The House of Favourite Newspapers

Yanga Yashtukia Mchezo Mchafu, Yabadili Mbinu

0

ZILE sare tatu mfululizo walizozipata Yanga katika mechi zilizopita za Ligi Kuu Bara, zimewakera mashabiki, viongozi na hata wachezaji wa timu hiyo ambao wamesema kuna mchezo mchafu wanafanyiwa, hivyo wameupatia dawa na kubadili mbinu juu kwa juu.

 

Yanga katika mechi tatu iliambulia pointi tatu, ilitoka sare ya 1-1 na Mbeya City kwenye Uwanja wa Taifa, Dar, kisha suluhu dhidi ya Prisons uwanjani hapo na kumaliza kwa sare ya 1-1 dhidi ya Polisi Tanzania kwenye Uwanja wa Ushirika, Kilimanjaro.

 

Luc Eymael ambaye ni kocha mkuu wa timu hiyo, ameweka wazi kwamba hafurahishwi na aina ya matokeo ambayo wanayapata, lakini wapinzani wao wanawafanyia mchezo mchafu kwa kujiangusha sana uwanjani na kulinda zaidi goli lao.

 

“Kama ukiangalia kwenye mechi zetu tumekuwa tukifanya vizuri kuliko wapinzani wetu. Tunacheza kwa kiwango cha hali ya juu kuliko wao.

“Mara nyingi wao wanakaa nyuma tu na wanapopata bao huwa wanajiangusha muda mwingi, hii haipo sawa, kiukweli tunastahili kupata mabao ya mapema ili tusiwape muda wa kufanya mambo hayo,” alimaliza Mbelgiji huyo.

 

Wakati kocha huyo akisema hivyo, mastaa kadhaa wa timu hiyo nao wakatoa ya moyoni wakati leo wakitarajiwa kucheza dhidi ya Coastal Union katika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

 

Kiungo Balama Mapinduzi, alisema: “Matokeo tuliyopata hivi karibuni siyo mazuri kwa upande wetu, hivyo tutafanya kila liwezekanalo kuhakikisha tunashinda dhidi ya Coastal Union.”

Kauli ya Mapinduzi iliungwa mkono na beki Ally Mtoni ‘Sonso’ aliyesema: “Mashabiki wetu wanataka kuona timu ikipata ushindi na si kingine kwa sasa, hivyo ni jukumu letu kupigana kuhakikisha tunapata ushindi dhidi ya Coastal Union.”

 

Msumari wa mwisho uligongelewa na Haruna Niyonzima aliyesema: “Mechi zote tunajiandaa vizuri lakini Mungu anapanga yake, bado tuko pamoja tutaendelea kufanya kile tunachokiweza kuisaidia timu katika mechi zijazo.”

STORI: SAID ALLY NA MARCO MZUMBE

Leave A Reply