MUME AMNUSISHA KIFO MKEWE!

KATIKA ndoa za siku hizi, wakati mwanaume na mwanamke wakikutana na kukubaliana kuoana, utadhani hakuna jambo baya linaloweza kutokea kati yao miaka kadhaa baadaye, Uwazi lina kisa cha kusikitisha.

KUMNUSISHA KIFO

Mwanaume mmoja aliyetajwa kwa jina la Michael anadaiwa kumnusisha kifo mkewe wa ndoa, Aida Michael (21) ambaye ni Mungu tu aliyemnusuru la sivyo tungekuwa tunazungumza mengine. Katika tukio hilo la kusikitisha kwa wanandoa hao waliopendana na kuamua kuwa mume na mke, Michael alidaiwa kumchoma na kumjeruhi Aida sehemu za matiti kwa kutumia maji ya moto na kumwachia majeraha yasiyotazamika.

Tukio hilo lilijiri hivi karibuni na kuacha gumzo kubwa katika Mtaa wa Mjimwema Kata ya Boma mjini Mafinga- Mufindi katika Mkoa wa Iringa.

UKATILI USIKU WA MANANE

Kwa mujibu wa Aida na maelezo yake aliyoandikishwa kwenye Kituo Cha Polisi cha Mafinga, Michael alimfanyia ukatili huo usiku wa manane alipokuwa amerejea nyumbani kutoka kwenye ulevi.

MUME AKAMATWA, AACHIWA

Aida alilieleza Uwazi kuwa, baada ya mumewe kumnusisha kifo, alikwenda kutoa taarifa Kituo cha Polisi cha Mafinga na kupewa fomu ya matibabu (PF-3) kisha kufunguliwa jalada la uchunguzi namba MFG/ RB/37/2019-KUDHURU MWILI. Mwanamke huyo alisema kuwa wakati akiendelea na matibabu, Michael alikamatwa, lakini baada ya siku mbili alidhaminiwa na kuachiwa wakati hali yake ikiwa mbaya.

AIDA ALILAZWA KATIKA HOSPITALI YA MAFINGA.

Hata hivyo, alisema kuwa, baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya, mama mdogo wake aliyefamika kwa jina la Florah Soteli (50) kutoka Sumbawanga mkoani Rukwa alifika Mafinga kujua kilichompata na kumuuguza.

KITUO CHA POLISI MAFINGA

Alisema kuwa mama yake mdogo alipofika, alikwenda Kituo cha Polisi cha Mafinga ili kujua namna binti yake atakavyopatiwa matibabu kwa kuwa mume wake, baada ya kudhamiwa alitoweka nyumbani na kutokomea kusikojulikana.

Aida alisema kuwa Florah alikwenda moja kwa moja kwenye Dawati la Jinsia kituoni hapo, lakini katika hali ya kusikitisha hakupata ushirikiano wa kutosha ikiwa ni pamoja na kusumbuliwa kupata PF-3 nyingine baada ya ile ya awali kuchukuliwa na Michael. Alisema Florah alielezwa na ofisa mpelelezi wa kituo hicho aliyetajwa kwa jina la Mwanaisha Khamis kuwa, suala hilo lilikuwa kwenye uchunguzi hivyo binti yake akipona ataendelea na kesi.

MKUU WA WILAYA

Aida alidai kuwa, baada ya Florah kuona hana msaada na kukosa ushirikiano kituoni hapo, alilazimika kwenda kwa Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Jamhuri David ili apatiwe kibali cha mchango aweze kumtibu mwanawe na nauli ya kurejea Sumbawanga. Alisema akiwa kituoni hapo ndipo Florah akakutana na Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Mafinga ambaye aliamuru askari wamkamate Michael haraka iwezekanavyo.

“Mkuu wa kituo alilazimika kuandika barua yenye kumbukumbu namba MFG/B.1/4/VOL.1/254 ikiomba kutolewa msaada kwa yeyote kutuwezesha kusafirishwa kwenda Sumbawanga. “Katika hilo, pia askari wa usalama barabarani walilazimika kutuombea tusaidiwe kwenye mabasi tofauti. “Mimi nilipakiwa kwenye basi la New Force huku mama yangu mdogo akiwa amesaidiwa kwenye basi la Majinja,” alisimulia Aida.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Florah, hali ilikuwa mbaya kwa mgonjwa (Aida) hivyo walilazimika kushuka jijini Mbeya ili kupatiwa matibabu kisha kuendelea na safari na hakukuwa na mawasiliano na Michael ambaye alikuwa akisakwa na polisi.

KAMANDA IRINGA

UWA ZI lilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, ACP Juma Bwire Makanya ili kujua mustakabali wa suala hili ambapo alisema suala hilo hana taarifa nalo na kuahidi kulifanyia kazi. “Hilo suala sina taarifa nalo lakini nitafuatilia na kulifanyia kazi,” alisema kamanda huyo.

STORI: MWANDISHI WETU, IRINGA

Loading...

Toa comment