The House of Favourite Newspapers

Maswa Waeleza Siri Kutokomeza Kipindupindu

0

MAMLAKA ya mji mdogo wa Maswa mkoani Simiyu imeeleza kuwa kupungua kwa kasi ya magonjwa ya mlipuko hususani kipindupindu katika mji huo kumetokana na usimamiaji  mzuri wa sheria na kanuni za mazingira pamoja na utoaji wa elimu hasa katika kipindi hiki cha Utawala wa awamu ya tano.

 

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Maswa mkoani Simiyu, Afisa Afya wa Mamlaka hiyo, Saimon Nyadwera alisema ni vizuri akachukua fursa hiyo kuwapongeza wananchi wa mji huo kwa kuweka mazingira safi na salama kwa hiyari.

 

Alisema kuwa licha ya wilaya kutenga siku ya jumamosi ya juma la mwisho wa mwezi kwa ajili ya kufanya usafi kuanzia saa 1.00  hadi saa 4.00 asubuhi lakini wakazi wa mji huo wamekuwa na utamaduni wa kufanya usafi wa mazingira yao kila siku.

 

“Tabia ya kuchukia uchafu na kutunza mazingira ambayo imejengeka katika jamii yetu ya wananchi wa mji wa Maswa  ni jambo zuri sana sambamba na kuheshimu sheria ya mazingira na kanuni zake kwa hiari ni kitu muhimu katika kulinda na kutunza mazingira, kulinda afya za watu na viumbe wengine kwa hili sina budi kuwapongeza wananchi,”alisema.

 

Alisema kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita chini ya serikali ya awamu ya tano wameweza kutoa elimu ya usafi wa mazingira kupitia mikutano mbalimbali ya wadau wa mazingira pamoja na vyombo vya habari.

 

“Sisi idara ya afya ya Mamlaka ya mji mdogo wa Maswa katika kipindi cha miaka mitano tumetoa elimu kupitia vyombo vya habari na kuandaa mikutano mbalimbali ya wadau wa mazingira na wananchi kwa ujumla wake tumepata mafanikio makubwa kwani takwimu zinaonesha magonjwa ya milipuko kama kipindupindu kasi ya kuenea kwake imepungua sana, sikumbuki kama tumekumbana na kipundupindu miaka mitano iliyopita,’’ alisema.

 

Alisema  kwamba chanzo kikubwa cha magonjwa ya milipuko katika maeneo mbalimbali hapa nchini ni utiririshaji wa maji taka katika maeneo ya makazi ya watu pamoja na maji ya kemikali zenye sumu kutoka viwandani ambayo huelekezwa katika mito na makazi ya watu.

“Kwa kiasi kikubwa kipindupindu husababishwa na uchafu ambao huzalishwa majumbani, tumekuwa na utaratibu mzuri wa kudhibiti maji taka katika makazi ya watu lakini pia tumeweza kukutana na wenye viwanda vilivyoko katika mji wetu wa Maswa na kuwapa elimu juu ya kudhibiti mifumo ya utiririshaji maji yenye kemilkali zenye sumu kutoka kwenye viwanda,’’ alieleza.

 

Aidha, alisema kuwa mafanikio hayo yamepatikana kutokana na ushirikiano mkubwa walioupata kutoka kwa wananchi kupitia kwa viongozi wa dini,viongozi wa serikali za mtaa na halmashauri ya wilaya ya Maswa nasi tutaendelea kusimamia kanuni na sheria za mazingira ili ziweze kuwaletea tija wananchi wa mji huo.

 

Naye Mkuu wa wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyonge akizungumzia mafanikio hayo alisema kutokana na mwitikio chanya wa wananchi katika eneo hilo nitamwelekeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Dk Fredrick Sagamiko kuunda timu ambayo itakuwa na kazi ya kuhakikishachangamoto za kimazingira zinashughulikiwa kwa wakati.

 

“Mafanikio haya hayawezi kusemwa vizuri kama hatutaweza kutambua mchango wa wananchi ambao wamekuwa wakitoa taarifa za mara kwa mara juu ya uharibifu wa mazingira unaotokea katika maeneo mbalimbali jambo ambalo sasa nitamwelekeza Mkurugenzi wa halmashauri yetu ya Maswa  kuunda timu ambayo itafanyakazi  kutatua changamoto ya masuala yote ya kimazingira yanapotokea tena kwa muda muafaka,” alisema.

 

Pia alisema kuwa licha ya mafanikio yaliyopatikana lakini aliwaonya baadhi ya wenye viwanda vidogo vidogo  na wananchi katika mji huo wanaoendelea kutitirisha maji machafu kuacha mara moja tabia hiyo kwa kuwa serikali ipo macho na inapokea taarifa zote muhimu kutoka kwa wananchi wema na kuahidi kuwachukulia hatua kali za kisheria watakapobainika.

NA MWANDISHI WETU SIMIYU

 

Leave A Reply