The House of Favourite Newspapers

Mwamuzi Aliyempa Kadi Nyekundu Chirwa Adai Alirogwa

KATIKA hali ya kushangaza, mwamuzi Ahmad Simba, ambaye wiki iliyopita alitoa maamuzi ya utata kwenye mechi ya Yanga dhidi ya Ruvu Shooting, amejitetea kwamba alifanya maamuzi hayo akiwa hajielewi kutokana na kurogwa. Simba alimtoa straika wa Yanga, Obrey Chirwa kwa kumpa kadi nyekundu kwenye mechi baina ya timu hizo iliyofanyika katika Uwanja wa Taifa, Dar ambapo ilimalizika kwa Yanga kushinda mabao 2-0.

Hata hivyo, marudio ya video ya mchezo huo yalionyesha kuwa Chirwa hakuwa amefanya kosa lolote kabla hajakwamisha mpira kimiani. Mmoja wa mabosi wa Chama cha Waamuzi wa Soka Tanzania (Frat) ambaye hakupenda kutajwa jina, ameliambia Championi Jumatano kuwa mwamuzi huyo aliweka maelezo hayo kwenye ripoti aliyoiwasilisha kwao muda mfupi baada ya mechi hiyo kumalizika na kuainisha sababu za kumpa kadi Chirwa.

“Mechi yoyote inapomalizika huwa kuna ripoti ambayo inawasilishwa na mwamuzi husika pamoja na kamishna wa mechi juu ya matukio mbalimbali ambayo yanakuwa yametokea kwenye mechi kwa ajili ya kupewa alama za kiuchezeshaji ambazo hupatiwa waamuzi wote.

“Kamati ilikuwa inasubiri sana ripoti hiyo ya mwamuzi kwa kuwa wengi waliona mazingira ya ile kadi. “Sasa kwenye maelezo yake akaeleza sababu ya kadi ya Chirwa ambayo ilikuwa gumzo kwenye mechi ile kwa kuwa alimpa kimakosa baada ya kufunga bao la wazi yeye akidhani aliushika mpira huo. “Kasema kwamba alishindwa kuendana na spidi ya mchezo kwa sababu alikuwa anajihisi kama amerogwa jambo ambalo lilimfanya aboronge kwa kufanya maamuzi mengi ambayo yalikuwa yana utata ndani yake.”

Hata hivyo, jana jioni taarifa zilitoka kwamba, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limemuondoa mwamuzi huyo katika orodha ya waamuzi watakaochezesha mechi za Ligi Kuu Bara na kudai kuwa hata kama akiitwa kwenye kamati ya waamuzi atazungumza mambo yaleyale aliyoandika katika ripoti yake ambayo Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas, hakutaka kuyataja mambo hayo.

Comments are closed.