The House of Favourite Newspapers

Mkuki moyoni mwangu – 34

2

CATARINA amefanikiwa kuingia katika ulimwengu wa uanamitindo na ndoto yake kutimia lakini ghafla anafanyiwa kitendo cha kinyama na tajiri kijana Jackson Motown, mpango wote huo ukisukwa na Craig Anderson na baadaye kumwomba Catarina msamaha bila mafanikio.
Akiwa katika machungu hayo anapata taarifa kwamba wanahitajika kwenda nchini Ufaransa kwenye shoo ya mbunifu maarufu duniani, Mario Pizaro, moyo wake unafurahi na kuapa kwamba huko angetafuta wakala mwingine kujitoa mikononi mwa Craig Anderson.
Je, nini kitaendelea? Atafanikiwa?

SONGA NAYO…

HAKUAMINI macho pale miguu yake ilipoikanyaga ardhi ya Ufaransa kwenye Uwanja wa Ndege wa Charles De Gaulle jijini Paris, ilikuwa ni kama anaota, akamshukuru Mungu kwa kumpa uzuri ambao hakuulipia gharama yoyote, uliosababisha yeye hatimaye kuingia kwenye jiji ambalo siku zote alilisoma tu kwenye ramani.
Walikuwa ni jumla ya wanamitindo kumi, kiongozi wa msafara akiwa ni Craig Anderson ambaye mpaka wanafika mwisho wa safari uhusiano wake na Catarina ulikuwa bado una ukakasi, moyoni mwake alimchukia, picha ya siku aliyozinduka usingizini na kukuta amepoteza bikira aliyoitunza kwa ajili ya Kevin, bado ilimwijia kichwani mwake na kumfanya ahisi hasira.
Nje ya uwanja wa ndege walipokelewa na Mario Pizaro, ambaye walikuja nchini humo kwa ajili ya kuvaa nguo alizozibuni, macho yake yalipogongana na ya Catarina butwaa lilionekana waziwazi, alikuwa katika hali iliyowakuta watu wote waliokutana na Catarina kwa mara ya kwanza, akawa anamwangalia kuanzia chini hadi juu na kupandisha tena akionyesha kusahau kabisa kulikuwa na warembo wengine eneo hilo.
“I am tantalized to witness what will happen tomorrow!”(Nimetiwa shauku kushuhudia kitakachotokea kesho!)
“By what?” (Na nini?) Craig akamuuliza.
“This girl’s beauty! What is your name?”(Uzuri wa msichana huyu! Jina lako nani?)
“I am Catarina, they call me Cat!”(Naitwa Catarina, rafiki zangu huniita Cat!)
“You are a really cute Cat girl, in Paris to make incredible Cat walks on stage tomorrow!”(Hakika wewe ni paka mzuri! Uko hapa Paris kutembea mitembeo mizuri ya paka jukwaani kesho!) aliongea Mario Pizaro kwa utani.
Mario Pizaro alikuwa ni Kijana wa Kiitaliano aliyefanikiwa sana kwenye ulimwengu wa mitindo, akimiliki maduka makubwa katika miji ya Paris, Milan, New York na Los Angeles. Kwenye umri wa miaka thelathini na nne tu, tayari alikuwa miongoni mwa mamilionea walioheshimiwa katika kazi ya ubunifu wa mitindo.
Aliwachukua kutoka uwanja wa ndege hadi katikati ya Jiji la Paris kwenye hoteli kubwa ya Ritz iliyomilikiwa na Mohammed Al- Fayed baba wa Dodi Fayed aliyewahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Princess Diana ambaye walikufa naye pamoja katika ajali mbaya ya gari, alipowaingiza tu ndani ya hoteli hiyo aliwaeleza kidogo historia ya hoteli, wote wakafurahi kuingia ndani yake, kwani walishasoma sana habari yake kwenye vyombo vya habari.
“This is a dream come true!”(Hii ni ndoto imetimia!) Catarina alijikuta akitamka maneno hayo.
Kila mmoja alipelekwa kwenye chumba chake na Mario Pizaro pamoja na Craig Anderson wakaondoka kwenda kuangalia maandalizi ya shoo ambayo ilitarajiwa kufanyika siku iliyofuata saa moja jioni, wakawaacha wanamitindo wakipumzika vyumbani kwao, muda huo ndio Catarina aliutumia kupiga simu nyumbani akaongea na wazazi wake lakini pia akampata Kevin.
“Paris pakoje?” Kevin aliuliza.
“Pazuri mno, natamani ungekuwa hapa!”
“Ipo siku tutakuwa pamoja.”
“Naisubiri hiyo siku, vipi masomo?”
“Naendelea vizuri sana, nakuomba tu uwe makini maana ulimwengu huo unaoishi una vishawishi vingi, sitaki kukupoteza, nakupenda mno Catarina.”
“Nakupenda pia Kevin.”
“Bado unatunza ile zawadi yangu?”
Catarina hakuweza kulijibu hilo swali, akakata simu na kuanza kulia kwa uchungu, kidonda kilikuwa kimetoneshwa, zawadi ya bikira aliyomuahidi Kevin ilishaondolewa na tajiri Jackson Motown, tena bila ridhaa yake! Hasira ikampanda, akatamani kufanya jinai, lakini akauzuia moyo wake, hakuelewa kabisa ni kitu gani angekifanya ili amfurahie Craig tena.
Simu yake ilipigwa mara kadhaa, ikaonyesha namba ya Kevin lakini hakuthubutu kuipokea maana alielewa swali lingekuwa lilelile, mwisho Kevin aliacha kupiga, Catarina akaendelea kulia kwa uchungu mpaka mlango wake ulipogongwa saa tatu baadaye, akafungua na kukutana na Mario Pizaro.
“Are you okay?”(Uko sawa?)
“I have got some flu!”(Nina mafua!)
“Suddenly?”(Ghafla?) aliuliza kwa mshangao maana wakati anaondoka alimwacha akiwa katika hali ya kawaida.
“I am allergic to some stuff!”(Nina mzio na baadhi ya vitu!)
“Sorry! Will manage tomorrow?”(Pole! Utaweza kesho?)
“I will manage!”(Nitaweza!)
Baada ya hapo walianza kuongea mambo mbalimbali juu ya maisha na kazi ya mitindo, Mario Pizaro akimwambia wazi Catarina kwamba kama angeutumia ipasavyo uzuri wake, hakika maisha yake yangebadilika milele, akidai alikuwa na zawadi ambayo si kila mwanamke duniani alikuwa nayo, yaani uzuri wa asili, si wa kununua dukani.
“What are you doing in Africa?”(Unafanya nini Afrika?)
“Why are you asking?” (Kwa nini unauliza?)
“With that beauty of yours, you are supposed to be living in New York, Paris, Milan or Los Angeles!” (Kwa uzuri wako, unatakiwa kuwa unaishi New York, Paris, Milan au Los Angeles!)
“Sure?” (Kweli?)
“Yeah! Those are the fashion cities in the world!”(Ndiyo! Hiyo ndiyo miji ya mitindo hapa duniani!)
“How can I do that?”(nawezaje kuhama?)
“You want to shift?”(Unataka kuhama?)
“Even now!”(Hata sasa!)
“Leave that in my hands, I will make meet one tycoon who owns the largest modeling agency in North America!”(Niachie hilo mikononi mwangu, nitakukutanisha na tajiri mkubwa anayemiliki kampuni kubwa ya mitindo huko Amerika ya Kaskazini!)
Kauli hiyo ya Mario Pizaro ilimfanya Catarina aliyekuwa amejilaza kitandani anyanyuke na kuanza kushangilia, alichokitaka kilikuwa mbioni kutokea kwa njia rahisi kuliko alivyotarajia! Furaha yake ilikuwa bayana mbele ya Mario Pizaro, alipoketi kitini alimwelezea juu ya mabaya aliyofanyiwa na Craig, kiasi kwamba hakuwa tayari kuendelea kufanya naye kazi.
Wakakubaliana baada ya maonyesho hayo tu angejitoa chini ya utawala wa Craig Anderson na kampuni ya Fonex, mara moja waondoke kwa ndege binafsi ya tajiri aliyeelezwa habari zake kwenda New York, wakiwa ndani ya ndege ambamo pia Mario Pizaro angepanda, wangeongea kila kitu na hata kusaini mkataba wa makubaliano.
“I am so lucky!”(Nina bahati sana!)
“It was pre-planned by God…”(ilipangwa na Mungu kabla…) aliongea Mario Pizaro kwa sauti ya unyenyekevu.
“It seems!”(Inaonekana hivyo!)
“God is so good!”(Mungu ni mwema!)
“Sure! Are you a born again?”(Hakika! Umeokoka?)
“Yeah, I love God!”(Ndiyo, nampenda Mungu!)
Catarina akiwa na furaha siku hiyo alitolewa hotelini pamoja na wenzake kutembezwa Jiji la Paris, machozi yalimtoka alipoyaona mabango yake makubwa yametundikwa karibu kila kona ya jiji hilo, yakiwa na maneno “ La reine de la mode” yaliyomaanisha “Malkia wa Mitindo” ambayo yaliwafanya wenzake wajisikie vibaya kwani ilionekana kama vile wananchi wa Ufaransa walikuwa wameandaliwa kumpokea Catarina peke yake.
“Why are you crying?”(Kwa nini unalia?) Mario Pizaro alimuuliza.
“I didn’t expect!”(Sikutegemea!)
“There is so much more ahead for you to see!”(Yako mambo mengi zaidi mbele yako kuyaona!)
“Thank you Mario!”(Ahsante Mario!)
Craig alikuwepo ndani ya gari lakini hakuongea sana na Catarina, alionekana kuwa karibu zaidi na wanamitindo wengine. Saa tatu za usiku walirejea hotelini na kulala mpaka siku iliyofuata ambayo ilikuwa ni siku ya maandalizi ya mitindo tangu asubuhi mpaka saa kumi na mbili jioni walipoondolewa kupelekwa ukumbini ambako walikuta ukumbi umejaa watu mbalimbali mashuhuri duniani na matajiri wenye ukwasi wa kutosha.
Shoo ilifanyika kwa saa nne ndipo ikamalizika, Catarina ndiye akiwa kivutio kuliko warembo wengine wote kutoka sehemu mbalimbali za dunia, nguo za Mario Pizaro zilipata ushindi mkubwa! Zoezi lilipomalizika na kurejea hotelini, kwa wiki nzima maonyesho yaliendelea mpaka yakafikia tamati, siku hiyo ndiyo Catarina aliwakusanya wenzake wote pamoja na Craig na kuwatangazia kuwa alikuwa anajitoa kwenye kampuni.
“Why?”(Kwa nini?) Craig aliuliza na lilikuwa swali la kila mtu.
“I have decided to try another agency in New York!”(Nimeamua kujaribu kampuni nyingine huko New York!)
Walijaribu kumshawishi abadilishe msimamo lakini haikuwezekana, siku iliyofuata alikuwa ndani ya ndege binafsi aina ya Boeing 737, iliyomilikiwa na tajiri ambaye Catarina alikuwa bado hajamwona wala kutajiwa jina lake, aliwekwa ndani ya chumba maalum ndege ikikata mawingu angani, moyo wake ulikuwa umejawa na furaha kwamba sasa alikuwa amefanikiwa kutimiza ndoto yake, kilichokuwa kikifuata mbele ni kumhamisha Kevin kutoka Tanzania hadi New York ili wafaidi maisha pamoja.
“Get ready, the boss will be in your room in the next five minutes!”(Kaa tayari, bosi atakuwa kwenye chumba chako ndani ya dakika tano zijazo!) Mario Pizaro aliongea akitabasamu.
“I am ready!”(Niko tayari)
“Okay!”(Sawa!) akajibu na kuondoka.
Dakika tano baadaye mlango ukafunguliwa, akaingia mtu akiwa uchi wa mnyama, Catarina alipomwangalia usoni akamtambua, moyo wake ukapiga kwa kasi, jasho jingi likamtoka; ALIKUWA JACKSON MOTOWN!

Je, nini kitaendelea? Fuatilia siku ya Ijumaa katika Gazeti la Championi Ijumaa.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW

INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/

TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari

FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers

YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1

2 Comments
  1. hussein hassani says

    duu mkuki moyoni mwangu

  2. Emmanuel says

    Mbona haiendi kwa series?

Leave A Reply