

‘’Tangu 1983 nimekuwa nikihesabu katika karatasi, amekufa mara 14. Hayo ni kwa mujibu ya watu wasiompenda, lakini hiki ndio kifo chake rasmi’’, Lee Njiru alikuwa akizungumza na runinga ya Citizen nchini Kenya.

Lee Njiru ambaye amekuwa katibu wa habari wa Moi, amemfanyia kazi kiongozi huyo kwa muda wa zaidi ya miaka 40.

GARI LAPAKWA MATOPE

Katika miaka ya mwisho ya uongozi wake, umaarufu wake ulishuka kutokana na kashfa mbalimbali. Katika uchaguzi wa 2002, ambao Moi alizuiwa kushiriki kikatiba, alidharauliwa kiasi kwamba gari lake lilitupiwa matope.

MAZIWA YA BURE SHULENI

Mwandishi wa BBC, Ferdinand Omondi anaeleza kuwa katika moja ya mambo anayoweza kumkumbuka Moi, ni maziwa ya ‘nyayo’.

Nyayo, ilikuwa ni filosofia yake ya amani, upendo na umoja. Miradi yake mingi ilitumia neno ‘’Nyayo’’.

Maziwa ya Nyayo yalikuwa ni mpango wa lishe aliouanzisha kwa mfuko wa serikali kwa ajili ya wanafunzi wa shule za msingi.

“Tulikuwa tunapata maziwa mara mbili kwa wiki; wakati mwingine pakiti moja, wakati mwingine mbili,” alisema.

ASHUKIWA KUMUUA WAZIRI WAKE

Katika mojawapo ya kashfa iliyomtikisa Moi, ni mauaji ya Dk. Robert Ouko aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wa Kenya.

Dk. Ouko alipotea usiku wa Februari 12, mwaka 1990 akiwa katika shamba lake lililoko huko Koru karibu na Muhoroni.

Tarehe 16 Februari, 1990 siku nne baada ya kupotea kwake, serikali ilitoa taarifa kwamba mwili wake ulikuwa umepatikana katika kilima cha Got Alila karibu na yalipo makazi yake.

Mwili wake ulikuwa umechabangwa mapanga kisha kuchomwa moto na ulikuwa umekutwa ukiwa na vitu mbalimbali ikiwemo bunduki, dumu la mafuta ya Diesel pamoja na kiberiti. Vyote isipokuwa hilo dumu la mafuta vilikuwa mali ya Ouko. Habari hii ya mauaji yake ilifanya mji wa Nairobi ulipuke kwa vurugu na maandamano.

Taarifa za mwanzo kutoka jeshi la polisi zilisema kuwa Ouko alijiua, lakini haikuchukua muda kugundulika kwamba Ouko alikuwa ameteswa, akapigwa risasi na mwili wake kuchomwa moto. Maswali na vurugu za wananchi zilimlazimu Moi, kuomba makachero kutoka shirika la upelelezi la Uingereza lijulikanalo kama New Scotland Yard, kusaidia kuchunguza kifo chake.

Uchunguzi uligundua kwamba Ouko alikuwa akiandaa ripoti kuhusu mwenendo wa rushwa kwenye serikali ya Kenya na jinsi rushwa ilivyozuia mipango yake ya kufungua kiwanda cha kuzalisha Molasses katika jimbo lake. Ripoti hiyo haikuonekana baada ya mauaji yake na ilikisiwa kwamba mauaji hayo yalikuwa na lengo la kuzuia hiyo ripoti isitoke.

Machi mwaka 2003, Serikali mpya ya Mwai Kibaki ilifungua upya uchunguzi wa kifo cha Ouko kwa kutengeneza kamati ya bunge ya kuchunguza suala hilo. Machi mwaka 2005, bunge liliamuru Moi kwenda bungeni kutoa ushahidi.

Leave A Reply