The House of Favourite Newspapers

Mastaa Hawa: Utamu wa Udoa Zao Unakuja, Unakata!

0

NDOA si kitu cha mchezo, watu hufikiri kwamba kuingia katika maisha ya ndoa ni kitu cha mchezo, nani kasema? 

Ndoa inahitaji kujitolea sana, maana ya kusema hivi ni kwamba mastaa wetu hapa Bongo, wengi wao wamekuwa wakitangaza ndoa na mwisho wa siku wanabaki wanaheng’i tu!

Leo katika makala haya utapata kujua baadhi ya mastaa ambao wamekuwa wakitangaza kuingia katika maisha ya ndoa lakini utamu unakuja halafu ghafla unakata.

 

DIAMOND NA TANASHA

Naseeb Abdul ‘Diamond’ na Tanasha Dona, wapenzi hawa wenye mahaba shatashata na wamejaaliwa mtoto mmoja wa kiume Naseeb Junior, mara kadhaa wametangaza ndoa lakini baadaye ishu imeyeyuka.

Diamond Platnumz alitangaza kuwa ndoa yake na Tanasha itafanyika kwenye sikukuu ya Valentine mwaka jana; watu wamesubiri weee tena kwa udi na uvumba, mwisho wa siku wawili hao waliishia kusherehekea sikukuu hiyo katika bonge moja la hoteli jijini Nairobi, Kenya na vumbi likapita bila ndoa yoyote kufanyika.

 

BEN POL NA ANERLISA

Msanii wa Bongo Fleva Bernard Paul ‘Ben Pol’ na mpenzi wake Anerlisa Joseph Karanja Mungai, wawili hawa wamekuwa katika penzi zito ambapo wamekuwa wakizunguka miji mingi wakila bata, kitu ambacho kimefanya kaka yetu kupotea kidogo kwenye gemu.

Juni 22 mwaka jana, ilisemekana kuwa wawili hawa wamefunga ndoa ya kimila na baadaye itafuatiwa na ndoa nyingine ambayo itakuwa bonge la ndoa Afrika Mashariki.

Mpaka sasa hakuna kinachoendelea kati yao, utamu wa ndoa unakolea na kukata.

Badala yake, yameanza maneno maneno kuwa huwenda hata penzi lao siku hizi ni kama limenyauka flani hivi tofauti na ilivyokuwa zamani.

 

RAYVANNY NA FAHYMA

Msanii Raymond Mwakyusa ‘Rayvanny’ na Fahyma ni wazazi wa mtoto Jaydan.

Wawili hawa walikuwa katika penzi motomoto lenye malavidavi ya kilo, kiasi kwamba mwanadada huyo ambaye ni Video Vixen (muuza nyago) aliyeunakshi hata wimbo wa mpenzi wake ujulikanao kwa jina la Siri, alikuwa akijimwambafai mara kadhaa kwamba yuko mbioni kufunga ndoa.

 

Rayvanny ambaye ni msanii kutoka lebo ya WCB, naye alitangaza kufunga ndoa na mpenzi wake huyo wa muda. Inasemekana kuwa alishawahi kumpeleka mpenzi wake hadi nyumbani kwao Mbeya kumtambulisha.

 

Ya Mungu mengi, maana kwa sasa penzi hilo halijulikani limekumbwa na jini gani maana mara limevunjika mara lipo hai, basi ni sarakasi tupu lakini ukweli unabaki kuwa ndoa yao haijafanyika mpaka sasa.

 

LULU NA MAJIZO

Muigizaji nguli wa Filamu Bongo, Elizabeth Michael ‘Lulu’ na bosi wa kituo cha redio moja nchini, Francis Siza ‘Majizo’ nao ni miongoni mwa wapenzi ambao ndoa zao utamu wake unakuja na kutoweka.

Wawili hawa wamekuwa katika makopakopa mujarabu kwa muda mrefu mpaka 2018, ambapo mzee Baba Majizo akaamua kumvisha pete ya uchumba mrembo huyo na kutangaza ndoa.

 

Katika tukio la kumvisha pete, Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda alichaguliwa kuwa kama mwenyekiti wa kamati.

Watu wakasema sasa mambo yameiva kisawasawa, lakini mpaka sasa kumekuwa na ukimya unaoleta sintofahamu.

 

Mara kadhaa wawili hao wamekuwa wakiulizwa “Vipi ndoa yenu ipo au haipo?” Ambacho wamekuwa wakikijibu kimekuwa kama lugha ya kigeni, wanaofahamu ni wachache.

 

DULA MAKABILA NA MAIYA

Dula Makabila ama kama anavyopenda kuitwa eti ‘mfalme wa singeli hapa Bongo’ alikuwa kwenye dimbwi zito la mahaba na aliyekuwa mpenzi wake aliyetambulika kwa jina moja la Maiya ama Mwarabu.

Penzi motomoto lilimpagawisha mfalme wa singeli hadi kumfanya aende kumtambulisha mwanamama huyo kwa mama’ake na kutangaza ndoa kwamba itafanyika Februari mwaka huu, hata hivyo ukimya umekuwepo kuwepo.

 

Licha ya kuandamwa na maneno kibao kuwa mwanamke huyo amemzidi umri mzee baba, lakini mwanzo jamaa hakuonekana kujali sana na kwamba aliendelea kutangaza ndoa.

Baadaye kuna jini makata fulani inaonekana kama amepita na kuiyeyusha ndoa hiyo, maana hata Dula akiulizwa leo mipango inaendeleaje amebaki kuwa ‘msanii anayejibu kisanii sanii’ mambo siriaz kama haya ya ndoa.

 

EMMANUEL MBASHA

Huyu jamaa ni muimbaji wa nyimbo za Injili, alikuwa ni mume wa Flora Henry (Flora Mbasha), si vibaya hata sasa ukamuita mume wa mwanadada huyo kwa sababu Imani ya Kikristo haitambui talaka.

Lakini baada ya upepo wa shetani kuwapitia wawili hao na kuivunja ndoa yao miaka kadhaa iliyopita, Flora aliamua kuolewa na kijana aitwaye Daudi Kusekwa na kumuacha Mbasha akiwa ‘msimbe.’

 

Mbasha alipovumilia kukaa usela na kujiona kachoka, akaja na ngonjela kuwa naye anao mke mwema.

Lakini cha kushangaza kila alipotoa tangazo hilo, watu walipomuuliza “Shemeji yetu ni nani?” Alificha jina lake kana kwamba ni suala la kichawi, basi watu waliendelea kumuamini kuwa jamaa anaoa lakini hadi leo hakuna cha ndoa wala mtoto wake.

MAKALA: KHADIJA BAKARI NA HAPPYNESS MASUNGA

Leave A Reply