The House of Favourite Newspapers

MONDI, TANASHA WAWEKA REKODI MPYA

0

 STAA wa Bongo Fleva kutoka Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB), Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ na mzazi mwenzake, Tanasha Donna, wameandika historia mpya Bongo. Ukisoma maoni ya kolabo ya wimbo wao mpya wa Gere kwenye Mtandao wa YouTube, utaachana na stori za kumshindanisha Diamond au Mondi na akina Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’ na Rajab Abdul ‘Harmonize’.

Rahj Ommy ni shabiki wa Mondi ambaye ameandika chini ya video ya wimbo huo kwenye YouTube; “Diamond Platnumz wewe ni nguli wa muziki Afrika nzima. Ongeza utundu zaidi uizimishe Nigeria nzima. Wote uwazike japo hawakufikii ila wapo wanaokuumiza kichwa kaka Chibu. Wewe ni mwisho mzee. Afrika namba moja.”

REKODI ZA GERE

Ilikuwa Jumatano ya saa 4:00 asubuhi ndipo Wimbo wa Gere ulipopostiwa kwenye Akaunti ya Mondi ya Mtandao wa YouTube. Kabla ya siku hiyo kumalizika (saa 5:59 usiku), wimbo huo uliandika historia ambayo haijawahi kutokea Bongo na Afrika Mashariki kwa ujumla.

MIL 1 KWA SAA 14

Ndani ya saa 14 wimbo huo ulikuwa umesambaa kote kwenye mitandao ya kijamii na kutazamwa mara milioni moja.

Rekodi hiyo ilimfanya Tanasha kujitokeza kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii za Instagram na Twitter na kuwashukuru kwa kuonesha sapoti na upendo mkubwa kila anapoachia kazi mpya;

“Nimeamka, ninajisikia furaha ya ajabu. Mkongwe Swizz Beats (prodyuza) anaburudika na Gere na ninafurahi kusikia nimevunja rekodi kama msanii mwanamke wa kwanza Afrika kufikisha watazamaji milioni moja kwa saa 14 kwenye YouTube. “Mungu ni mwema na kwenu wote mliosapoti hili.”

GERE NAMBA MOJA

Hata kabla ya kufikisha idadi hiyo ya watazamaji, wimbo huo wa Gere ulikuwa umezipangua nyimbo kibao na kushika namba moja (YouTube trending number one) na kung’ang’ania hapo hadi jana wakati gazeti hili linakwenda mitamboni.

Kama ilivyokuwa kwa Tanzania, ndivyo ilivyokuwa kwa Kenya ambapo wimbo huo uliteka hisia za wengi.

SWIZZ BEATS APAGAWA NA GERE

Ukiachilia mbali mashabiki wa Afrika Mashariki, mtayarishaji maarufu wa muziki nchini Marekani, Swizz Beats alimuomba Mondi kumtumia wimbo huo wa Gere.

Beatz ambaye jina lake halisi ni Kasseem Dean, aliandika ujumbe kwenye ukurasa wa Mondi wa Instagram, akimuomba amtumie wimbo huo, jambo ambalo Mondi alikubaliana naye na kumtumia.

Prodyuza huyo ambaye ni mume wa mwanamuziki mkubwa wa Marekani, Alicia Keys ameshawatengenezea nyimbo wanamuziki wakubwa duniani kama, Beyonce katika Wimbo wa Check on It na Ring the Alarm.

Nyimbo nyingine alizozitengeneza ni Jigga My Nigga na Girl’s Best Friend za Jay Z, Ultralight Beam wa Kanye West, Touch It wa Busta Rhymes, Party Up (Up in Here) wa DMX na Gotta Man wa Eve E.

Prodyuza huyo, baada ya Mondi kumtumia aliuposti kwenye ukurasa wake wa Instagram.

SIRI YA MONDI NA SWIZZ BEATS

Kuhusu uwepo wa kolabo ya Mondi na Swizz Beats, mmoja wa mameneja wa Mondi, Babu Tale alitoa siri kwamba kuna mambo makubwa yanaendelea kuiva.

“Mambo mazuri yanakuja, cha muhimu tuendelee kusapoti wasanii wetu na muziki huu ufike mbali zaidi.

“Kukubalika na mtu kama yule (Swizz Beats) kunaonesha kwamba muziki wetu sasa unatoboa Marekani ambako dunia iliamini ndipo kuna muziki mzuri tu na siyo kwingine.

“Alichokifanya Swizz Beats (kuposti Wimbo wa Gere kwenye ukurasa wake wa Instagram) ni kuuonesha ulimwengu kuwa muziki wetu ni mzuri na sasa unakubalika zaidi duniani,” alisema Tale.

ZILIZOPIGWA KIKUMBO

Nyimbo nyingine za Bongo Fleva zilizopigwa kikumbo na Gere kwenye YouTube ni pamoja na Teamo wa Rayvanny na Wanga wa Lava Lava na Meja Kunta.

REKODI YA RAYVANNY

Septemba mwaka jana, Rayvanny ambaye naye ni memba wa Wasafi aliweka rekodi kwenye tasnia ya muziki barani Afrika baada ya kuachia Wimbo wa Pepeta alioshirikiana na staa wa filamu wa Bollywood nchini India, Nora Fatehi ambao ulipata watazamaji milioni moja ndani ya saa sita. Sasa Gere umeweka rekodi mpya Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.

 

 STORI: PAUL SIFAEL, RISASI

Leave A Reply