The House of Favourite Newspapers

Maskini Menina, Anahitaji Msaada wa Haraka

0

WAKATI Dunia ikiwa kwenye pilikapilika za mwisho wa mwaka 2021 na kuingia 2022, aliibuka msanii wa Bongo Fleva, Tamthiliya na MC maarufu Bongo aitwaye Menina Attick na kufunguka mambo mazito ambayo kwa bahati mbaya hayakupewa kurasa za mbele za magazeti au mitandao.

 

Menina alisema kuwa, baada ya ukimya wa muda mrefu amerejea kwenye muziki wa Bongo Fleva; safari hii alijitambulisha kama Queen of Bongo Fleva (Malkia wa Bongo Fleva).

Nanukuu kwa ufupi kile alichokisema ili twende kwenye msingi wa makala hii; “Baada ya kimya cha muda mrefu nimekuwa nikilisoma gemu, lakini nimegundua kuna utani mwingi sana, sasa nimeamua kurudi mwenye Bongo Fleva yangu.

 

“Mimi ndiye Queen wa Bongo Fleva, yes I’m the Queen, safisha njia malkia nipite, nibebe, chahamu, kungwi (majina ya nyimbo zake mpya ndani ya EP yake ya The Queen Is Back)…”

Menina ni zao la shindano la kusaka vipaji vya kuimba la Bongo Stars Search (BSS); anadai amegundua kuwa kuna utani mwingi kwenye tasnia ya muziki hivyo ameamua kurudi rasmi kwenye gemu. Usiniulize aliwahi kutikisa na wimbo gani!

 

Katika mkutano wake na vyombo vya habari, Menina alisema mengi kuhusiana na kufiwa na mumewe kisha mtoto wake ambaye alikuwa hajafikisha hata siku 40! Inauma na si lengo langu kumkubusha Menina machungu, lakini kuna kitu hakipo sawa!

 

Mbali na kuzungumzia misiba hiyo mizito miwili, Menina alizungumzia pia maelewano hafifu na waandaaji wa Tamthiliya ya Juakali aliyokuwa akionekana, lakini ghafla akawa hayupo. Hapa akaelekeza tuhuma nzito kwa Lamata; muandaaji wa tamthiliya hiyo maarufu Bongo.

 

Nilirudia mara kadhaa kumsikiliza Menina hatua kwa hatua nikimtazama pia kwa lugha ya ishara au ‘mudi’ yake ndipo nikagundua; maskini Menina anahitaji msaada wa haraka mno wa kisaikolojia.

Naelewa machungu ya mtu kufiwa na watu muhimu kama mume na kubaki mjane kisha kufiwa na mtoto; matukio ambayo yalifuatana.

 

Nilidhani kwamba, haukuwa muda mwafaka kwa Menina kujitokeza hadharani na kuzungumza aliyoyazungumza akionekana kabisa ‘bado hajapona maumivu ya kufiwa’.

Katika kuthibitisha hilo ninalolisema, baada ya kuachia EP yake hiyo na matokeo kuwa kama yalivyo ndipo akaibuka na waraka mzito. Usome kisha nitahitimisha;

 

“Habari ndugu zangu, leo ningependa kuongea yale ya moyoni, nafikiri kuna watu wananiona mimi kama mtu mwenye roho mbaya kwa sababu nimerudi kufanya kazi, la hasha napenda kuweka wazi kuwa nimepitia mambo mengi magumu sana.

 

“Nilipolia hamkuwepo na niliponyamaza pia hamkuwepo…. Nilitukanwa sana nikayabeba au huwenda kutokana na nature (asili) ya kazi zangu naonekana kama naparty (kusherehekea) kumbe maskini ya Mungu ndiyo mfumo wa kazi yangu ili uingize pesa inabidi ucheke hata kama moyo unalia…..

 

“Nimejaribu kujiweka sawa Mungu amejua kuijenga Imani yangu na mwenye Imani hakufuru sitatetereshwa na kitu chochote abadani asilani….. “Faraja pekee niliyokuwa nikiitegemea ni ya Mwenyezi Mungu na ndugu zangu wanaonipenda kwa haki, ama kwa hakika Mungu hakupi mtihani akakunyima namna ya kuuvuka.

 

“Ni ngumu mimi kama binti tena ninayetegemewa kama muhimili wa familia nimekaa ndani miezi mitano na siku kadhaa bila kufanya kazi yoyote na kutumia akiba tu, mimi nina mahitaji muhimu kama binadamu kuna bills, kuna ada za watoto na mengine mengi.

 

“Maisha siyo rahisi kiasi cha kukaa ndani na maumivu kila siku, Jamani nilishaomboleza, nilishalia na Mungu wangu itoshe kusema Mungu ni mwema sana….nimeona nitoke nijitafutie ni ngumu kukaa ndani muda woote huo.

 

“Hata mimi nina moyo na maumivu pia ila ili maisha yaende hatutakiwi kubaki na majeraha yenye kuzuia kusonga mbele… Hakuna mabadiliko ukiendekeza hasi bali kuna mabadiliko ukiizingatia chanya. Lawama, fedhea, matusi na mambo yote ya maangamizi kila jambo baya ni langu mimi, ndiyo fungu langu, nalipokea, lakini sitaacha kuwapenda wote mnaonipenda na mnaonichukia na kunitukana, Mungu aliwaleta kwangu na mimi simpingi, nawapokea wote kwa idadi Mungu anayonikabidhi hata iwe kwa makundi…Nawapenda wote.

 

“Hata wewe uliumbwa binadamu, laweza kukutokea lolote, mitihani ni ya binadamu, siyo mawe wala vyuma kila mtu apokee lake analopewa na kushushiwa na Mwenyezi Mungu kwa maana hakuna limfikalo mja bila Mungu kuliruhusu. Usiombe likukute.. Sijawahi kuishi kwa kusikiliza maneno ya watu, naishi kwa kusikiliza maneno ya Mungu..Siyo kila mtu atanipenda hata Mungu yupo lakini kuna wasioamini kama yupo, sijawahi kukatata maa, sitakata tamaa, imara kuliko jana…”

 

kwa kusoma waraka huu wa Menina na kuutafakari neno kwa neno, utakubaliana na mimi kwamba anahitaji msaada wa haraka wa kitaalam au kisaikolojia ili kumuweka sawa.

Ni matumaini yangu kwamba, walio karibu yake wataifanya kazi hiyo, badala ya kumuacha mwenyewe kwani anaweza akashindwa kuhimili na tukajikuta tunazungumza mengine.

Makala; Sifael Paul, Bongo

Leave A Reply