The House of Favourite Newspapers

Mastaa Hawa Wamekwepa Mishale Mingi!

0

 

KWENYE uwanda wa burudani Bongo hii, kumekuwa na wimbi la wasanii wengi na wanaofanya vizuri.

Miaka ya nyuma waliibuka wasanii wakali katika Hip Hop na Bongo Fleva.

Wasanii hao walitikisa vilivyo kwa kutoa kazi ambazo zilibamba kwenye vyombo vya habari na kuwakusanyia mashabiki kibao.

Kati ya wasanii hao, wapo ambao safari zao ziliishia njiani na kushindwa kufika mbele zaidi kwa sababu zao binafsi, lakini wengine wamekaza na kuendelea kutikisa mpaka sasa.

Makala haya yanakuletea wasanii wakongwe kwenye gemu la muziki ambao unaweza kuwaita nyani wazee ambao wameruka mishale mingi, lakini bado wanakiwasha ile mbaya;

JIDE

Judith Wambura ‘Jide’ ni kati ya wasanii wa kike waliofanya ‘wandaz’ na bado kukiwasha kwenye muziki.

Jide aliwika na ngoma kama Machozi, Siku Hazigandi na nyingine nyingi ambapo ngoma hizo zilikuwa ndani ya album zake kali na kubwa.

Aliamsha kinoma kwenye albam zake za Machozi ya mwaka 2000,

Binti ya mwaka 2003,

Moto ya mwaka 2005, Shukrani ya mwaka 2007, The Best of Lady Jaydee ya mwaka 2012, Nothing But The Truth ya mwaka 2013

na Woman ya mwaka 2017.

Mbali na hilo, Jide anafanya poa katika ngoma aliyoshirikishwa na Harmonize inayokwenda kwa jina la Wife.

MADEE

Rais wa Manzese, Hamad Ally ‘Madee’ amefanya poa katika muziki wa kuchana (Hip Hop) kabla ya kulainika na kuimba Bongo Fleva.

Madee ni memba wa kundi la Tip Top Connection chini ya meneja Hamis Taletale ‘Babu Tale’. Jamaa amekinukisha na ngoma kama Goma la Manzese Bado Tunapanda, Kiboko Yao, Riziki na nyinginezo.

Aliendelea kufanya poa na mapigo mengine kama Hela, Kazi Yake Mola, Vuvula, Pombe Yangu, Tonight, Sikila, Disco Vumbi na kwa sasa anakimbiza na mkwaju wake mkali wa Shenzi Type aliouachia hivi karibuni.

MWANA-FA

Hamis Mwinjuma ‘Mwana-FA’ unaweza kumuita Binamu. Jamaa amewika kinoma tangu miaka ya 2000 na vibao kama Ingekuwa Vipi, Alikufa kwa Ngoma, Msiache Kuongea, Bado Nipo Nipo, Ameen, Kama Zamani, Yalaiti, Dume Suruali na nyingine kibao.

Mwana-FA amezidi kuonesha umwamba kuwa yeye bado yuko mzigoni kwa kuachia goma kali la Gwiji likiwa linakimbiza katika Mtandao wa YouTube na kwingineko.

KIBA

Mfalme wa Bongo Fleva, ndivyo unavyoweza kumuita na Bosi wa Lebo ya King’s Music Records, Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’. Ni mwanamuziki mkubwa anayetikisa katika Bongo Fleva.

Kiba ni mwanamuziki asiyechuja tangu enzi za Cinderela, Nakshi Nakshi, Dushelele, Usinisemee, Njiwa, Cheketua, Single, Mwana, Mapenzi Yana-Run Dunia na nyingine kibao ambazo zilifanya poa.

Ameendelea kufanya poa na vibao kama Mshumaa, Dodo, Mbio na sasa anakimbiza na mkwaju mkali wa So Hot aliouachia Juni mwaka huu.

AY

Ambwene Yessayah ‘AY’ ni mwanamuziki mkubwa wa Hip Hop ambaye alikuwa memba wa Kundi la East Coast Team lililokuwa chini ya mwanamuziki Gwamaka Mujuni ‘Crazy GK’.

Amefanya poa na kolabo za kimataifa akiwa na wasanii wakali na wanaokubalika mfano J Martins wa Nigeria au Sean Kingston (Jamaica).

Jamaa amekimbiza na ngoma kama Machoni Kama Watu, Nangoja Ageuke, Raha Kamili, Binadamu na nyingine kibao.

AY alifanikiwa kutoa album zake mwenyewe zilizokwenda kwa majina; Raha Kamili ya mwaka 2003, Hisia Zangu ya mwaka 2005 na Habari Ndiyo Hiyo ya mwaka 2008, zote zikiwa zimesheheni ngoma kali.

Hivi karibuni aliachia ngoma mpya inayokwenda kwa jina la Danihela na imekuwa ikifanya poa kwenye mitandao yote ikiwemo YouTube.

MR BLUE

Khery Sameer ‘Mr Blue’ amekimbiza kinoma kwenye Bongo Fleva.

Mr Blue alikuwa gumzo na wimbo wa Blue kabla ya kuja kupata umaarufu zaidi na wimbo wake wa Mapozi ambao ndiyo uliomzidishia kupendwa kutokana na mpangilio wa mashairi na sauti aliyotumia pamoja na maujanja ya ala ya muziki wenyewe.

Aliendelea kufanya poa na ngoma kama Tabasamu, Baki na Mimi, Kiss Kiss, Mboga Saba na kwa sasa anafanya poa na ngoma yake ya Mautundu. Pia amekuwa akishiriki kolabo kibao.

DULLY SYKES

Jamaa ana kipaji cha hali ya juu na manjonjo ya kutosha, Abdul Sykes almaarufu ‘Dully’. Alijipatia umaarufu mkubwa kwa kufanya poa na ngoma kama Nyambizi, Salome, Julieta, Leah, Hi na nyingine nyingi.

Akafanya maajabu kwa kuachia album kali kama Historia ya Kweli, Handsome na Hunifahamu ambazo zilifanya poa na kumpa sifa ya kuwania Tuzo za Tanzania Music.

Dully ameendelea kutikisa kwa kizazi cha sasa kwa kufanya kolabo na wanamuziki wakali kama Harmonize kwenye ngoma mbili.

CHEGE

Memba wa Kundi la Wanaume Family lenye maskani yake Temeke jijini Dar, Said Chigunda ‘Chege’ ni miongoni mwa wasanii wenye ngoma kali hapa Bongo na kufanya kolabo na wasanii wakubwa katika Bara la Afrika.

Amefanya poa na ngoma kama Lover Boy, Chapa Nyingine, Uswazi Take Away, Mkono Mmoja, Twen’zetu, Kinomanoma, Kama ni Gangstar, Weka, Mwanayumba, We Mtoto, Unanishawishi.

Nyingine ni Manjegeka, Sweety, Kaunyaka, Kelele za Chura, Najiuliza, Waache Waoane, Go Down, Mwananyamala, Wiper, Good Bye, Njoo na nyingine kibao ambazo ni kali ikiwemo Wafoo inayoendelea kufanya poa mitandaoni.

TID

Khaleed Mohamed anafahamika zaidi kama TID (Top In Dar). Ni mwanamuziki wa Bongo Fleva. Alijipatia umaarufu na ngoma kama Mrembo, Zeze, Girl Friend, Siamini, Nyota, Wazuri ni Wengi, Kiuno, Asha, Nilikataa, Siku Kama Hizi na nyingine nyingi.

Aliendelea kufanya poa baada ya kuachia album zake kama Sauti ya Dhahabu, Only One, Girlfriend na Wazuri ni Wengi.

Mpaka sasa, bado anatajwa kama mkongwe anayeendelea kufanya maajabu kwani Aprili, mwaka huu, aliachia ngoma yake inayokwenda kwa jina la Bamba akiwa na sexy lady, Lulu Abass ‘Lulu Diva’.

MAKALA: HAPPY MASUNGA, DAR

Leave A Reply