The House of Favourite Newspapers

Mchungaji wa KKKT Ashikiliwa na Takukuru kwa Kutoa Mikopo Umiza

0

Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) Mkoani Manyara inamshikilia mchungaji kiongozi wakanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Ufana Emanueli Petro Guse kwa kuendesha biashara ya mikopo umiza bila ya kuwa na leseni ya Biashara ya ukopeshaji fedha.

 

Mkuu wa Takukuru mkoani hapa Holle Makungu, amesema awali walipokea malalamiko toka kwa mwananchi wa eneo la Bashneti aliyekopa kwa mchungaji huyo kiasi cha shilingi laki mbili (200,000/=) na kurejesha shilingi laki nne (sh400,000/=) huku akiendelea kudaiwa shilingi laki nne na themanini (sh480,000=) kutokana na mkopo huo wa laki mbili hali iliyowalazimu kumuita mchungaji Guse kwa mahojiano.

 

Makungu amesema walimtaka mchungaji huyo kwa hiari yake aripoti katika ofisi za TAKUKURU zilizopo mjini Babati lakini alikaidi hatua iliyowalazimu kuwatuma makachero.

 

Amesema walipomkamata mchungaji Guse walimuuliza iwapo anafanya biashara ya kukopesha fedha ambapo mchungaji huyo alikana na kudai kuwa hajawahi kufanya biashara hiyo.

 

Makachero wa takukuru walilazimika kufanya upekuzi nyumbani na ofisini kwa mchungaji huyo ambapo waliweza kupata mikataba ya mikopo umiza arobaini na nane (48) nyumbani kwake.

 

Baadaya kukusanya nyaraka katika upekuzi, makachero wa TAKUKURU walimchukua hadi ofisi za Takukuru mjini babati na kufanya naye mahojiano ambapo mtuhumiwa alikiri kufanya biashara hiyo ya mikopo umiza bila leseni.

 

Mtuhumiwa alipoulizwa kuhusu mlalamikaji, alikiri kwamba ni kweli alimkopesha shilingi laki mbili (Sh.200,000/=), na kwamba mtuhumiwa amekwisha kurejesha kiasi cha shilingi laki nne (Sh.400,000/=) lakini bado anamdai tena shilingi laki nne na elfu themanini (Sh.480,000/=).

 

Mchungaji huyo anaendelea kushikiliwa na TAKUKURU Mkoa wa Manyara wakati uchunguzi wa mikataba umiza 48 iliyokutwa nyumbani kwake wakati wa upekuzi ukiendelea.

 

TAKUKURU Mkoa wa Manyara inatoa wito kwa mwananchi yeyote aliyeathirika na mikopo umiza ya mchungaji huyo katika maeneo ya bashnet, Ufana, Madunga na vijiji jirani wafike ofisi za TAKUKURI Mkoa wa Manyara zilizopo mjini Babati Jumamosi Agost 29, 2020 ili changamoto zao ziweze kushughulikiwa kwa pamoja.

Na John Walter-Manyara

Leave A Reply