Fenerbahce Yamtwisha Zigo Samatta

MSIMU  wa 2018/19 haukuwa msimu mzuri kwa Klabu ya Fenerbahce, wakiwa katika hali mbaya karibu na kushuka daraja, kilichotokea ni kumsajili Victor Moses raia wa Nigeria kwa mkopo kutoka klabu ya Chelsea, dirisha la Januari 2019.

 

Licha ya kuwa tayari walipoteza michezo mingi ya mwanzo, wakiwa wameshinda mechi tatu kati ya 18, walianza maisha mapya na Moses, chini ya Mkurugenzi wa Ufundi, Damien Comolli, walishinda mechi 12 zilizofuata na kumaliza ligi wakiwa nafasi ya nane, kutokana na ubora mkubwa wa Victor Moses.

 

Mabingwa hao wa mara 19 wa ligi ya Uturuki, walianza msimu wa 2019/20 kwa kasi ya hali ya juu sana, lakini matatizo mengi ya nje ya uwanja yaliwafanya wasiweze kufanya sajili za maana baada ya kufungiwa na UEFA kutokana na sheria ya FINANCIAL FAIR PLAY, walipambana kucheza msimu huo wakati pia Mkurugenzi wao Comolli alikuwa ameondoka tayari na kocha waliyekuwa naye akiwa ametimuliwa.

 

Mwisho wa siku Fener wakamaliza msimu uliopita nafasi ya saba, wakikosa kushiriki michuano ya kimataifa, imewalazimu wakae chini na kuanza na project mpya msimu huu, ikiwemo kupunguza sehemu kubwa ya wachezaji ambao hawakuwa na muhimu mkubwa kikosini mwao, wakiachana na wachezaji takribani 11 na kwenda sokoni kusaka wachezaji wapya.

 

Kwenye dirisha la usajili walikuwa wanahitaji wachezaji wenye uwezo wa kuja na kuleta utofauti mkubwa kama Victor Moses, kwenye maingizo mapya takribani 14 mchezaji Mtanzania, Mbwana Samata, naye jina lake limewekwa hapo.

 

Waturuki wanamuona Victor Moses kwenye sura ya Mbwana, wanaamini atawafikisha nchi ya ahadi, ubora wake kutoka Ligi ya Ubelgiji na uzoefu wake wa Ligi ya England ilikuwa vigezo tosha.  Waturuki wamepitia sana video za Mbwana kwenye YouTube wanaamini ni kama Alex de Souza aliyeteka mioyo yao, wanaamini zaidi kwenye wachezaji wa Afrika, kama ambavyo kaletwa Papis Demba Cisse.

 

Msimu uliopita Max Kruse, Mjerumani aliwaangusha Fenerbahce, sasa ni zamu ya Mbwana kupokea kijiti kile cha Mwafrika mwenzake, Victor Moses, na kuirudisha timu hiyo kwenye nne bora.


Toa comment