The House of Favourite Newspapers

Mserbia Amuongezea Mabao Sarpong

0

KOCHA Mkuu wa Yanga Mserbia, Zlatko Krmpotic amekiangalia kikosi chake kwa dakika 90 na kugundua upungufu kwenye safu yake ya ushambuliaji na kutamka kuwa inahitaji maboresho makubwa kuhakikisha inapata matokeo mazuri kwenye michezo ijayo.

 

Mserbia huyo alikisimamia kikosi hicho kwenye mchezo uliopita wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Prisons uliomalizika kwa sare ya bao 1-1 akiwa amekaa kwa mara ya kwanza kwenye benchi kuifundisha timu hiyo, tangu akabidhiwe majukumu hayo akimrithi Mbelgiji, Luc Eymael.

Safu ya ushambuliaji ya Yanga hivi sasa inaundwa na Michael Sarpong, Yacouba Songne, Carlos Fernandez ‘Carlinohs’, Tuisila Kisinda na Ditram Nchimbi.

 

Akizungumza na Championi Ijumaa, Krmpotic alisema kuwa ameamua kufanya hivyo kutokana na kuona kwamba eneo hilo linatengeneza nafasi za kufunga lakini wanashindwa kuzifanyia kazi kama ilivyokuwa kwenye mechi yao na Tanzania Prisons.

 

“Tunahitaji kufanya marekebisho katika eneo letu la ushambuliaji kwani nimeona kuna upungufu. Tunatengeneza nafasi lakini bado tunashindwa kuzifanya kuwa mabao.

“Hivyo nimeona tulifanyie kazi eneo hilo kwa kuhakikisha kwamba linazalisha mabao mengi tofauti na ilivyokuwa katika mechi yetu ile ya kwanza na naamini tutafanikiwa,” alisema Krmpotic.

 

Kwa upande wake Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli alikazia kuwa kwa wiki hii kocha huyo alikuwa analifanyia kazi eneo hilo kwenye mazoezi yao kabla ya kuwavaa Mbeya City.

WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam

Leave A Reply