The House of Favourite Newspapers

Medeama Vs Yanga… Dakika 90 Za Afe Kipa, Afe Beki Ghana

0

MOTO unawaka kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi msimu huu, kumekuwa na matokeo na matukio mengi ya kushangaza.

Nani aliamini vibonde Jwaneng wangeweza kumuua kigogo Wydad Casablanca kwao pale Morocco? Achana na hilo ulitarajia mabingwa wa African Football League, Mamelodi wangekufa kwa TP Mazembe?

Hii inaendea kuthibitisha ugumu wa mashindano ya mwaka huu. Leo Ijumaa tena moto utawaka kwenye viwanja mbalimbali. Kwa Tanzania wawakilishi Yanga watashuka uwanjani Ghana kuvaana na Medeama ya huko.

Championi Ijumaa, linakuletea dondoo muhimu za mchezo huu kama ifuatavyo:

YANGA KISASI, MEDEAMA REKODI

Katika soka la kimataifa timu hizi mbili sio mara ya kwanza kwa kukutana, kwani waliwahi kuvaana katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2016 ambapo Medeama waliibuka wababe.

Katika michezo miwili ambayo Yanga walikutana na Medeama katika mashindano hayo, mchezo wa kwanza uliopigwa June 16 Dar es Salaam uliisha kwa matokeo ya sare ya bao 1-1, huku mchezo wa marejeano ambao ulipigwa nchini Ghana Juni 26, ya mwaka huo ukishuhudiwa Yanga wakipoteza kwa kipigo cha mabao 3-1.

Hivyo mchezo wa leo kwa Yanga ni kama mchezo wa kisasi cha mwaka 2016, huku Medeama wao wakitaka kuendeleza rekodi yao bora kwa Yanga.

REKODI ZINAIPA JEURI YANGA KIMATAIFA

Tangu iliponunuliwa rasmi mwaka 2001 na mfanya biashara maarufu wa madini, Moses Armah, Medeama imekuwa timu ambayo inakuwa kwa kasi kwenye soka la Afrika lakini mafanikio yao makubwa yapo kwenye soka la ndani.

Kwenye mashindano ya kimataifa wana rekodi ya kucheza hatua ya mtoano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwenye vipindi tofauti. Kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika hii ni mara ya kwanza.

Kwa upande wa Yanga, wao kimataifa bado wanatambia rekodi yao kali kwenye Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita ambapo walimaliza washindi wa pili, wakipoteza mchezo mmoja tu, kwenye uwanja wa nyumbani mbele ya USMA ya Algeria, kwenye fainali ya kwanza na kupoteza ubingwa kikanuni kufuatia matokeo ya jumla ya mabao 2-2 kwenye michezo miwili ya fainali.

LOMALISA APANGUA KIKOSI CHA GAMONDI

Kuelekea mchezo wa leo kunatarajiwa kuwa na mabadiliko kidogo kwenye kikosi cha Yanga kutokana na changamoto ya majeraha ambayo ameyapata mlinzi, Joyce Lomalisa ambaye alipata majeraha ya kifundo cha mguu katika mchezo dhidi ya Al Ahly na anatarajiwa kukosekana kwa kipindi cha wiki moja.

Pamoja na majeraha ya Lomalisa, mchezaji Jonas Mkude naye yupo chini ya ulinzi wa madaktari baada ya kupata shambulio la ‘allergy’, lakini pia mfumo ambao amekuwa akiutumia kocha wao Muargentina, Miguel Gamondi katika michezo ya ugenini huathiri kikosi.

Kuhusina na uwezekano wa mabadiliko ya kikosi chake kwenye mchezo dhidi ya Medeama, Gamondi alisema: “Ukiachana na mabadiliko ya kimfumo kuendana na mahitaji ya mchezo tunalazimika kufanya mabadiliko kutokana na changamoto ya majeraha ya baadhi ya wachezaji wetu, lakini pia kwa kuwa tunacheza ugenini dhidi ya wapinzani bora.”

MIFUMO YA MAKOCHA

Hapa kutakuwa na vita kubwa kwani makocha wote wanaamini kwenye mfumo mmoja, kwa upande wa wenyeji Medeama kocha wao mkuu, Ignatius Osei-Fosu, ni muumini mkubwa wa soka la kushambulia akitumia muundo wa 4-2-3-1 kwa kuwekeza nguvu kubwa katika kujenga mashambulizi ya kasi.

Kwa upande wa wageni Yanga ambao wanaongozwa na Muargentina, Miguel Gamondi pia wanahusudu zaidi soka la kasi na kushambulia ambapo mfumo ni uleule 4-2-3-1.

YANGA WANASEMAJE?

Licha ya kuvuna pointi moja tu, katika michezo yao miwili ya kwanza baada ya kufanikiwa kutinga hatua ya makundi ambalo lilikuwa lengo mama, uongozi wa Yanga umetangaza sasa hesabu zao ni kucheza Robo fainali ya mashindano hayo.

Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe alisema: “Tunafahamu mchezo huu utakuwa mgumu zaidi kwetu kulinganisha na michezo iliyopita ya mashindano haya msimu huu, kwa kuwa kule hesabu za kila timu ni kupata pointi tatu muhimu.

“Tunaheshimu ubora wa wainzani wetu ila hata sisi pia tumekuwa na kikosi bora na tunajiamini, mafanikio ya kucheza fainali ya Mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita na kufuzu makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu yameongeza ari na sasa tunataka kuhakikisha tunakwenda kucheza Robo Fainali ya mashindano haya.

“Tumesahau matokeo ya michezo iliyopita tunaanza mapambano upya, benchi la ufundi limefanyia kazi mapungufu yetu ili kuandika rekodi mpya.”

KOCHA WA MEDEAMA ANAITAKA REKODI

Licha ya ubora wa kiosi chake na nafasi ya kuanzia nyumbani, lakini kocha mkuu wa Medeama ameweka wazi kuwa wanaiheshimu Yanga lakini hesabu zao ni kuandika rekodi kwenye mashindano hayo..

Akizungumzia mchezo wa leo Kocha huyo alisema: “Tunafahamu ubora wa Yanga na tunajua hautakuwa mchezo rahisi, tumewafuatilia na tunafahamu ni miongoni mwa timu bora sana kwa sasa, hivyo ni lazima tupambane licha ya kwamba tutakuwa nyumbani.

 

“Lakini malengo yetu ni kuandika rekodi mdimu huu katika mashindano haya licha ya kushiriki kwa mara ya kwanza.”

KUNDI D CAF

P    W D   L    GF GA Pts

1.Al Ahly       2    1    1    0    4    1    4

2.Belouizdad 2    1    0    1    4    2    3

3.Medeama   2    1    0    1    2    4    3

4.Yanga          2    0    1    1    1    4    1

Stori na Joel Thomas

Leave A Reply