Miaka Minne Ndani ya Mapango ya Amboni – 30

ILIPOISHIA

“Wenzetu watatu wameshakufa” nikamwambia.

 “Ninaamini kuwa nyinyi mtapona. Safari hii mkiondoka mhakikishe kuwa mnatoka ndani ya pango hili.”

 “Tatizo ni hizi njia, zinatutatiza sana.”

 SASA ENDELEA…

Tutakapofika pale kwenye njia mbili tushike  ile njia ya upande wa kushoto, ile ya upande wa kulia inaturudisha huku huku,” nikawaambia wenzangu.

“Kama mmeshajua hivyo mhakikishe mnafuata njia sahihi,” Faiza akatuambia.

“Nadhani kwa leo hatutaweza kuondoka. Hii miguu ilivyovimba sidhani kama nitaweza kutembea.”

“Lakini maumivu si yamepungua?” Faiza akaniuliza.

“Maumivu yamepungua kidogo lakini nitakapoanza kutembea naamini yatarudi upya.”

“Una maana kuwa leo tutalala hapa?” mwenzetu mmoja akaniuliza.

“Kama itabidi mlale mnaweza kwenda kulala sehemu nyingine mbali kidogo na hapa,” Faiza akatuambia.

“Sasa huo mwendo!” nikang’aka.

“Pale utakapoona huwezi kuendelea kutembea ndipo mnaishia hapo hapo,” Faiza aliendelea kutupa nasaha.

“Ninaamini miguu yangu itauma sana.”

“Sasa mtafanyaje?”

Nikawatazama wenzangu. Na wao walikuwa wakinitazama. Hakukuwa na aliyekuwa na jibu.

Siku ile tulishinda pale pale. Ilipofika jioni Faiza alitupa chakula. Tulipokula tukamwambia tunaondoka.

Faiza alitusindikiza na mwenge wake hadi mbali kidogo ambapo tuliweka makazi yetu. Palikuwa na sehemu nzuri ya kupumzika.

“Inabidi tubaki hapa. Miguu haikubali tena kwenda,” nikasema.

“Nyinyi bakini hapa. Naamini hapa mnaweza kuwa salama. Mtakapojisikia vizuri mnaweza kuendelea na safari,” Faiza akatuambia.

Hatukuzungumza naye sana Faiza akaondoka. Alisindikizwa na mwenzetu mmoja. Baada ya kama nusu saa hivi mtu huyo alirudi akiwa ameachiwa ule mwenge.

“Nimemuacha njiani. Ameniambia anaweza kuendelea kwenda mwenyewe,” akatuambia.

Mtu huyo aliuchomeka mwenge huo kwenye tundu kando kidogo na mahali tulipokuwa tumeketi, akaja kukaa na sisi.

Tulikuwa watu wawili ambao miguu yetu ilikuwa imevimba. Ule mwendo mdogo tuliokwenda uliturudishia maumivu upya. Kila mmoja akawa anaichua miguu yake.

Tulihisi tungeweza kukaa pale kwa siku mbili kabla ya kuanza tena safari. Tatizo ni kuwa hatukuwa na chakula cha akiba wala maji.

“Kama Faiza atatukumbuka atatuletea chakula,” nikawaambia wenzangu.

Tukakaa pale kwa siku mbili. Faiza hatukumuona. Njaa haikuwa tatizo kwetu isipokuwa kiu ya maji. Mimi na mwenzangu mmoja tukaamua kwenda kwa Faiza kufuata maji.

Tukaenda na ule mwenge. Tulitembea mwendo wa taratibu sana. Miili yetu haikuwa na nguvu isitoshe miguu ilikuwa inauma.

Tukafika katika lile eneo analokaa Faiza.

Nikamwambia mwenzangu aingie yeye kwanza kuchunguza usalama.

“Ingia kimyakimya uchunguze, kama utagundua Faiza yuko peke yake uje uniambie,” nikamwambia.

Yule mwenzangu akaingia. Ule mwenge nilibaki nao mimi. Alinyata hadi mahali palipokuwa na pazia akalipenua na kuchungulia ndani kisha akaingia.

Nikauchomeka ule mwenge kwenye tundu kisha nikamfuata. Nilipenua lile pazia nikamchungulia. Nilimuona amesimama mbele ya pazia jingine lililokuwa kwenye sehemu (chumba) aliyokuwa akikaa Faiza.

Nilimuona ametega sikio kwenye pazia kisha akaanza kuita kwa sauti ya chini.

“Faiza!  Faiza!”

Ghafla nikamuona Faiza akitoka.

“Umefuata nini, si mlikwishaondoka?” Faiza akamuuliza huku akiwa amekunja uso wake.

Kabla ya yule mtu kumjibu Faiza akaongeza.

“Ondoka haraka. Kaikush anakuja.Chupa imeanza kuingia moshi. Tangu aanze kusikia harufu za watu humu ndani anakuja mara kwa mara.”

“Tulikuwa tumefuata maji ya kunywa lakini acha tuondoke.”

Hapo hapo pazia likapenuliwa tena. Akatokea mtu ambaye mwenzangu alitaka kumkimbia lakini hakuwahi.

Alikuwa Kaikush aliyekuwa amevaa kanzu na kilemba kama Muarabu. Kanzu yake ilikuwa ni ileile iliyochafuka na kujaa madoa ya damu.

Faiza alipomuona aligwaya. Yule mwenzangu aliyekuwa ameshageuka akimbie alishikwa ukosi.

“Wewe nani?” Sauti ya Abdallah Kaikush ikavuma kama iliyokuwa imewekewa kipaza sauti.

“Mimi… mimi…!” Maskini yule mtu alianza kubabaika. Maneno yakawa hayamtoki.

“Hivi nyinyi mnamfuata nani humu?” Kaikush alimuuliza.

Deogratius Mongela na Chande Abdallah

Loading...

Toa comment