The House of Favourite Newspapers

Msanii Bongo Muvi Akatwa Mguu

0

USIOMBE yakukute, ndivyo unavyoweza kutafsiri mapito ya msanii wa Bongo Muvi, Martin Deus ‘Chiba Kismati’ (32), baada ya kukatwa mguu kutokana na kuathiriwa na ugonjwa wa sikoseli.

Msanii huyo ambaye ni mkazi wa Kigogo-Luhanga jijini Dar, anasumbuliwa na sikoseli tangu alipozaliwa.

 

Akilisimulia Gazeti IJUMAA WIKIENDA mkasa wa maisha yake hivi karibuni, Martin alisema, ugonjwa huo huwa unamsumbua mara kwa mara, jambo linalosababisha kushindwa kumudu gharama za matibabu.

 

Alisema, amekuwa akitumia dawa kwa kipindi chote cha maisha yake tangu alipozaliwa kutokana na ugonjwa huo wa sikoseli.

“Mama yangu yupo Mpanda (Katavi), naye ni mgonjwa, lakini baba yangu ni marehemu… kwa hiyo katika familia sina ninayemtegemea ili aweze kunisaidia katika hali hii,” alisema.

 

Alisema licha ya kuzaliwa na miguu yote isiyo na mushkeli wowote, chanzo cha mguu wake kukatwa ni kidonda kilichotokea mgunii wakati akiwa anasoma elimu ya sekondari.

“Sikumbuki nilikuwa kidato cha ngapi, lakini kidonda kile kilisababisha mguu wangu kuoza ndipo madaktari waliponipa rufaa kutoka Mpanda kwenda Muhimbili (Dar).

 

“Nilipofika Muhimbili, nililazwa, nikafanyiwa vipimo vilivyoonesha kidonda kimeoza kiasi kwamba walishindwa njia ya kufanya, ikabidi wanikate mguu. Iliniuma sana kupoteza mguu na maumivu yake usiombe.

“Daktari aliniambia hatua hizo ni kutokana na ugonjwa nilionao,” alisema.

Alisema ilibidi aanze maisha mapya ambayo hakutegemea kama ingelikuwa hivyo.

 

“Baada ya kupona, nikawa naenda kwenye Chama cha Waigizaji Wilaya ya Kinondoni ambapo kulikuwa na kikundi cha waigizaji ndipo nilipokutana na Dokta Almasi, akanisaidia kisha Tino (mwigizaji Hisani Muya), akanichukua, nikawa ninafanya naye kazi kama ndugu yangu.

 

“Tino alinipangishia chumba na kuninunulia vitu kama vile kitanda, godoro na vingine. “Kwa hapa Dar sina ndugu zaidi ya waigizaji wenzangu na chama chao ndicho ambacho kilikuwa kikinilipia kodi baada ya ile aliyonilipia Tino kuisha,” alisema.

 

Aliendelea kufafanua kuwa, kwa muda wa mwezi huu pekee ameshalazwa mara mbili kutokana na ugonjwa huo unaomsumbua.

“Ingawa wasanii wenzangu wananisaidia kidogo, lakini nao hawawezi kutosheleza mahitaji yangu ndiyo maana ninamuomba Rais Dk John Magufuli atupatie msamaha wa huduma za afya kwa sisi tulio na magonjwa sugu ili kupunguza gharama za matibabu.

 

“Kwa sababu ya kuomba mara kwa mara, hasa ukizingatia hali ya maisha ni ngumu, naamini kama nikipata huduma za ugonjwa huu bure nitashukuru sana,” alisema.

Jamaa huyo aliomba Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo kuingilia kati malipo ya muvi yake aliyocheza inayoitwa Maamuzi ya Mwisho kwa kuwa alitapeliwa na wasambazaji kwani hadi sasa hajalipwa chochote.

 

Alitaja baadhi ya filamu nyingine alizocheza kuwa ni Black Agle akiwa na Mussa Banzi, Queen Elizabeth; Shetani wa Mguu Mmoja na Mapenzi Kizungumkuti.

Kwa yeyote anayeguswa na mkasa wa msanii huyu anaweza kuwasiliana naye kwa namba; 0714 272 026 na 0757 319 302 ambazo zimesajiliwa kwa jina la Martin Deus.

Stori: Neema Adrian, Dar

Leave A Reply