The House of Favourite Newspapers

Msanii Bongo Movie Azua Simanzi

0

HAYA ni zaidi ya mateso! Ukisema wewe unaumwa, lakini unapata usingizi, kumbe hujawaona wagonjwa wenyewe! Hawa Ibrahim almaarufu Carina kwa jina la uigizaji kwenye tasnia ya Bongo Muvi na video vixen (muuza sura) wa nyimbo za wanamuziki wa Bongo Fleva, mkazi wa jijini Mwanza, anapita kwenye bonde la mauti kiasi cha kuzua simanzi nzito kwa mastaa wenzake. Hawa au Carina, yupo kwenye hali hiyo kwa miezi kadhaa baada ya tumbo lake kutoa usaa kila wakati.

OPERESHENI TANO

Carina yule tuliyezoea kumuona kwenye fi lamu za Kibongo, sasa hawezi kutembea wala kuongea vizuri baada ya kufanyiwa operesheni zipatazo tano. Alianza kwa operesheni ya kwanza ya uvimbe kwenye kizazi, yapata miezi mitatu iliyopita, lakini hadi leo hajaamka kitandani.

 

SIMULIZI YA MATESO

Akilisimulia Gazeti la IJUMAA WIKIENDA juu ya mateso aliyopitia Carina, mama mdogo wa mwigizaji huyo, Amina Seif, huku akilia kwa uchungu, anaanza kwa kusema; “Kiukweli mwanangu anateseka mno, ukisikia mtoto anakuambia anaumia, kweli ujue anaumia na mimi kama mzazi ninaumia mno.”

MAUMIVU YA TUMBO

Amina anasema kuwa, mpaka sasa hawajui ni nini kimemkumba mtoto wao kwa sababu alikuwa mzima wa afya, lakini alianza kusumbuliwa tu na tumbo kama utani. Anasema kuwa, baada ya kuona hali hiyo, walikwenda Hospitali ya Kamanga (Mwanza) na kugundulika ana uvimbe, ndipo alipofanyiwa upasuaji ili kuuondoa uvimbe huo.

 

“Hawa au Carina kama mnavyomjua, hakuwa na tatizo kabisa, zaidi ya uvimbe ambao walimfanyia upasuaji kama wanavyofanyiwa upasuaji wengine na kukawa na matumaini makubwa ya kuwa sawa kama alivyokuwa zamani.

 

“Hata hivyo, hali haikuwa kama tulivyotegemea, kwani hali ilizidi kuwa mbaya hata kuliko mwanzo,” anasema Amina. Anaendelea kusema kwamba, baada ya kumalizika kwa upasuaji, akiwa hospitalini, Carina alianza kuhisi kama kitu chenye ncha kali kikipita kwenye mshono, akaomba msaada wa madaktari kumuangalia, lakini cha ajabu ni kwamba, walivyoziangalia nyuzi walizoshona, walipigwa na butwaa kwani zilikuwa kama mtu amezikata na kiwembe.

 

“Sijui nisemeje, lakini kama ungeziona zile nyuzi zilivyojicharanga, ni kama mtu amechukua kiwembe au kitu chenye ncha kali na kuzikata, jambo ambalo hata madaktari walishangaa. “Baada ya kuona hivyo, ilibidi madaktari wamrudishe tena chumba cha upasuaji na kumshona, kisha walituambia turudi naye nyumbani,” anasema mama huyo.

 

ATOA HARUFU KALI

Amina anasema kuwa, walipomrudisha nyumbani, alikaa kwa muda wa siku tatu, akaanza kuhisi kama anatoa harufu kali ambapo aliomba msaada wa watu anaoishi nao kama wanasikia harufu anayoyasikia ndipo wakamjibu wanasikia harufu.

 

“Alianza kusema kuwa, anasikia harufu kutoka kwenye mwili wake na kweli tulipochunguza, tukagundua kuwa kwenye kitovu kunatoka usaa na vitu vyeusi. Hapo ndipo tulipokimbilia tena hospitalini, tukaonana na daktari ambapo ilibidi awashirikishe madaktari wengine na wakaamua afanyiwe tena upasuaji na hiyo ni ikawa ni upasuaji wa mara ya tatu.

 

“Baada ya upasuaji, ndipo wakakuta ile sehemu ya kitovu imeanza kuoza kwa ndani ambapo waliitoa yote na kutafuta nyama nyekundu na kuweka pale,” anasema mama mdogo wa Carina.

CHANGAMOTO KUBWA

Mama huyo anasema kwa uchungu kuwa, baada ya operesheni hiyo, ndipo kukaibuka changamoto kubwa kwenye kupata haja kubwa ambapo sasa tumbo lilianza kuvimba sana. “Ilibidi apigwe bomba, lakini shida ikawa pembeni kulikuwa na uvimbe mkubwa.

 

“Huwezi kuamini kabisa, pembeni ya tumbo kukavimba kama jipu ambalo lilikuwa likimsumbua sana na kuamua tena kumfanyia upasuaji mwingine wa nne.

“Katika upasuaji huo, safari hii hata nyuzi walizomshonea zilikuwa nene sana kwa sababu tumbo lake lilitanuka sana kwa ajili ya kupasuliwa kila mara na hata alivyofanyiwa alionekana kuleta matumaini japokuwa alikuwa na maumivu makali sana,” anasema Amina.

 

HOFU YAIBUKA

Mama huyo anaendelea kusema kuwa, Carina alipofanyiwa upasuaji huo, alionekana kuwa na matumaini lakini cha kushangaza baada ya siku kama mbili, alianza kutetemeka na kuanza kuongea kama mtoto na mikono kujikunja na kushindwa kufanya chochote kile. Anasema kuwa, hali hiyo ilizua hofu kubwa hadi kwa madaktari kwa sababu mwisho wa siku hawakuona ugonjwa wowote tena.

 

RUFAA YA MUHIMBIILI

“Sijui nisemeje kwa sababu Carina alibadilika ghafla, akaanza kuongea kama mtoto, mikono inatetemeka wakati wote, hivyo madaktari hawakuwa na jinsi yoyote kwa sababu walishajaribu kila wawezalo, hivyo tukaomba rufaa ya kuja Muhimbili (Dar),” anasema mama huyo ambapo juzi jioni, Carina alitarajiwa kufi kishwa Muhimbili kwa vipimo na matibabu ya kuokoa uhai wake.

 

MASTAA WAMLILIA

Baadhi ya mastaa waliofanya kazi na Carina wakiwemo Shamsa Ford, Johari, JB, Steve Nyerere, Hemedy na wengine wengi, walijikuta wakimlilia huku wakijitolea kumsadia ili aweze kupata matibabu.

 

HUJAFA HUJAUMBIKA

Hujafa hujaumbika! Ndivyo maisha yalivyo, leo kwako, kesho kwa mwingine hivyo hata wewe mpenzi msomaji unaweza kumsaidia Carina kupitia namba yake ya mkononi 0712 595 858 ili aweze kupata matibabu.

 

CARINA AMETAMBA…

Carina ametamba kwenye Filamu za Hukumu ya Ndoa, Kiu ya Kisasi, Usia wa Binamu na nyinginezo.

STORI: IMELDA MTEMA, DAR

Leave A Reply