The House of Favourite Newspapers

Mbowe na Wenzake Wakutwa Na Kesi Ya Kujibu

0

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu imemkuta na kesi ya kujibu, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na wenzake watatu katika mashitaka 5 kati ya 6 hivyo wanapaswa kuanza kujitetea.

 

Uamuzi huo umetolewa na Jaji Joachim Tiganga ambapo amesema Mahakama imepitia ushahidi wote wa Jamhuri wa Mashahidi 13 ambao umewafanya Washitakiwa wakutwe na kesi ya kujibu.

 

Hata hivyo Mahakama hiyo imemuachia huru Mshtakiwa wa kwanza baada ya kutokuwa na kesi ya kujibu katika shitaka la sita la kukutwa na sare na vifaa vya Jeshi licha ya kwamba atajitetea katika makosa mengine.

 

Hatua hiyo inakuja baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wake kwa kuwaita mahakamani mashahidi 13 kati ya 24 iliokuwa imepanga kuwaita, huku ikitoa vielelezo 39.

 

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine ni Halfan Bwire Hassan, Adamu Hassan Kasekwa maarufu kama Adamoo na Mohamed Abdillahi Ling’wenya.

Tangu kesi hiyo ianze, imesikilizwa na majaji watatu; Elinaza Luvanda, Mustapher Siyani na Joachim Tiganga.

Kwa upande wa Jamhuri, mawakili ni Robert Kidando, Pius Hilla, Abdallah Chavula, Jenitreza Kitali, Nassoro Katuga, Esther Martin, Tulimanywa Majige na Ignasi Mwinuka.

Leave A Reply