The House of Favourite Newspapers

MR. EBBO AFURAHIA MO KUPATIKANA, AHIMIZA UZALENDO

NIPO ndotoni, nasikia DJ akichanganya nyimbo mbalimbali za Bongo Fleva huku wasanii sauti nyingine zikisikika kufuatisha mashairi hayo. Kuna wakati nilisikia wimbo wa Mikasi wa Mangwair, ghafla nikasikia Matawi ya Juu wa Langa.

 

Kabla sijakaa sawa nikasikia Hata Kwetu Wapo wa Sam wa Ukweli, baadaye nikasikia Sina Makosa wa Mtoto wa Dandu. Wakati nikiendelea kusikiliza muingiliano huo wa nyimbo, muziki ukazima ghafla na ndani ya sekunde kadhaa, nikasikia wimbo wa Mr. Ebbo (Abel Loshilaa Motika) uitwao Mi Mmasai.

 

Sijakaa sawa muziki ukazima ghafla, nikaguswa begani na mtu aliyekuwa nyuma yangu. Nilipogeuka nikamuona Mr. Ebbo mwenyewe, akaanza kunisemesha.

Mr. Ebbo: Kijana vipi tena mbona hapa? Nakumbuka nilikuacha mwaka 2011 nilipoondoka duniani.

Mimi: Ni kweli kabisa, hujakosea wakati huo nilikuwa ndio kwanza nimeanzaanza kazi ya uandishi wa habari. Wewe ukaondoka duniani.

 

Mr. Ebbo: Vipi lakini huko duniani, mambo yanakwendaje?

Mimi: Mambo yanakwenda vizuri kama ulivyoyaacha. Kikubwa ni kwamba watu wamezidi kupiga hatua.

Mr. Ebbo: Muziki wa Bongo Fleva vipi unakua au bado wahindi wanaendelea kutunyanyasa?

Mimi: Soko la albamu tulishalisahau, siku hizi wasanii wanatoa singo tu na kuishia kufanya matamasha.

Mr. Ebbo: Mwendo huo si mbaya lakini wanapaswa pia kutoa albamu. Jamaa zangu Wagosi wa Kaya tuliokuwa nao kule Tanga vipi wapo? Bado wanafanya muziki?

Mimi: Kwa kweli lile kundi sijalisikia muda kidogo nadhani kila mtu anafanya yake.

Mr. Ebbo: Enhe halafu nimekumbuka, juzikati alipokuja Pancho alituambia kuhusu ishu ya mfanyabiashara Mo kutekwa, vipi amepatikana?

 

Mimi: Eee amepatikana bwana baada ya kutekwa kwa takriban siku 9!

Mr. Ebbo: Wee, unasema kweli? Acha masihala bwana.

Mimi: Masihala gani, huo ndio ukweli kaka!

Mr. Ebbo: Amepatikanaje? Waliomteka walikuwa na lengo gani sasa? Walimtesa?

 

Mimi: Amepatikana kwenye viwanja vya Gymkhana Posta jijini Dar. Waliomteka hadi sasa hatujajua walikuwa na lengo gani maana hawakutaka pesa wala nini. Kuhusu kumtesa pia inasemekana hawajamtesa.

Mr. Ebbo: Daah! Kwa kweli kama amepatikana ni jambo la kumshukuru Mungu na ni vizuri Watanzania wakadumisha umoja, wakawa wazalendo, wakashikana pamoja ili vikundi hivi vya utekaji vishindwe kuendelea kufanya mambo hayo. Si nilisikia mbali na Mo hata Roma naye walimteka.

 

Mimi: Yeah, naye ilikuwa hivyo hivyo na bahati mbaya sana watekaji nao hatukujua walimteka kwa sababu gani. Hawakumtaka atoe hela wala nini.

Mr. Ebbo: Polisi wanasemaje kuhusu tukio la Mo?

Mimi: Uchunguzi unaendelea, wameapa kula sahani moja hadi wawapate hao watekaji.

Mr. Ebbo: Hayo matukio hayaleti picha nzuri, ni vyema jeshi la polisi likajipanga vilivyo kuyatokomeza.

 

Mr. Ebbo: Vipi kwenye upande wa michezo, vilabu vyetu Simba na Yanga vinaendelea kushika hatamu?

Mimi: Ligi bado mbichi ingawa dalili zinaonesha, Simba na Yanga wataendelea kushika hatamu maana wanasajili vizuri, wana uwezo kifedha. Ila Azam nayo si ya kubeza, ndiyo inayoongoza ligi kwa sasa.

Mr. Ebbo: Matukio gani mengine yanatikisa nchi kwa sasa?

Mimi: Ni mengi lakini ya wanandoa kuuana na watoto kuibiwa ndiyo yanaonekana kushamiri.

 

Mr. Ebbo: Wanauana kwa nini? Hao watoto nao wanawaiba wa nini? Watanzania wanaelekea wapi?

Mimi: Kwa kweli sababu zao hazieleweki ila mimi naona watu kukosa utu na ubinadamu ndio kumechangia haya yote yatokee.

Mr. Ebbo: Waambie Mungu yupo, anawaona wanayoyafanya, anajua watakayoyafanya hivyo ni vyema wakamrudia yeye, wakaacha kufanya matukio ya aina hiyo.

Mimi: Sijui kama wataelewa maana hata kabla hujanituma niwaambie, Wachungaji, mashehe kila siku wanawahubiria lakini bwana…

 

Mr. Ebbo: Hao dawa yao naijua, njoo nikuoneshe (akanivuta kwenye sehemu yenye moto mkalii)

Wakati anazidi kunielekeza kwenye hilo tanuru la moto, nilishindwa kuendelea mbele, nikawa natamani kumwambia anirudishe lakini nashindwa.

Ghafla nikashtuka na kugundua kumbe mazungumzo yangu na Mr. Ebbo yalikuwa ni ndoto na si uhalisia. Ndoto hizi bwana!

NA ERICK EVARIST :  SAA 9 USIKU KITANDANI MWANGU!

Comments are closed.