The House of Favourite Newspapers

Morrison Apewa Miaka Miwili, Yanga Watoa Tamko

0

MORRISON is red! Ndiyo kauli iliyoteka mitandao ya kijamii na vijiwe vyote vya soka jana mchana ikiwa ni muda mchache baada ya Simba kumtambulisha kiungo mshambuliaji raia wa Ghana, Bernard Morrison kuwa mchezaji wao.

 

Simba chini ya mwekezaji wake, Mohammed Dewji ‘Mo’, hivi karibuni ilitangaza kufanya usajili wa kishindo kuelekea msimu ujao na kutamba ina uwezo wa kumchukua mchezaji yeyote kutoka sehemu yoyote.

 

Morrison ambaye alijiunga na Yanga Januari, mwaka huu ikiwa ni katika kipindi cha usajili wa dirisha dogo, alikuwa gumzo baada ya kuonesha uwezo wa hali ya juu wa kuuchezea mpira.

Kitu kikubwa kilichompa umaarufu zaidi ni kitendo cha kutembea juu ya mpira, kisha kuja kuwatungua Simba katika mechi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Machi 8, mwaka huu jijini Dar ambapo Yanga ilishinda 1-0.

 

Kwa siku za karibuni, wakati Yanga ikifanya usajili wake kwa fujo, Simba walikaa kimya, kisha jana wakaibuka na kusema: “Leo ni 8/8, saa 8:00 mchana tuna jambo letu. Tulieni msitufokeeeeeee.

 

”APEWA MIAKA MIWILI

Wakati Morrison akitambulishwa jana mchana, Simba wamesema wamempa mkataba wa miaka miwili kuitumikia timu hiyo ambayo msimu huu imebeba makombe yote. Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la Azam Sports, huku msimu ujao ikiwa na nafasi ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

DAU LAKE KUFURU

Katika mkataba wake huo wa miaka miwili, Simba imetoa shilingi milioni 230 za usajili ikiwa ni dau la kufuru na kumfunika kiungo Mzambia, Clatous Chama ambaye wakati anatua hapo, inaelezwa dau lake halikuzidi Sh milioni 100.

 

YANGA WAPATWA KIGUGUMIZI

 

Baada ya Morrison kutambulishwa na Simba, huku Yanga wakiwa na kauli yao kwamba bado ni mchezaji wao hadi Julai 2022, Spoti Xtra liliwatafuta viongozi wa Yanga kuzungumzia usajili huo wa Morrison kwenda Simba. Mkurugenzi wa Uwekezaji wa Kampuni ya GSM inayoidhamini Yanga, Injinia Hersi Said, alipotafutwa, alisema: “Sitaki mnilishe maneno, mtafuteni katibu atawapa majibu.”

 

Alipotafutwa Kaimu Katibu wa Yanga, wakili Simon Patrick, alikuwa akikata simu.Ikumbukwe kuwa, kwa muda mrefu, kumekuwa na mvutano wa Morrison na Yanga juu ya mkataba wake, Morrison alikuwa anasema mkataba wake umemalizika Julai 14, mwaka huu, huku Yanga wakisema ni mali yao hadi Julai 14, 2022 kwa sababu baada ya mkataba wake wa miezi sita kumalizika, aliongeza mwingine wa miaka miwili.

 

Sakata hilo liliripotiwa hadi Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na wote kuitwa kujieleza, kisha ikaelezwa kwamba Yanga waliupeleka mkataba wake mpya hadi Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kuonesha kwamba ni mchezaji wao.

 

Pia katika majina ya wachezaji ilioachana nao, jina la Morrison limebaki kati ya wale ambao msimu ujao wataichezea Yanga.

 

Spoti Xtra lilikuwa la kwanza kuandika ishu ya Morrison kumalizana kabisa na Simba ikiwa ni baada ya kujiridhisha kwa kila kitu ikiwemo kuhamishwa nyumba, kununuliwa vifaa vya mazoezi na kigogo mmoja wa Simba.

 

Katika gazeti lililotoka Julai 16, 2020, lilikuwa na kichwa cha habari kilichosomeka hivi: “Morrison, Simba mchezo umeisha.”

 

TAMKO LATOKA

Baada ya viongozi kuwa na kigugumizi, jana jioni kupitia mitandao yao ya kijamii, Yanga waliposti taarifa iliyosema:

“Uongozi wa Klabu ya Yanga, umeona kinachoendelea kwenye mitandao ya kijamii na kuibua taharuki kwa mashabiki wa soka hapa nchini.

 

“Uongozi unafuatilia kwa ukaribu na umakini mkubwa suala hilo na ikithibitika hatua na za mfano zitachukuliwa kwa pande zote zinazohusika.

 

“Aidha uongozi unawataka wanachama na wapenzi wa Yanga kuwa watulivu kwani mchezaji Bernard Morrison ana mkataba na klabu yetu hadi 2022 na shauri baina yake na klabu bado liko mikononi mwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Jumatatu linaendelea kusikilizwa.”

 

MWENYEWE AFUNGUKAMorrison jana muda mchache kabla ya kucheza mechi ya hisani kati ya Team Kiba na Team Samatta, alizungumzia ishu yake ya kutambulishwa kuwa mchezaji wa Simba ambapo alisema: “Ndiyo mpira ulivyo, mimi kujiunga na Klabu ya Simba ni sehemu ya soka, najua mashabiki wa Yanga watakuwa wamejisikia vibaya sana kwa sababu walikuwa wananipenda.

 

“Nakwenda kufaya kazi sehemu nyingine sasa, nitakwenda kucheza kwa nguvu zangu zote ili mashabiki wa Simba na wanachama wapende kile nitakachofanya uwanjani na kunipenda mimi.“Naomba mashabiki wa Simba wanipokee kwa sababu nimeshakuwa mwanafamilia wao, nipo nyumbani sasa.

Leave A Reply