The House of Favourite Newspapers

Mastaa Wavaa Mlegezo si Heshima Kwenu!

Nay wa Mitego.

Na GABRIEL NG`OSHA| GAZETI LA AMANI| SHOW BIZ XTRA

IMEZOELEKA kuwa wasanii ni kioo cha jamii kwa sababu wana nafasi kubwa ya kuonekana mbele ya hadhira. Kuonekana kwao kwa mazuri basi na jamii inajifunza kupitia wao hasa vijana wanaochipukia na watoto ambao muda mwingi wanawafuatilia kwenye runinga.

Lakini kwa sasa imekuwa tofauti, wasanii wengi wa Kibongo wamegeuka kuwa si kioo cha jamii bali ni waharibifu  wa jamii kutokana na tabia zao. Huku tabia zingine zikiwashushi heshima wao wenyewe.

Jux

Tumeshuhudia baadhi ya wasanii wakitajwa kwenye orodha ya kuuza na kutumia madawa ya kulevya, huko nyuma pia kumekuwepo na tetesi za wasanii hao kudaiwa kujiuza, kusagana na mambo mengine ambayo hayastahili kuigwa.

Hivi ni mzazi gani ambaye anaweza kuruhusu mtoto wake wa kike  kuchumbiwa au kuolewa na mwanaume mhuni, mwanaume ambaye anapenda kuvaa suruali chini ya makalio? Bila shaka hakuna, hivyo si jambo zuri katika jamii ni suala linalopaswa kupingwa na kukemewa kwa nguvu zote.

Aka katabia ka wasanii kupanda jukwaani wakiwa wamevaa suruali chini ya makalio si kakufanyiwa mzaha kwani kanawashushia heshima hata wao wenyewe. Ni wasanii wengi ila baadhi ya waliowahi kuonekana wakiwa wamevaa au wanavaa mlegezo ni pamoja na Nay wa Mitego, Dogo Janja, Baba Levo, Christian Bella, Tunda Man, Jux, Aslay na wengine kibao.

Hivi hili la kuvaa nguo kwa mtindo huo maarufu kama mlegezo linaifundisha nini jamii ya Kitanzania? Je, watoto wa kizazi kijacho wanajifunza au kuiga nini kwa wasanii wa Bongo kuvaa hivyo wanapokuwa majukwaani?

Madee

Vivyo hivyo kwa vijana wengi huko mitaani wanaona ni kama fasheni kuvaa kwa mtindo huo, kijana anatembea barabarani huku sehemu ya nguo yake ya ndani ikiwa nje tena hana wasiwasi kabisa. Kama mwanaume huwa nachagua mwanamke mwema wa kuoa, naamini hata wanawake nao huwa wanaangalia tabia za vijana walio maeneo yao kama wanafaa kuwa baba wa familia zao.

Sidhani kama mwanamke au msichana anayejitambua na kujiheshimu yuko tayari kuanzisha uhusiano na kijana au mwanaume mwenye tabia ya kuvaa nguo kiajabu. Kuvaa mlegezo ni ishara ya uhuni na pia inahusisha mtindo huo wa uvaaji na masuala ya matendo ya jinsia moja (ushoga), ingawa hata akina dada (tom boy) wapo pia wenye tabia hiyo ambayo siyo nzuri katika jamii.

 

Comments are closed.