The House of Favourite Newspapers

Mnyama Amtafuna Lyon Taifa

Picha ya Mtandao

Na WILLBERT MOLANDI| CHAMPIONI IJUMAA| MICHEZO

TIMU ya Simba, jana Alhamisi ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya African Lyon katika mchezo wa Kombe la FA raundi ya sita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar. Katika mchezo huo uliokuwa na ushindani kwa pande zote, ulishuhudiwa Simba wakijipatia bao hilo dakika ya 58 lililofungwa na Mrundi, Laudit Mavugo baada ya shuti lake hafi fu kushindwa kudakwa na kipa wa Lyon, Rostand Youthe raia wa Cameroon.

Katika kipindi cha kwanza dakika ya 18, Simba ilionekana kuhitaji zaidi ushindi kwenye mchezo huo baada ya Juma Liuzio kupiga shuti kali langoni mwa Lyon na kuokolewa na Youthe na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Dakika ya 32, mshambuliaji wa Ibrahim Ajib alikosa bao la wazi baada ya kuwatoka mabeki wa Lyon lakini shuti lake lilipaa. Kipindi cha pili Simba walifanya mabadiliko kwa kuwatoa Juma Liuzio na Said Ndemla ambao nafasi zao zilichukuliwa na Shiza Kichuya na Moham
med Ibrahim ambaye alikosa bao la wazi baada ya kuunganisha mpira krosi kwa kichwa uliopigwa na Besala Bokungu.

Kwa upande wa Lyon walifanya mabadiliko ya kuwatoa  Hamad Manzi na kumuingiza Awadh Juma na Omary Salum nafasi yake ilichukuliwa na Cosmas Lewis. Dakika kumi za mwisho Simba walifanya mashambulizi mengi kupitia kupitia kwa Ajib, Kichuya na Mohammed Ibrahim lakini hata hivyo hayakuweza kuzaa mabao na mpaka  dakika 90 zinamalizika.

Kocha wa Msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja aliwapongeza wachezaji wake kwa ushindi huo kutokana na kufuata maelekezo waliyowapa ambapo amesisitiza ushindi huo kwao ni sehemu ya kulipiza kisasi baada ya kufungwa na timu hiyo katika mchezo wa ligi.

Upande wa Kocha wa Lyon, Charles Otieno alisema anawapongeza wachezaji wake kwa kuonyesha uwezo mkubwa katika mchezo huo licha ya kupoteza kwao bao moja ambalo halikuwa la mipango yoyote zaidi ya kubahatisha.

Katika mchezo huo, kocha wa zamani wa Simba, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ alikuwepo jukwaa kuu ambapo alionekana mwenye furaha muda mwingi huku akicheka pamoja na viongozi wa Simba waliokuwepo katika mchezo huo.

Comments are closed.