The House of Favourite Newspapers

MKE ADAI KUCHOMWA KWA PASI NA MUMEWE

FARIDA Angelo (24) ni mkazi wa Gongo la Mboto jijini Dar ambaye ameibuka na kuangua kilio mbele ya gazeti hili akidai kuchomwa kwa pasi ya umeme ya kunyooshea nguo na mumewe na kumsababishia majeraha mwilini.

Kwa mujibu wa mwanamke huyo, tukio hilo lilijiri nyumbani kwa wawili hao, Gongo la Mboto jijini Dar, majira ya asubuhi ambapo mwanaume huyo alitoweka ambapo sasa anasakwa kwa RB namba STRB/8533/2018 iliyosomekana kosa la KUDHURU MWILI.

Akilisimulia Ijumaa Wikienda mkasa huo, Farida alisema kuwa, sababu ya mumewe kumfanyia hivyo ni baada ya mtoto wake wa kike kumwambia baba yake kwamba, asubuhi ya siku hiyo kuna mgeni wa kiume aliyefika nyumbani hapo.

Alisema kuwa, ni kweli alifika mgeni ambaye ni dereva wa wazazi wa mwanaume huyo ambaye walikuwa wanasalimiana baada ya kutoonana kwa muda mrefu, jambo ambalo mumewe alifikiria tofauti (alijua kuna usaliti) ndipo akafanya kitendo hicho cha kinyama ambapo alimchoma mkononi. “Mimi na huyu mwanaume tulifunga ndoa ya Kiislam mwaka 2010.

“Wazazi wake hawakunikubali, lakini yeye aling’ang’ania kunioa kwa sababu alikuwa ananipenda. Lakini baada ya ndoa mambo yalibadilika hadi akawa harudi nyumbani kwani wakati huo alikuwa anaendesha magari ya mafuta. “Wakati anafanya hivyo mimi nilikuwa na mtoto mdogo, sikuweza kumuuliza maana alikuwa mkali. “Kuna kipindi mateso yalikuwa makali hadi nikaondoka nikaenda kupanga chumba Ubungo (Dar).

“Baadaye majirani (kule Gongo la Mboto) walinipigia simu wakaniambia wanangu wanateseka mno na mume wangu naye alinipigia ndipo nikarudi. “Kweli niliwakuta wanangu wana hali mbaya sana. Nikajua labda mume wangu atakuwa amejifunza na amebadilika, lakini haikuwa hivyo.

“Nilishawahi kumpeleka Polisi mwaka 2014, nakumbuka alinipiga na mbao yenye misumari kichwani, lakini ndugu zake walinimbeleza nifute kesi, tukayamaliza nyumbani. “Sasa hili tukio la juzi ni kiboko, yule mgeni ambaye ni dereva wa wazazi wake alikuwa ananishangaa kutokana na maisha maisha ya hapa nyumbani kuwa magumu.

“Kumbe mwanangu alielewa vibaya, aliporudi baba yake akamwambia kuwa anko alikuja, baba yake akamuuliza anko gani, akajibu sijui ni mgeni wake mama. “Hapo ndipo ugomvi mkubwa ukaanza usiku, kulipokucha akaenda kuchukua pasi akaichomeka kwenye moto na kunichoma mkononi na kama sikuikwepa ilikuwa inatua usoni.

“Baada ya hapo ndipo nikaenda kuripoti Polisi ambapo nilipewa RB namba STRB/8533/2018- KUDHURU MWILI ambapo mume wangu sasa anasakwa kwa kosa hilo,” alimalizia kusimulia farida. Ijumaa Wikienda lilifika kwa wazazi wa mwanaume huyo na kupewa taarifa kuwa haijulikani alipo.

STORI: Shamuma Awadhi, DAR

Comments are closed.