The House of Favourite Newspapers

Mrembo Oman atajwa kumng’oa tanasha kwa Mondi

0

MREMBO kutoka Uarabuni nchini Oman, anatajwa kumng’oa mzazi mwenza wa staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Tanasha Donna, Risasi limetonywa.

KILICHOJIRI KABLA YA KUIBUKA MAPYA

Mwishoni mwa wiki iliyopita, gazeti hili lilipokea ubuyu wa kila aina kutoka kwa vyanzo vyake vingi kuwa; “Tanasha amefungasha virago kwa Diamond na amerudi kwao nchini Kenya.”

Katika kufuatilia kwa ukaribu, gazeti hili lilinusa asilimia zaidi ya sabini na tano kuwa, kuna msukosuko kwenye kasri la Diamond au Mondi na Tanasha lililopo Mbezi-Beach jijini Dar. Wakati watu wakitafakari hili na lile, Tanasha akafuta picha zote za Mondi kwenye ukurasa wake wa Instagram na kushusha waraka mzito kuhusu watu ambao hujipenda kwa kiwango cha kuvuka mipaka.

Kwenye waraka wake huo, Tanasha aliwataka mabinti kujiepusha na watu wenye hulka za aina hiyo akiwataja kama watu hatari. Tanasha alisema, wafungue macho na kujua kuwa hilo si penzi, bali ni mtu kumtumia mwingine. Alisema kuwa, kwa sasa anajisikia huru kwani baadhi ya watu wametolewa kwenye maisha yake.

Aidha, Tanasha aliongeza kuwa, amepata funzo, lakini ameyaweza yote kupitia kwa maombi. Waraka huo wa Tanasha ulionekana kumlenga mtu aliye karibu naye ambaye anatajwa kuwa ni Mondi. “Ni kama kucheza na ibilisi. Wasamehe, jiondoe kwa maisha yao na acha Mungu akabiliane na wao,” ilisomeka sehemu ya waraka huo.

MAPYA YAIBUKA

Baada ya habari hizo kushika kasi kama moto wa kifuu kwenye mitandao ya kijamii, gazeti hili lilizama chimbo na kuibuka na mapya. Chanzo ndani ya familia ya Mondi kilidai kuwa, chanzo cha yote ni mrembo kutoka familia ya kitajiri na ya kifalme nchini Oman.

Ilidaiwa kuwa, kwa muda mrefu sasa, mama mzazi wa Mondi, Sanura Kassim ‘Mama D’ amekuwa akimpiga vita Tanasha kwa kuwa ana lake moyoni. Ilisemekana kwamba, mwaka jana, Mondi alipata ziara ya kikazi (shoo) nchini Oman ambapo aliambatana na timu kubwa ya lebo yake wa Wasafi Classic Baby (WCB) pamoja na familia yake.

Kwenye msafara huo, ukiacha madansa, wasanii wenzake na mama yake, pia aliambatana na dada yake, Esma Khan na rafiki wa familia hiyo, Juma Lokole. Wakiwa nchini humo, ilidaiwa kwamba, Mondi alipata mwaliko kwenye familia moja ya kitajiri na kifalme.

BINTI WA MFALME AMZIMIA MONDI

Ilidaiwa kuwa, kwenye mwaliko huo, ndipo lilipoibuka suala la binti wa familia hiyo kumzimia Mondi na ‘kumpa kichaa’ Mama D ambaye alianza harakati za kuhakikisha binti huyo ndiye anakuwa mkwe wake. “Kuanzia hapo, yule mama (Mama D) hakutaka tena kusikia habari za Tanasha, kwa hiyo hatushangai kuona haya yanayotokea,” kilidai chanzo hicho kwa sharti la kutotajwa gazetini.

SHEREHE KWA MAMA MONDI

Wakati hayo yakiendelea, usiku wa kuamkia juzi Jumatatu, nyumbani kwa Mama D, Madale-Tegeta jijini Dar, kulishuhudiwa bonge la pati iliyosemekana ni ya kusherehekea kusepa kwa Tanasha. Katika pati hiyo, watu walikula, kunywa na kucheza Kibao-Kata hadi majogoo.

MAMA D SASA

Kuhusu mambo hayo yote ya kuondoka kwa Tanasha na kuangusha pati, mapema Jumatatu, gazeti hili lilimtafuta Mama D au Mama Dangote ambapo baada ya kupokea simu, alisikiliza kila kitu kisha akakata simu.

ANKO SHAMTE: NI PATI YA SINGO

Alipotafutwa mume wa Mama D, Maisara Shamte ‘Anko’ na kuulizwa juu ya kuangusha pati baada ya Tanasha kusepa, alisema pati hiyo ilikuwa ni kwa ajili ya singo. “Hiyo pati ilikuwa ni kwa ajili ya singo,” alisema Anko Shamte.

SINGO NI NINI?

Kwa mujibu wa watoto wa mjini, single (singo) ni sherehe ya kumuaga mwanaume ambaye yupo mbioni kuoa ambayo ni kama send-off kwa mwanamke. Hata hivyo, Anko Shamte alipobanwa hiyo singo ni ya nani, hakuwa tayari kutoa ufafanuzi.

BABA D: HAYA MAMBO NI MAZITO

Pia gazeti hili lilizungumza na baba mzazi wa Mondi, Abdul Juma ‘Baba D’ kuhusiana na mwanaye huyo kuachana na Tanasha kisha kuwepo kwa tetesi kuwa ana ‘kifaa’ kingine kutoka nchini Oman ambapo alikiri kusikia mambo hayo mazito na kuomba apewe muda afuatilie zaidi.

“Hayo mambo mazito, nimesikiasikia kuhusu huyo binti wa Oman, lakini ili kupata ishu zaidi ngoja nifuatilie, maana sasa hivi nipo bize kidogo,” alisema Baba D.

DALILI ZILIONEKANA MAPEMA

Dalili za Tanasha kuachana na Mondi zilianza kuonekana mara tu baada ya kumaliza sherehe ya 40 ya kumtoa mtoto wao Naseeb JR iliyofanyika nyumbani kwa Mama D, Desemba, mwaka jana, ndipo mwanamama huyo akafungasha kila kilicho chake na kurejea kwao, Mombasa nchini Kenya.

Kuondoka kwa Tanasha kulielezwa kuwa hakukuwa kwa uzuri, bali kuna sababu kubwa ambayo ni kutofautiana na mama mkwe wake.

Katika ishu hiyo, ilidaiwa kuwa, chanzo cha kutofautiana kwao ni baada ya Mama D kuwapeleka wageni wake nyumbani kwa Tanasha, lakini badala ya kuwapokea, akaenda kujifungia chumbani kwake na kulala.

Baadhi ya wachambuzi wa habari za burudani walilieleza gazeti hili kwamba, kwa Mama D haishindikani kukorofishana na Tanasha kwani ilishatokea hivyo wakati Mondi akiwa na Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’, Hamisa Mobeto na hata Wema Isaac Sepetu.

 

STORI :Memorise Richard, Risasi

Leave A Reply