The House of Favourite Newspapers

Mtoto augua, miaka 10 avimba kisogoni

0

Gabriel Ng’osha na Suzan Kayogela

YA Mungu mengi! Hivyo ndivyo unaweza kusema ukimuona mtoto Joel Sabasi (11) mkazi wa Ifakara Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro, anayeteseka kwa muda wa zaidi ya miaka 10 na tatizo la kichwa chake kuvimba kisogoni, hali inayomfanya kusikia maumivu na kupata tatizo la kupoteza kumbukumbu mara kwa mara.

CHANZO CHA TATIZO
Akizungumza na Uwazi, baba mzazi wa mtoto huyo aliyefahamika kwa jina la Sabasi Bernad Mapande alisema;

“Tatizo hili lilimuanza tangu akiwa na mwezi mmoja ndipo tulianza kuona mabadiliko ya kichwa chake kuanza kukua kidogo kidogo upande mmoja wa kisogoni.

HOSPITALI YA MUHIMBILI
“Bila ya kupoteza muda tulimuanzishia matibabu katika Hospitali ya St.Francis iliyopo Ifakara, Morogoro.“Tangu mwaka 2004 alipoanza kuugua alikuwa akitibiwa hospitalini hapo mpaka Septemba 2, mwaka 2009 ndipo tulipewa rufaha ya kuja Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ili kupata matibabu zaidi.

“Tulipofika Muhimbili alifanyiwa vipimo na kupatiwa dawa lakini walisisitiza awe anakwenda kufanyiwa vipimo mara kwa mara, tatizo kubwa lililopo ni kutokuwa na fedha kwa ajili ya vipimo ambayo vinagharimu zaidi ya shilingi milioni moja na elfu sabini.

“Tuliambiwa akishafanyiwa vipimo ndipo itafahamika kama afanyiwe upasuaji au la, lakini kwa kweli mtoto anaumwa na anaumia sana maana kuna wakati usiku anashindwa kupata usingizi kutokana na maumivu makali kichwani.

“Nawaomba sana Watanzania wote msaada wenu ili kunisaidia pesa kwa ajili ya vipimo pamoja na matibabu ya mwanangu, naamini ukitoa chochote utakuwa umeokoa maisha ya mwanangu,” alisema Sabasi.

MGONJWA ANENA
Akizungumza na safu hii mtoto Joel ambaye ni mwanafunzi wa darasa la nne, Shule ya Msingi Mahutanga iliyoko Ifakara alisema;

“Nawaomba wasamaria wema wanichangie fedha ili baba anipeleke Muhimbili nikapatiwe vipimo kisha matibabu. Nawaomba sana msaada huo ili niweze kuendelea na masomo nikipona.”

Yeyote aliyeguswa na habari hii, awasiliane na baba mzazi wa mtoto huyu kwa namba 0684 585251 na 0659 585251.

Leave A Reply