The House of Favourite Newspapers

Mkataba wa Metacha Wawekwa Kiporo Yanga SC

0

VINARA wa Ligi Kuu Bara Klabu ya Yanga, wanajiandaa kuanza mazungumzo ya kumpa mkataba mpya mlinda mlango wao, Metacha Mnata mara tu watakapokamilisha utaratibu wa kuunda upya benchi lao la ufundi.

 

Hivi karibuni kumekuwa na taarifa kuwa kipa huyo anawindwa na watani zao wa jadi klabu ya Simba, na Yanga wanataka kuhakikisha hawarudii makosa kwa kumpa mkataba mpya mapema iwezekanavyo.

 

Mlinda mlango huyo aliuanza vizuri msimu huu ambapo aliweka rekodi ya kucheza michezo 11 bila kuruhusu bao yaani ‘Clean Sheet’, kabla ya kuruhusu mabao matano kwenye michezo mitatu ya mwisho aliyoichezea Yanga dhidi ya Mbeya City, Kagera Sugar na Polisi Tanzania.

Akizungumza na Championi Jumamosi,Kaimu Katibu Mkuu wa Klabu ya Yanga, Haji Mfikirwa alisema: “Ni kweli tulipata nafasi ya kukutana na meneja wa Metacha, ambaye ni Jemedari Said, lakini mazungumzo yetu kwa kiasi kikubwa yalihusiana na kumaliza tofauti zilizotokea kati ya mchezaji na klabu baada ya mchezo dhidi ya Polisi Tanzania.

 

“Lakini watu wanapaswa kutambua kuwa Metacha bado ana mkataba na Yanga mpaka mwishoni mwa msimu huu, na uongozi wa klabu yetu ulijikita ukimaliza mahitaji ya benchi la ufundi ili kuanza kushughulikia mazungumzo ya mkataba mpya na Metacha.

 

Naye Meneja wa Metacha, Jemedari alisema: “Sisi kama upande wa mchezaji, wala hatuna tatizo lolote na Yanga, Metacha ni mchezaji wa Yanga mpaka mwisho wa msimu na kabla ya kusikiliza ofa ya timu yoyote itakayohitaji huduma yake tutawasikiliza Yanga na kuangalia kama ofa yao itafaa basi tutasaini mkataba mpya.”

Stori na Joel Thomas, Dares Salaam

Leave A Reply