The House of Favourite Newspapers

Mtatiro Atembea Km 14, Atatua Mgogoro Bonde la Mpunga

0

MKUU wa Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Julius Mtatiro amelazimika kutembea kilomita 14 kwa miguu kwenda na kurudi kwenye bonde la ulimaji mpunga la Mbunda wilayani Namtumbo.

 

Mtatiro ametekeleza wajibu huo akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo, Bi. Sophia Kizigo ambaye anatekeleza majukumu mengine maalum.

 

Akiwa na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma wamelazimika kutumia miguu kuwafikia wakulima walio katika mzozo juu ya bonde kwenye kijiji cha Kitanda.

 

Mmoja wa walalamikaji katika mgogoro huo, ambaye ni mkazi wa wilaya ya Songea, Andrew Mhagama, amemweleza DC Mtatiro kuwa yeye na wenzake wawili wamelima kwenye bonde hilo tangu mwaka 1990 lakini wanashangaa kuona mwaka 2020 serikali ya kijiji cha Kitanda ikiwaondoa kwenye bonde walilomiliki kwa miongo mitatu.

 

Uongozi wa kijiji cha Kitanda umeeleza umuhimu wa walalamikaji kufuata utaratibu wa kisheria wa kuomba kumiliki au kukodi ardhi hiyo kwa kutuma maombi yao kwa serikali ya kijiji.

 

Jambo lililovutia katika mchakato wa kulifikia bonde la Mbunda ni pale ambapo  Mtatiro alionekana kuendesha mchakamchaka usiokwisha na kuifanya safari ya kilomita saba kuwa fupi kwa walalamikaji, viongozi wa kijiji na Kamati ya Ulinzi na Usalama.

 

Idd Mohamed,
Namtumbo,
Oktoba 2, 2020.

 

Leave A Reply