Meya Dar Akubali Yaishe, Afuta Kesi Mahakamani – Video

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeifuta kwa gharama kesi ya Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita,  ya kutaka kusitisha mchakato wa kumuondoa madarakani.

 

Hatua hiyo inatokana na Mwita kuwasilisha maombi hayo kupitia Wakili wake, Hekima Mwasipu,  mbele ya Hakimu Mkazi, Janeth Mtega.

 

Mwasipu ameieleza mahakama kwamba miongoni mwa sababu zao ni kwamba anaona kesi hiyo haina maana kuwepo mahakamani kwa sababu hatua za kumng’oa madarakani zilishafanyika.

 

Pia, muombaji (Mwita) hakupewa nafasi ya kusikilizwa mahakamani, hivyo anaomba kuliondoa shauri hilo bila gharama.

 

Hata hivyo, Wakili wa Serikali, Rashid Mohammed, amedai kuwa hawana pingamizi na maombi hayo ila wanaomba suala la gharama liwepo kwa sababu wamepoteza muda, rasilimali na uandaaji wa majibu kuhusu shauri hilo.

 

Akijibu hoja hizo, Mwasipu amedai kuwa wanaomba gharama zisiwepo kwa sababu mawakili wa serikali wanatumia kodi za wananchi, hivyo meya naye ni mwananchi na analipa kodi.

 

Akitoa uamuzi, Mtega amesema anakubaliana na maombi ya muombaji (Mwita) ya kuliondoa shauri hilo, hivyo akaliondoa kwa gharama.

 

Katika kesi hiyo ya madai,  Meya Mwita alikuwa anaomba kusitisha mchakato wa kutaka kuondolewa madarakani moja kwa moja kwa sababu umekiuka kanuni za jiji na hata sababu hazina msingi,  ikiwemo matumizi mabaya ya gari.

MEYA WA JIJI LA DAR ALIONDOA SHAURI LAKE MAHAKANI, ASEMA HANA NIA NA KUENDELEA NA KESI

Toa comment