The House of Favourite Newspapers

Mtoto Miaka 3 Auzwa Akatolewe Kafara!

omba-omba-kuwauza-watoto-w

Stori: Waandishi Wetu, Gazeti la Risasi Jumamosi

Dar es Salaam: Ni madai ya kushangaza! Kwamba, baadhi ya wanawake ombaomba waliopiga kambi maeneo ya Fire, Msimbazi na Baridi-Mnazi Mmoja jijini hapa, wameanza kuingiwa na tamaa ya fedha na kuamua kuwauza watoto wao kwa wafanyabiashara wakubwa kwa ajili ya kwenda kutolewa kafara au kuasiliwa bila utaratibu, Risasi Jumamosi limefanyia kazi.

Lakini madai hayo yakaenda mbali zaidi kwamba, mbali na watoto hao kwenda kufanyiwa kafara, wengine wamefikia hatua ya kuwanunua kwa ajili ya kuwalawiti ili kukidhi matakwa ya maelekezo ya waganga wa kienyeji.

TWENDE NA MTOA HABARI

“Inauma sana jamani, ndiyo maana matukio ya miili ya watoto kukutwa mahali yamekuwa yakisikika kila kukicha. Naamini kwamba watoto wengine ni wa ombaomba.

“Mfano siku za karibuni, kuna jamaa yangu mmoja alikuwa anatafuta mtoto wa miaka mitatu kwa ajili ya kumfanyia kafara la utajiri, akampata. Nina wasiwasi sana na hawa akina mama wanaoombaomba.

“Unajua wale hawana uchungu na watoto wao kwa sababu wamewazaa na wauza maji au watu wengine tu lakini hawakuwa na mpango nao.

omba-omba-kuwauza-watoto-waMama omba omba akiwa na mwanaye huyo.

MADAI YAFANYIWA KAZI

Baada ya madai hayo na ili kuona kama kweli yapo, Risasi Jumamosi likaona kazi hiyo inaweza kufanywa na kikosi cha Oparesheni Fichua Maovu ‘OFM’ cha Global Publishers.

Hiki ndicho kikosi pekee katika vyombo vya habari za uchunguzi ambacho kinaweza kuingia mahali pagumu pasipoingilika na kuchunguza chochote, hasa kwenye maovu.

OFM ilijiweka sawa, ikaingia mtaani na kuweka kambi kwenye maeneo yaliyotajwa ili kuwasaka wanawake hao na kuongea nao lengo likiwa ni kubaini ukweli wa madai hayo.

omba-omba-kuwauza-watoto-waOMBAOMBA WA MAENEO YA FIRE

OFM ilitua maeneo ya Fire na kukutana na baadhi ya ombaomba wanawake wa eneo hilo ambao wengi wao kwenye maongezi walionesha kutokubali kuzungumzia habari hiyo kwa sababu ya kutowajua wanaongea nao ni akina nani!

“Mimi sijui,” alisema mmoja wa ombaomba hao huku akihangalia huku na kule kisha akahama eneo alilokaa.

Ombaomba mwingine mwanamke alipofuatwa na OFM alisema kuwa, kuna mtu anafanya biashara hiyo lakini hakuwa anajua muda huo amepiga kambi wapi.

omba-omba-kuwauza-watoto-waOMBAOMBA WA MSIMBAZI

Baada ya kutoka Fire, OFM ilipiga hatua na kufika kwa wale wa Msimbazi, tena jirani na Kituo cha Polisi Msimbazi ambapo, mwanamke wa kwanza kukutana naye alionesha kuufahamu mchezo huo wa kuuza watoto. Ikawa hivi…

OFM: Habari yako mama?

Mama wa mtoto: Nzuri tu.

OFM: Samahani sana, kuna ishu ya pesa. Lakini samahani sana. Kuna tajiri mmoja, ana pesa lakini hajajaliwa kupata mtoto. Sasa anatafuta mtoto. Sijui anaweza kupata wa kumnunua?

Mama wa mtoto: Ana bei gani?

OFM: We ndiyo useme unataka kiasi gani?

Mama wa mtoto: Anakalia wapi?

OFM: Yeye ni mfanyabiashara.

Mama wa mtoto: Atampenda lakini?

OFM: Atampenda, yaani atamhudumia freshi.

Mama wa mtoto: Atanipa shilingi ngapi?

OFM: We ulikuwa unataka kiasi gani?

Mama wa mtoto: Milioni mia na hamsini (150,000,000).

OFM: Nyingi sana. Unajua mi mwenyewe ni mtu wa kati. Punguza kidogo. Maana si kwamba hutamwona tena, yeye anamnunua ili akawe mtoto wake, lakini wewe utakuwa huru kumwona. Tutaandikishiana kabisa.

Mama wa mtoto: Anipe milioni mia na hamsini.

OFM: Punguza kidogo. Nyingi sana.

Mama wa mtoto: Siyo nyingi. Unaweza kujenga nyumba moja ya ghorofa kama ile. Au ndogo mbili. Ye atatoa ngapi?

OFM: Milioni tano (5,000,000).

Mama wa mtoto: Ongeza kidogo, milioni kumi na tano (15,000,000). Nina wengi,  ye anataka mtoto gani?

OFM: Wa kiume. Kwani mtoto mwenyewe yuko wapi?

Mama wa mtoto: Ninao watatu. Si yule pale (mtoto anacheza pembeni ya mama yake).

OFM: Basi ngoja nikaongee na jamaa halafu nitakuja tena.

Mama wa mtoto: Sawa, utanikuta.

OFM: Sawa, si utakuwa hapahapa?

Mama wa mtoto: Hapahapa.

MTOTO HAJUI KITU, ACHEZA ZAKE

Maskini mtoto huyo, bila kujua kuwa, mama yake alikuwa kwenye biashara hiyo haramu ya kuuza binadamu (human trafficking) na alikuwa akifika bei kuhusu yeye, mwenyewe alikuwa akichezacheza eneo hilo.

OFM YABAINI HATARI KUBWA

Kama hali ipo hivyo, ina maana kwamba, kuna familia nyingi jijini Dar zina watoto wa kununua kwa mtindo huo wa wizi. Madhara ya watu kulea watoto wa staili hiyo ni kuingiza tabia isiyofanana na asili ya ukoo katika nyumba. Ni vyema kutumia njia halali kuwaasili watoto kutoka kwenye vituo vya kulea watoto.

Lakini pia, inaonekana wale watoto wanaokutwa wamekufa wakiwa wamefanyiwa vitendo vya ukatili, si ajabu kabisa wametoka kwenye kununuliwa kwanza kutoka kwa wazazi wa aina hii.

Ni vizuri kama serikali kupitia taasisi husika wakavalia njuga ishu hizo ili kumaliza kama si kukomesha biashara hiyo haramu kwenye jamii.

SIRO, MAKONDA WASAKWA

Hata hivyo, gazeti hili liliwasiliana na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, CP Simon Siro ili kumweleza kuhusu uhalifu huo unaodaiwa kushamiri ambapo simu yake ilipokelewa na msaidizi wake aliyedai kuwa kamanda huyo yupo kwenye kikao lakini atamfikishia ujumbe.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama ya Jiji, alipotafutwa kwa njia ya simu na kuelezewa mkasa huo, alifunguka:

“Kwanza ni kosa kisheria, wakati tunataka kuwaondoa jijini watu wa haki za binadamu walipiga kelele ni vizuri nao wakalijua hilo. Natumia nafasi hii kuviagiza vyombo vya dola kufuatilia kiundani ili sheria ichukue mkondo wake na kama mlivyosema mna ushahidi inaweza kusaidia sana mtu huyo kufikishwa mahakamani.”

Comments are closed.