The House of Favourite Newspapers

MSHINDI SHINDA NYUMBA… DAR SIPAWEZI, NITABAKI DOM

0
George Majaba na familia yake.

MSHINDI wa Bahati Nasibu ya Shinda Nyumba Awamu ya Pili, George Majaba ambaye ni mkazi wa Makole Dodoma, wakati wowote kuanzia sasa atakabidhiwa nyumba yake aliyojishindia Septemba 27, mwaka huu.

Ni mjengo wa kisasa, wenye vyumba vitatu ikiwemo Master Bed Room, lakini pia ikiwa na vyumba vingine kwa ajili ya chakula, kusomea, jiko, sebule, choo na bafu, pia ikiwa tayari imeshaingizwa umeme ndani yake, ambayo imejengwa Bunju B nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Majaba ambaye ni kondakta wa mabasi ya abiria yanayofanya safari zake kati ya Dodoma na vijiji vya mkoa huo, alizungumza na gazeti hili juu ya ushindi wake huo, akizungumzia mambo mbalimbali yanayohusu shindano hilo na maisha kwa jumla.

“Nimefarijika sana kwa ushindi huu na kwa kweli sina cha kufanya zaidi ya kumshukuru Mwenyezi Mungu na kuitakia maisha marefu kampuni ya Global Publishers, ambayo imefanya jambo zuri na la kuigwa.

George Majaba na familia yake.

“Pamoja na kushinda, lakini sidhani kama nitaweza kuishi Dar es Salaam kwa sababu mimi maisha yangu nipo Dodoma, hapa ndipo ninapopata riziki yangu, nikisema niondoke nikaishi Dar, kila kitu kitakuwa kigeni kwangu, kwa hiyo nadhani kwa sasa nitaendelea kubaki hapa.

“Ila nadhani nyumba hiyo inaweza kusaidia sana maisha yangu kwa sababu kuwa na nyumba Dar es Salaam siyo jambo dogo, mimi nitaendelea kubangaiza maisha yangu hapahapa Dodoma, nitajadiliana na familia yangu kuona tunafanyaje na hiyo nyumba, lakini yote hayo ni hadi pale nitakapokabidhiwa,” alisema mshindi huyo mwenye umri wa miaka 42.

Nyumba aliyoshinda.

Shinda Nyumba Awamu ya Pili ilifanyika Septemba 27, mwaka huu katika Viwanja vya Las Vegas, vilivyopo Mabibo jijini Dar es Salaam baada ya kuwa wasomaji wa magazeti ya Global Publishers ambayo ni Ijumaa, Championi, Uwazi, Ijumaa Wikienda, Amani na Risasi wamefanya droo ndogo tano, ambazo washindi waliweza kujipatia zawadi za aina mbalimbali, ikiwemo pikipiki, vyombo vya nyumbani, mashuka, ving’amuzi na vitu vingine kibao.

Majaba anakuwa mshindi wa pili kujipatia nyumba kutoka Global Publishers baada ya mwaka uliopita, msomaji mwingine mwenye makazi yake mkoani Iringa, Nelly Mwangosi kupata nyumba, ambayo nayo imejengwa Dar es Salaam eneo la Salasala, nje kidogo ya jiji.

Makala: Mwandishi Wetu.

Breaking News: CHADEMA Wampinga Sirro Kuhusu Marufuku ya Kutojadili Sakata la Lissu

 

Leave A Reply