The House of Favourite Newspapers

Mfahamu Zaidi Mrithi wa Maalim Seif

0

 

WAZANZIBARI na Watanzania kwa ujumla kwa sasa wameelekeza macho na masikio kwa raisi wa Zanzibar, Dkt Hussein Mwinyi wakisubiri amtangaze Makamu wa Kwanza wa Rais wa visiwa hivyo.

 

 

Tayari uongozi wa chama cha ACT Wazalendo umeshapendekeza jina la mwananachama wake atakayerithi nafasi hiyo iliyoachwa wazi kufuatia kifo cha Maaalim Seif Sharif Hamad.

 

 

Baada ya hatua hiyo, inategemewa rais Mwinyi kumteua rasmi kiongozi huyo kama inavyobainisha Katiba ya Zanzibar katika ibara ya 40 (1).

 

 

Tarehe 17 Februari, Rais Dkt. Hussein Mwinyi alitangaza kifo cha makamu wake wa kwanza, Maalim Seif Sharif Hamad kupitia runinga ya taifa ya ZBC. Kifo hicho kilikuja takriban wiki tatu tangu Maalim atangaze kuugua Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO-19).

 

 

Kwa kuwa chama cha ACT-Wazalendo kilipata asilimia 19 ya kura za urais na kushika nafasi ya pili katika uchaguzi wa Oktoba mwaka jana. Chama hicho kinaendelea kuwa na haki ya kuwa na Makamu wa Kwanza wa Rais katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).

 

 

Mwinyi na nani?

Baada ya uchaguzi wa mwezi Oktoba uliogubikwa na ghasia na madai ya wizi wa kura kutoka upinzani Dkt. Mwinyi alionesha nia ya kutaka uwepo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Hata baada ya kifo cha Maalim, Mwinyi ameendelea kudhihirisha nia ya kuyaendeleza matakwa ya kikatiba.

 

 

Kuthibitisha hilo, Februari 26 katika msikiti wa Raudhwa, aliwaomba waumini wa Kiislam kumuomba Mungu apatikane kiongozi mwenye nia njema na dhamira njema kwa Zanzibar kama Maalim Seif.

 

 

Kwa upande wa ACT Wazalendo, Ijumaa ya wiki iliyoisha, kamati ya uongozi ya chama hicho ilifanya vikao vyake vya ndani.

 

 

Ajenda kuu ilikuwa ni kulichagua na kuliwasilisha jina la mrithi wa Maalim kwa Rais wa Zanzibar. Taarifa zinaeleza, tayari kazi hiyo imekamilika na sasa anasubiriwa Dkt. Mwinyi kulitangaza jina hilo.

 

 

Litatangazwa jina moja tu. Ingawa upepo wa mambo na habari za chini ya kapeti, jina hilo litatoka miongoni mwa vigogo hawa watano wa chama hicho:

 

 

Othman Massoud

Aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) chini ya Dkt. Ali Mohammed Shein. Wadhifa huo ulifikia tamati Oktoba 2014 baada ya kuenguliwa.

 

 

Sura yake sio maarufu katika siasa za upinzani lakini tangu afukuzwe ndani ya SMZ, amekuwa maarufu kwa misimamo yake ya kutetea maslahi ya Zanzibar katika Muungano.

 

 

Wakati wa pirikapirika za uchaguzi mkuu alikuwa mjumbe katika kamati ya ilani ya chama cha ACT Wazalendo kwa upande wa Zanzibar.

 

 

Mansour Yusuf Himid

Chini ya Dkt. Shein, Himid alikuwa Waziri asiyekuwa na Wizara Maalum kabla ya kuachishwa kazi hiyo Oktoba 2012. Pia aIiwahi kuwa Mwakilishi wa jimbo la Kiembesamaki kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM).

 

 

Mgogoro wa kimsimamo na chama chake juu ya Zanzibar na Muungano, ulisababisha afukuzwe CCM mnamo Agosti 2013. Baadaye alihamia Chama cha Wananchi (CUF), kabla ya wimbi la ‘ulipo tupo’ kumburuta hadi ACT Wazalendo. Toka alipoahamia upinzani, Himid amekuwa mshauri maalumu wa Maalim Seif mpaka alipofikwa na mauti.

 

 

Juma Duni Haji

Ni mkongwe wa umri na katika siasa za Zanzibar, kwa lakabu ya Babu Duni. Kwa sasa ndiye makamu mwenyekiti wa ACT Wazalendo Zanzibar.

 

 

Amewahi kuwa Mwakilishi wa kuteuliwa na kuchaguliwa katika Baraza la Wawakilishi kupitia CUF na Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano katika serikali ya kwanza ya Umoja wa Kitaifa (2010-2015). Babu Duni pia alikuwa mgombea mwenza wa urais wa Edward Lowassa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

 

 

Ismail Jussa Ladhu

Ukiuliza juu ya watoto wa Maalim kisiasa, huwezi kuacha kulitaja jina la Ismail Jussa. Amekuwa bega kwa bega katika harakati zote za kisiasa na Maalim kwa miongo mitatu iliyopita.

 

 

Kwa sasa ni mjumbe wa kamati kuu ya chama cha ACT Wazalendo. Amewahi kuhudumu kama Mwakilishi wa CUF jimbo la Mji Mkongwe.

 

 

Katika uchaguzi uliopita ni mmoja wa wanasiasa wa ngazi ya juu walioshambuliwa vibaya na vikosi vya usalama tarehe 29 Oktoba, dakika chake baada ya chama chake kutangaza maandamano ya kupinga ushindi wa Dkt. Mwinyi.

 

 

Nassor Ahmed Mazrui

Pia ni mwanasiasa aliyekumbwa na misukosuko katika uchaguzi uliopita. Chama chake kilifanya juhudi kubwa kumsaka na wanachama wengine baada ya kutoa taarifa za kutekwa.

 

 

Ni naibu Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo Zanzibar na mwakilishi katika Baraza la sasa la Wawakilishi baada ya kuteuliwa. Amewahi kuwa Waziri wa biashara, viwanda na masoko katika serikali ya kwanza ya umoja wa kitaifa akiwa CUF.

 

 

Jibu la kitendawili hiki sasa kipo mikononi mwa Rais Mwinyi. Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla, wanasubiri siku kama sio masaa ya jina la mmoja wao kutangazwa, kisha kuapishwa na kuanza majukumu yake.

 

 

Nini maana ya kuwa mrithi wa Maalim?

Rais wa sasa wa Marekani, Joe Biden amekuja na msemo wake, ‘Marekani Imerudi.” Ni baada ya taifa hilo kupotea katika siasa na sera za mtangulizi wake Donald Trump, ambazo hazikuwa rafiki kwa mataifa mengi.

 

 

Hata kwa Zanzibar, si dhambi kusema ule ‘Ustaarabu wa Waswahili,’ sasa unaonekana kurudi polepole. Ustaarabu ambao ulipotea kwa sababu ya dhulma kwa misingi ya kisiasa, dhulma zilizozalisha chuki katika jamii.

 

 

Kwa Wazanzibari wengi hawategemei mrithi ajae wa Maalim aje na urithi jina tu, bali ni urithi wa kivitendo wa kuyaendeleza yale mazuri Maalim aliyoyaacha akishirikiana na Mwinyi. Hasa hili la mshikamano na maridhiano ya Wazanzibari.

 

 

Jioni ya tarehe 28 Febuari, timu ya makada kutoka CCM ilikwenda katika ofisi za ACT Wazalendo, Zanzibar kutoa pole rasmi kwa msiba wa Maalim Seif.

 

 

Kwa wanaozijua siasa za Zanzibar na uhasama wa muda mrefu uliokuwepo, kususiana mazishi na harusi. Tukio lile liliashiria muujiza wa kisiasa, muujiza ambao umekuja kwa sababu ya maridhiano yaliyopo.

 

 

Yamkini huu ndio mwanzo wa kufukiwa kwa sintofahamu za kisiasa zilizokuwepo tangu baada ya Mapinduzi ya Januari 1964. Sintofahamu ambazo daima zilizalisha makovu, mateso, majeruhi, wakimbizi na vifo.

 

 

Punde safari inaanza kwa ngwe ya kisiasa bila Maalim. Matarajio ya walio wengi, ni kuzidi kuiona Zanzibar mpya bila chuki za kisiasa, bila ubaguzi katika utoaji wa ajira, bila ya vifo na majeruhi wakati wa uchaguzi.

Leave A Reply