MBUNGE: NIMEPAKWA KINYESI GEREZANI

DAR ES SALAAM: Mbunge wa Tarime Mjini kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleao (Chadema), Ester Matiko amefunguka mambo mazito ikiwemo kupakwa kinyesi cha binadamu alipokuwa gerezani, Gazeti la Ijumaa lina habari ya kipekee (exclusive).

 

Kwa mujibu wa Matiko, dhahama hiyo ya aina yake ilimfika alipokuwa mahabusu katika Gereza la Segerea jijini Dar. Matiko na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe walikaa siku 104 gerezani tangu mwishoni mwa mwaka jana hadi mwanzoni mwa mwaka huu baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar kuwafutia dhamana katika kesi inayowakabili ya jinai namba 112.

 

Katika kesi hiyo ambayo bado inaendelea, washtakiwa hao na wenzao ina mashtaka 13, ikiwamo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari Mosi na 16, mwaka 2018.

 

Katika mahojiano hayo maalum na Gazeti la Ijumaa, Matiko anafunguka mambo mbalimbali mazito kiasi cha kumfanya kuangua kilio wakati anahojiwa kama ifuatavyo;

Ijumaa: Matiko wewe ni mwakilishi wa wananchi wa Tarime, umekaa gerezani kwa miezi kadhaa, je, unawezaje kuzungumzia maisha yalikuwaje?

 

Matiko: Kwanza sijutii kwenda gerezani, natamani nirudi maana nimejifunza mengi sana. Nimejifunza kuwa kuna watu wengi sana wanateseka gerezani. Wapo wezi wadogowadogo ambao kesi zao zingeweza kumalizika serikali za mitaa na ngazi nyingine za chini kuliko kwenda kujaza magereza.

 

Nimeshtuka kujua kwamba magerezani kuna akina dada wa kazi wengi sana ambao hawana mtetezi. Kwa kifupi naomba kusema niliinjoi sana.

 

Ijumaa: Je, ni kweli kwamba waheshimiwa na watu wengine wakubwa wanawekwa vyumba maalum (VIP) tofauti na watu wengine?

Matiko: Hakuna VIP, lakini naweza kusema kwa Segerea hali ni nafuu ukilinganisha na magereza mengine ambayo ninajua hali zake kwa kuwa niliwekwa humo, mfano mkoani Mara. Mimi niliwekwa selo ya wagonjwa kwa sababu selo nyingine (za wanawake) zilikuwa zimejaa, lakini kwa wagonjwa kulikuwa na watu wachache na kuna afadhali kidogo.

 

Kule (gerezani) hakuna uhuru, watu wanafungiwa tu kwa hiyo siwezi kusema ni kuzuri. Kule niliwamisi sana watu wangu wa Tarime kwanza, kisha familia yangu hasa mume na wanangu watatu. Lakini kubwa ninaloweza kukumbuka ni kitendo cha kukutana na mahabusu watatu waliokuwa na tatizo la afya ya akili.

 

Nawakumbuka kwa majina. Kulikuwa na Zawadi, Lulu na Swaumu. Hawa walikuwa ni hatari kwa sababu tulichanganywa nao jambo ambalo ni hatari kwani nakumbuka siku moja mmoja alijisaidia usiku kisha akaanza kushika kinyesi chake na kuja kunishika na kunipaka, ilikuwa si hali ya kawaida.

 

Kwa kifupi nimepanga kufungua NGO (shirika lisilo la kiserikali) la kuwasaidia watu mbalimbali ambao wapo gerezani wanaokosa msaada wa kisheria.

 

Ijumaa: Mbali na kukaa mahabusu, kuna mambo mengine mengi umepitia kwenye siasa kama kupigwa, je, hilo halijakukatisha tamaa?

 

Matiko: Ni kweli nimepitia misukosuko mingi ya kupigwa na kuwekwa mahabusu. Nakumbuka ilikuwa mwaka jana kule Tarime kulikuwa na uchaguzi mdogo wa udiwani.

 

Kwenye zile kampeni niliambatana na wabunge wenzangu, Zitto Kabwe na Upendo Peneza tukitokea Dar. Tulipofika uwanjani tulikuta watu wametawanyika, nilipouliza kuna nini niliambiwa Polisi walisema hakuna kibali cha kufanya mkutano.

 

Wananchi waliponiona walisogelea uwanja, lakini bado Polisi waliendelea kuwatanya. Zitto akasema tuache. Sasa wakati tunaondoka uwanjani kama mita 30, Polisi wakanivamia, nakumbuka nilipigwa sana hadi leo nimepata matatizo ya mgongo. Kibaya zaidi aliyekuwa akinipiga ni Polisi mwanamke mwenzangu na ninamfahamu hadi leo.

 

Nakumbuka nilichukuliwa nikawekwa mahabusu ambako nililala hadi kesho yake kisha nilinyimwa PF-3 (fomu namba tatu) kwa ajili ya matibabu kwa sababu walijua nitawashtaki. Hata hivyo, baada ya tukio lile niliamua kusamehe na kujua kuwa ni sehemu ya changamoto ya kazi yangu ya kuwatetea wananchi wangu. Ijumaa: Katika mambo hayo yote mumeo alichukuliaje?

 

Matiko: Namshukuru Mungu mume wangu ananisapoti sana kwenye jukumu nililonalo la kutumikia wananchi na ni mwelewa. Kibinadamu, nilipopigwa sana kule Tarime alisema niache siasa na kama ikiwezekana, basi tuhame nchi tuhamie Marekani.

 

Wanangu pia waliumia sana, lakini kadiri siku zilivyosonga waliendelea kunisapoti. Hata wakati nikiwa Segerea familia yangu ilikuwa ikiumia hasa mwanangu wa mwisho ambaye alikataa hata kula akitaka kumuona mama yake. Kwa hayo yote waliona bora niache siasa, lakini mimi nikawaambia ninazidi kuwa strong (imara) na kweli sasa hivyo hata wao wanasema niko strong.

 

Ijumaa: Tunajua kabla ya kuingia kwenye siasa ulikuwa mwalimu mzuri wa hesabu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kwa nini uliacha na kuingia kwenye siasa? Matiko: Nilitaka kutimiza ndoto yangu ya kuwa sauti ya jamii yangu, lakini hata sasa hivi siyo kwamba nimeacha kabisa, ninaweza kurudi na kuendelea kufundisha.

 

Ijumaa: Jamii ya watu wa Tarime ni miongoni mwa jamii nyingi zinazoamini mfumo dume na kwanza

hawawezi kuongozwa na mwanamke, je, wewe ulifanikiwaje?

 

Matiko: Ni kweli mimi ni Mkurya, jamii ambayo ilikuwa inaamini mfumo dume, lakini sasa hivi hali ni tofauti. Ni kweli kwenye jamii yetu mimi ni mbunge wa kwanza mwanamke hivyo nilifanya kazi kubwa kuwahakikishia ninaweza kuwatumikia na sasa wanajua hawakukosea.

 

Ijumaa: Una mpango wa kuhama Chadema kwenda Chama Cha Mapinduzi (CCM) kama walivyofanya baadi ya wabunge na madiwani?

 

Matiko: Siwezi kuhama kwa sababu naweza kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli nikiwa Chadema. Mbona mara nyingi tu tunapongeza juhudi zake bila kujali vyama vyetu? Pia nikihama, kule Tarime kutatokea mauaji maana hawatakubali na ninawajua watu wangu. Kutatokea vita kubwa na watu watakatana mapanga.

 

Ijumaa: Umeshatekeleza kwa kiasi gani ahadi zako kwa wana-Tarime? Matiko: Hadi sasa nimekamilisha ujenzi wa shule nane mpya za msingi, tatu za sekondari na ninapigania maslahi ya walimu na ujenzi wa maktaba kubwa ambayo mbali na kutumika watu kupata elimu, pia itatumika kuhifadhi utamaduni wa watu wa Tarime.

 

Kwenye afya tumeboresha hospitali yetu ya mji wa Tarime na kujenga zahanati mbili kwa kutumia fedha za mfuko wa jimbo. Barabara nyingi zimejengwa na zinajengwa kwa kiwango cha lami, tumechimba visima 23 mpaka sasa na tuna mradi mkubwa wa maji hivyo, muda si mrefu tatizo la maji litapungua kama siyo kwisha kabisa jimboni Tarime.

 

Ipo mipango mingine mingi kama ujenzi wa Stendi ya Serengeti na soko la kimataifa la Tarime. Naamini kabisa wana-Tarime wana imani kubwa na mimi.

 

Achomwa NYETI Na ‘WAHUNI” Kisa Boss Wake / Kisa Chake Chashangaza!


Loading...

Toa comment