The House of Favourite Newspapers

Meneja Atoboa Siri Mamilioni Aliyopiga Idris

0

MWIGIZAJI wa kimataifa wa Bongo Movies, Idris Sultan ndiye mshiriki aliyechukua Tuzo ya Big Brother Africa mwaka 2014 nchini Afrika Kusini akiwa na umri mdogo zaidi.

 

Kipindi hicho alikuwa na umri wa miaka 21 pekee na kuifanya Tanzania kuongoza katika nchi za Maziwa Makuu kwani hakuna nchi nyingine ya ukanda huu iliwahi kuibuka mshindi wa BBA.

 

Katika umri wake mdogo tayari amejihusisha na mambo mbalimbali kama uigizaji, uchekeshaji, uimbaji, utangazaji, ujasiriamali na vitu vingine vingi, ilimradi tu siku moja afikie pale anapopataka; yaani kuwa bilionea!

 

Hivi karibuni aliandika historia nyingine kubwa mara baada ya kuwa mwigizaji wa kwanza Tanzania kupata nafasi ya kushiriki katika Filamu ya Slay iliyoanza kuoneshwa rasmi Aprili 26, mwaka huu katika mtandao maarufu wa kurusha filamu duniani wa Netflix ambao ni huduma namba moja duniani inayoonesha filamu na tamthiliya kwa njia ya intaneti maarufu kama streaming.

 

Gazeti la IJUMAA WIKIENDA limekaa mezani na meneja wa Idris, Doctor Ulimwengu na kufanya naye mahojiano maalum (exclusive interview) ambaye anafunguka ishu nyingi kuhusu staa huyo na namna alivyopiga mamilioni ya pesa kwenye mchongo huo;

 

IJUMAA WIKIENDA: Mambo vipi Doctor Ulimwengu?

ULIMWENGU: Salama kabisa, karibu…

 

IJUMAA WIKIENDA: Asante, kwanza nianze kwa kukupa hongera kwa kazi kubwa unayoifanya ya kuhakikisha wasanii wako wote unaowameneji wanafikia ndoto zao…

 

ULIMWENGU: Nashukuru sana, binafsi nasema kazi iendelee, lengo langu ni kutaka kuwafikisha mbali zaidi ya hapo walipo sasa na nina imani kwa uwezo wa Mungu tutafika tu.

 

IJUMAA WIKIENDA: Ulijisikiaje baada ya Idris kutajwa kama mwigizaji wa kwanza Tanzania kushiriki kwenye Muvi ya Slay ambayo imeshaanza kuoneshwa rasmi kwenye Netflix?

 

ULIMWENGU: Kwetu imekuwa ni furaha kubwa, naamini malengo ambayo tuliyaweka miaka mitatu iliyopita, sasa tumeanza kuona matunda yake, kwa sababu target ya kuifikia Netflix tulianza kuiweka muda mrefu na tumekuwa tukiifanyia kazi. Kwa naweza kusema kilichofanyika sasa hivi ni kitu kikubwa sana, siyo kwa Idris peke yake, bali ni kwa Watanzania wote na waigizaji wote kwa jumla.

 

IJUMAA WIKIENDA: Mliweza vipi kuwashawishi Netflix hadi wakakubali kufanya kazi na Idris?

 

ULIMWENGU: Tumekuwa tukiwashawishi sana Netflix kwamba Tanzania kuna soko kubwa la filamu kwa sababu kuna watu wengi sana wanaozungumza Kiswahili na kujaribu kuwaonesha kwamba contents (maudhui) ya Kitanzania pia wakiyachukua yanaweza kuwasaidia wao kupata subscribers (wafuasi) kutoka nchi zote zinazozungumza Kiswahili, hivyo ilikuwa ni safari ndefu ya kuwashawishi, lakini mapokezi ya Watanzania wote kwa jumla yamefanyika kuanzia Aprili 26 (mwaka huu); siku ambayo ndiyo walianza rasmi kuonesha hiyo Muvi ya Slay.

 

IJUMAA WIKIENDA: Mapokezi ya Watanzania yalikuwa makubwa sana, hii imewapa tafsiri gani?

 

ULIMWENGU: Kiukweli haya mapokezi yamefanya hata sisi kule tuonekane kweli Tanzania kuna soko, kweli Tanzania ni sehemu ambayo tunatakiwa kuiangalia kwa jicho la pili na siyo tu kuipita, kwa hiyo imekuwa ni ishu kubwa sana na hivi tunavyoongea Slay ni namba moja kwenye ‘trending’ za Netflix.

 

IJUMAA WIKIENDA: Baada ya hii muvi kutoka na mapokezi makubwa waliyoyapata kutoka kwa Watanzania, unahisi huko mbeleni tunaweza tena tukaibuka kidedea?

 

ULIMWENGU: Kwa sasa macho yao yapo Tanzania na sisi tunapokea simu nyingi tangu juzi za pongezi, hata kutoka Netflix ya SA (South Africa), tumepokea simu za mialiko mbalimbali ambayo mpaka sasa Idris amepata. Kwa hiyo hii imefungua njia kubwa sana na kwa Watanzania wengine, hivyo nina uhakika hata sasa hivi wao wenyewe watakuwa wameanza ku-review contents mbalimbali za Tanzania.

 

IJUMAA WIKIENDA: Salamu za pongezi kwa Idris zimekuwa nyingi sana, kuanzia kwa wasanii wenzake, mashabiki mpaka viongozi mbalimbali serikalini wakiongozwa na Rais wa Awamu ya Nne, Dk Jakaya Mrisho Kikwete ‘JK’ ambaye ali-tweet na kumpongeza, wewe kama meneja ulijisikiaje?

 

ULIMWENGU: Ni kitu kikubwa sana kwetu na tumefarijika mno, unajua muda mwingine mnafanya kazi kwenye mazingira magumu, lakini kwa kuwa tunajua malengo tunajipa moyo kwamba italipa, kwa hiyo inapotokea kwamba hadi viongozi wa nchi wanaona zile jitihada na kuzipongeza, ni zaidi ya malipo yote ambayo mtu angeweza kutulipa kipesa. Pia inatupa moyo sisi wa kuweza kuendelea na kupambana zaidi.

 

IJUMAA WIKIENDA: Mlijisikiaje baada ya Netflix kupitia akaunti yao ya Instagram na kumtambulisha Idris kama Raia wa Kenya badala ya Tanzania?

 

ULIMWENGU: Ni suala ambalo sisi kama Watanzania sasa hivi ndiyo tunalifanyia kazi, kuweza kutambulisha watu wetu, unajua kuna nchi nyingine huko nje wakisikia mtu anaongea Kiswahili wanajua ni Mkenya, kwa hiyo kwetu sisi ni changamoto na Serikali inatakiwa ihakikishe tunaitangaza sana lugha yetu ya Kiswahili.

 

IJUMAA WIKIENDA: Hebu tuibie siri kuhusu mamilioni aliyoyapiga Idris kwenye huu mchongo, yamekaaje?

 

ULIMWENGU: Malipo yake ni mazuri zaidi kwa sababu ile ni global platform (jukwaa la kimataifa), ni platform kubwa, ni platform ya duniani na malipo yake yanakuwa tofauti ukizingatia Idris hapa nyumbani anaweza akafanya kazi na mchekeshaji yeyote, lakini huko nje, Idris ni staa wa Afrika.

 

IJUMAA WIKIENDA: Tutegemee nini sasa hivi kutoka kwa Idris?

ULIMWENGU: Sasa hivi tutegemee vitu vingi tu kutoka kwake, kuna mambo mengi bado yapo jikoni.

Hii ni mara ya pili kwa Idris kulamba shavu la kimataifa na kujizolea mamilioni ya pesa.

Makala: MEMORISE RICHARD

Leave A Reply