Mjukuu Amkatakata Bibi Yake kwa Shoka na Kumuua

Kijana mwenye matatizo ya akili, Steve Olumbe amemvamia, kumkatakata kwa mapanga na shoka kisha kumuua bibi yake, Priscilla Were mwenye umri wa miaka 70, katika tukio lililotokea Desemba 7, 2021 katika Kijiji cha Ruga, Kaunti ya Homabay nchini Kenya.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, kijana huyo ambaye alikuwa akiishi na bibi yake huyo tangu akiwa mdogo baada ya mama yake kufariki, alifunga kwa ndani mlango wa chumba alichokuwa akiishi bibi yake kisha kumkata kwa panga, alipodondoka chini ndipo alipommalizia kwa kumkata na shoka.

Baada ya kufanya ukatili huo, kijana huyo alitoka na kufunga mlango kwa nje, lakini alipogundua kwamba mjukuu mwingine wa mwanamke huyo amegundua alichokifanya, alijaribu kumuua lakini akafanikiwa kutoroka na kwenda kutoa taarifa kwa majirani.

Kamanda wa Polisi Kaunti ya Homabay, Ester Seroney amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kwamba baada ya kufanya ukatili huo, kijana huyo alienda kwenye zizi la mifugo na kuwaua ng’ombe watatu, mbuzi watano na kumjeruhi punda mmoja kisha alijaribu kutoroka.

Akiwa njiani kutoroka, kijana huyo alitiliwa mashaka na maafisa usalama walioshangazwa na jinsi nguo zake zilivyokuwa zimelowa kwa damu, wakaanza kumfuatilia na kwa msaada wa madereva bodaboda katika kituo cha mabasi cha Homa Bay, walifanikiwa kumkamata na kumfikisha katika Kituo cha Polisi cha Homabay ambako anaendelea kushikiliwa huku uchunguzi zaidi ukiendelea.

Inazidi kuelezwa kuwa, kijana huyo mbali na kuwa na matatizo ya akili, alikuwa pia na ugonjwa wa kifafa ambao bibi yake ndiye aliyekuwa akimsaidia kufuata dawa hospitali mara kwa mara.3403
SWALI LA LEO

Kupanda Kwa Bei ya Mafuta Nchini, Nini Kifanyike Kupunguza Bei?
Toa comment