The House of Favourite Newspapers

Mbasha arudishwa kortini tena

0

Mwimbaji wa muziki wa Injili, Emmanuel Mbasha.

Brighton Masalu

SIKU chache baada ya kushinda kesi ya tuhuma za kubaka iliyokuwa ikimkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, mwimbaji wa muziki wa Injili, Emmanuel Mbasha anatarajiwa kupandishwa tena katika korti hiyohiyo kwa madai mengine, Risasi Mchanganyiko lina habari kamili.

 

Akizungumza na gazeti hili hivi karibuni kwa sharti la kutotajwa jina, mmoja wa watu wa karibu na wanandoa hao, alisema Flora amefungua kesi ya madai ya talaka katika Mahakama ya Kisutu na kwamba muda si mrefu shauri hilo litaanza kusikilizwa.

“Flora ameenda mahakamani kudai talaka yake, kwa hiyo kesi inatarajiwa kuanza kusikilizwa muda wowote kuanzia sasa,” alisema mtoa habari huyo.Baada ya taarifa hizo, mwandishi wetu alimtafuta Mbasha kwa njia ya simu na kumuuliza juu ya madai hayo, ambapo alikiri na kudai anajiandaa kukabiliana na shitaka hilo.

“Yeah, ni kweli kaka, Flora ameamua kwenda mahakamani kudai talaka yake, sioni kama ni tatizo, kwa sasa siwezi kuzungumza lolote kwa sababu limeshafika katika mkondo wa sheria na tunapaswa kusubiri tuone kitakachotokea, lakini naamini kila kitu kitakwenda sawa,” alisema Mbasha.

Kwa upande wake, mke wa mwimbaji huyo, ambaye pia ni mkali wa nyimbo za gospo, Flora Mbasha alipotafutwa hakupokea simu yake ya mkononi, lakini alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno (sms) alijibu kwa kifupi:
“Kaka, naendesha, kila kitu kiko mahakamani kwa hiyo sina la kuzungumza kwa sasa.”

Hali hiyo inatokea siku chache tu baada ya mahakama hiyo kumuachia huru mwimbaji huyo aliyekuwa akikabiliwa na mashtaka ya ubakaji ambayo pia yalimleta mkewe huyo mahakamani akiwa shahidi wa upande wa mashtaka.
Kwa muda mrefu, waimbaji hao wamekuwa katika mgogoro wa kifamilia ambapo juhudi za watu mbalimbali zimefanyika kusuluhisha lakini hazikufanikiwa.

JIUNGE NA GLOBAL BREAKING NEWS!

Leave A Reply