The House of Favourite Newspapers

Mbaroni kwa Madai ya Kuuza Nyama ya Mbwa

0

Nyama ya Mbwa (2)
Stephano Mango, RISASI JUMAMOSI

RUVUMA: Kimenuka! Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma linamshikilia Musa Moyo (40) wa Kijiji cha Mbangamawe wilayani Songea mkoani hapa kwa tuhuma za kuwauzia nyama ya mbwa majirani zake.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Revocatus Malimi alisema tukio hilo lilijiri Januari 12, mwaka huu katika kijiji hicho ambapo inadaiwa Moyo alikamatwa na afisa mtendaji wa kijiji hicho, Theopista Komba.

Kamanda Malimi alisema siku ya tukio, afisa mtendaji huyo alipokea taarifa kutoka kwa raia wema kuwa, Moyo anafanya biashara ya kuuza nyama ya mbwa kwa matumizi ya binadamu.

Alisema mtendaji huyo alilazimika kufuatilia tukio hilo kwa kina ambapo alikwenda nyumbani kwa Moyo akijifanya mteja wa nyama hiyo kwa ajili ya kitoweo.

Nyama ya Mbwa (1)Alisema, Moyo alimuuzia Komba nyama kidogo iliyokuwa imebaki ndipo mtendaji huyo alipomkamata na nyama hiyo iliyokuwa imekaushwa na kukatwa vipande.

Afande Malimi alisema Moyo alifikishwa kwenye Kituo Kikuu cha Polisi Mjini Songea na kufanyiwa mahojiano ambapo alikiri nyama hiyo ni ya mbwa aliyemchinja siku moja kabla ya kukamatwa.

Nyama ya Mbwa (3)Alijitetea kuwa, nyama hiyo ilikuwa ya matumizi binafsi ambapo mara kwa mara familia yake imekuwa ikitumia, ila kuna baadhi ya watu wamekuwa wakila nyama hiyo baada ya kuuziwa bila kujua kwa kuambiwa ni nyama ya porini.

Afisa Mifugo wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea alithibitisha kuwa, nyama hiyo ni ya mbwa ingawa jeshi la polisi likiendelea kufanya uchunguzi na kuwataka wananchi kuacha mara moja kununua nyama mitaani.

(PICHA ZOTE NA MAKTABA)

Leave A Reply