The House of Favourite Newspapers

The World You Left Behind

0

Ajali mbaya na ya kutisha inatokea kwenye Makutano ya Barabara za Morogoro na Msimbazi, katikati ya Jiji la Dar es Salaam. Gari la Mheshimiwa Abbas Magesa, Range Rover Evoque linagongwa na lori la mafuta na kuteketea kabisa.

Baadaye mwili wa Magesa unazikwa kwa heshima zote za kiserikali lakini utata mkubwa unaugubika msiba wake kwani mkewe haoneshi kuguswa hata kidogo na kilichotokea.

Upande wa pili, historia ya wanandoa hao inaelezewa ambapo mgogoro mzito unaibuka kati yao na kusababisha mpasuko mkubwa kwenye ndoa hiyo. Sehemu nyingine, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali, CAG Daniel Mwampashi anakutwa amekufa nyumbani kwake muda mfupi kabla hajawasilisha ripoti ya ukaguzi wake.

Kabla hilo halijaisha, Magesa anajikuta akiangukia kwenye mikono ya mwanamke aitwaye Grace ambapo wawili hao wanapigwa picha za utupu wakiwa hotelini. Magesa anatakiwa kutoa shilingi milioni hamsini ili picha zake za utupu zisivujishwe.

Anahangaika na hatimaye anazipata fedha hizo, anafunga safari ya kuelekea Msitu wa Kazimzumbwi, Kisarawe mkoani Pwani alikoelekezwa kuzipeleka ambako ananusurika kuuawa.

Baadaye Grace, mwanamke aliyemwambia kwamba anazo taarifa juu ya wauaji wa Mwampashi anakutana na Magesa hotelini ambapo mbali na mambo mengine wawili hao wanajikuta wakiangukia dhambini.

Inabaki kidogo mke wa Magesa agundue kwamba mumewe ametoka kumsaliti lakini mwanaume huyo anatumia mbinu za hali ya juu kumlaghai.

Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Ilibidi Magesa amueleze ukweli Kamanda Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jamal Kahungo kuhusu kila kitu kilichokuwa kinaendelea. Hata hivyo, bado kuna mambo kadhaa hakuyaweka wazi likiwemo la uhusiano wake wa kimapenzi na Grace.

Akamueleza pia na maelezo yote aliyopewa na mwanamke huyo kuhusu mhusika wa mauaji ya mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za serikali, CAG Mwampashi.

“Una uhakika na unachokizungumza?”

“Hicho ndicho nilichoelezwa na Grace na sina sababu ya kutomuamini.”

“Mh! Mbona mambo mazito? Hata sijui nitaanzia wapi.”

“Najua unaweza kufanya kazi na kuibua ukweli, nimeakuamini ndiyo maana nimekueleza, nakuomba sana usiniangushe.”

“Usijali ila nitahitaji kuendelea kuwasiliana na wewe kwa karibu sana, naamini tukishirikiana tunaweza kuifanya sheria ikafuata mkondo wake,” alisema Jamal Kahungo, mpelelezi aliyebobea kwenye kazi hiyo, Magesa akashusha pumzi ndefu na kushikana naye mkono.

Angalau alijihisi ahueni kubwa ndani ya moyo wake, ule mzigo mzito aliokuwa ameubeba ndani ya moyo wake sasa alijihisi kuutua. Baada ya mazungumzo hayo, ilibidi Magesa aende ofisini kwake kuendelea na kazi huku akimuomba Kahungo awe anampa maendeleo yote kuhusu msiba wa msichana huyo.

Hata alipofika ofisini kwake, Magesa alishindwa kabisa kufanya kazi, kila alipokuwa anamfikiria Grace, alikuwa hataki kabisa kuamini kwamba mwanamke huyo mrembo ameshaiaga dunia. Kuna wakati alikuwa akishtukia machozi yakimtoka bila mwenyewe kupenda, kifo cha Grace kilikuwa ni zaidi ya pigo kwake.

Baadaye alishindwa kabisa kuendelea na kazi, ikabidi aondoke na walinzi wake na kurudi nyumbani kwake ambako nako hakutaka mazungumzo na mtu yeyote, akapitiliza na kwenda kulala.

“Vipi mume wangu, unaumwa?” Vivian alimuuliza mumewe baada ya kumuona hayupo kwenye hali ya kawaida.

“Najisikia vibaya mke wangu, nimeona bora nipumzike.”

“Ooh! Pole, vipi mmefikia wapi na suala la msiba?”

“Bado upelelezi unaendelea kuhusu wahusika wa kifo chake, nafikiri mpaka kesho ndiyo taratibu za mazishi zitakapoanza.”

“Poleni, halafu nilitaka kukuuliza, ulisema mlikuwa mnafanya naye kazi, mbona nimesikiliza taarifa ya habari haielezi kwamba amewahi kufanya kazi serikalini?” Vivian alimuuliza mumewe swali ambalo lilimfanya Magesa ashtuke sana.

Hakuwahi kufikiria kama mkewe anaweza kuendelea kufanya udadisi wa kiasi hicho kuhusu Grace, kengele ya hatari ikalia ndani ya kichwa chake.

“Inawezekana wamekosea, mbona kila mtu anamfahamu?” alisema Magesa huku akigeukia ukutani, hakupenda kuendelea kuizungumzia mada hiyo kwani alihisi mkewe anaweza kushtukia mchezo, jambo ambalo hakuwa tayari kuona linatokea.

Siku hiyo ilipita, kesho yake ndugu wa mwanamke huyo walikabidhiwa mwili kwa ajili ya taratibu za mazishi, Magesa akawa anataarifiwa kila kitu kilichokuwa kinaendelea. Kwa jinsi alivyotokea kumpenda mwanamke huyo, alitamani awepo mpaka kwenye mazishi yake lakini alishindwa kufanya hivyo kutokana na sababu mbalimbali.

Alichoweza kukifanya, ni kwenda kutembelea kaburi lake siku kadhaa baadaye ambapo alitoa salamu zake za mwisho na kulia kwa uchungu wa hali ya juu.

MIEZI MITATU BAADAYE

Magesa akiwa ofisini kwake, alishangaa kuona namba ngeni ikiingia kwenye simu yake. Kama ilivyokuwa kawaida yake, kutokana na tishio la kuuawa, hakuwa mwepesi kupokea namba za simu asizozijua, simu ikaita mfululizo lakini hakuwa tayari kupokea.

Alipoona inaendelea kuita kwa fujo, ilibidi aipokee huku akiwa makini kutaka kujua ni nani aliyekuwa anampigia.

“Haloo!”

“Haloo Mr. Magesa, najua utashtuka kusikia sauti hii lakini nakuomba unisikilize kwa makini.”

“Kwani wewe ni nani?”

“Ni mimi Grace, najua unaamini kwamba nilikufa.”

“Grace? Grace yupi?”

“Nisikilize Magesa, mimi sikufa kama watu walivyoaminishwa lakini ni kweli kuna mpango ulikuwa umeandaliwa kwa ajili ya kunimaliza, yaani ni Mungu tu, siwezi kuzungumza na wewe kwa simu naomba tukutane ana kwa ana, niambie lini utakuwa na nafasi.”

“Grace, ni wewe kweli au naota? Sitaki kuamini, siamini kabisa.”

“Ni mimi Magesa, labda ukiniona utaamini.”

“Sasa yule aliyekufa na kuzikwa ni nani? Mimi nimefika mpaka kwenye kaburi lako, siamini.”

“Usijali Magesa, tukionana utapata majibu ya maswali yako yote.”

Magesa haamini kama Grace yuko hai. Je, nini kitafuatia? Usikose Ijumaa kwenye Gazeti la Uwazi Mizengwe.

Leave A Reply