The House of Favourite Newspapers

Mwanamke Alivyomfanya Zezeta Kaka Yangu – 30

0

ILIPOISHIA
Wakati tunaendelea kunywa maji yule bosi polisi alitoka mezani kwake na kuungana nasi. Tulisalimiana na mazungumzo yakaanza.
Tulimueleza kisa cha kuja pale na jinsi taarifa za kifo tulivyopata na mganga anavyoona.

“Yule mama tunamjua, ni kweli ana tabia hiyo, ngoja niandae polisi twende. Safari hii nataka nikashuhudie mwenyewe,” alisema. SONGA NAYO…

Tuliendelea kunywa maji wakati yule mkuu wa polisi, idara ya upelelezi akiondoka ofisini kwake na kutoka nje.

Hakuchukua muda mrefu alirudi na akaenda moja kwa moja kwenye meza yake na kuanza kupekua jalada moja huku akijikuna kichwani.
Alinyanyua simu ya mezani na kuanza kuzungumza:
“Haloo. Njoo na dispachi nataka upeleke jalada moja kwa mwendesha mashtaka.”

Baada ya kusema hayo sekunde chache baadaye aliingia kijana mmoja akiwa na magwanda ya polisi akapiga guu chini huku akitoa saluti kwa mkuu wake. Alipewa jalada na bila kuambiwa chochote aligeuka na kupiga guu, kisha kutoweka katika ofisi ile. Bila shaka alikuwa akiijua vema kazi yake aliyotumwa.

“Sasa jamani twendeni kwa huyo mwanamke aliyemfanya zezeta kaka yenu,” alisema kamanda yule wa polisi wa idara ya upelelezi.
Alichukua kofia yake ambayo ilikuwa imetundikwa kwenye moja ya viwekea kofia au koti katika ofisi ile.

Ilikuwa kofia yenye ‘ungaunga’, baada ya kuona hivyo nilimuangalia mtu yule kwenye mabega yake nikagundua kuwa ni mtu mkubwa ndani ya jeshi la polisi.

“Kumbe ni mtu mkubwa!” nilimnong’oneza mzee Makang’ako.
“Huyu ni mkuu wa upelelezi wa wilaya,” akanijibu.

Tulitoka nje na kukuta kuna gari mbili za polisi zimeandaliwa kwa safari hiyo. Moja lilikuwa na polisi kama sita hivi wenye silaha nzito yaani SMG na gari nyingine tulipanda sisi na mkuu huyo wa polisi pamoja na sangoma wetu.

Ndani ya gari hakukuwa na mtu yeyote ambaye alikuwa akiongea chochote, nadhani kila mmoja alikuwa akiwaza yake, mimi nilikuwa namfikiria kaka yangu huku nikimuomba Mungu kwamba nimkute akiwa hai.

Lakini nilikuwa namuomba Mungu pia kwamba tukimkuta hai, basi iwe rahisi kwa mganga wetu kumrudishia fahamu zake ili awe mtu wa kawaida.

“Litakuwa jambo baya sana kama tutamtoa katika kifungo cha kuwa msukule lakini akili yake ikawa ya kizezeta, itakuwa hakuna tulichofanya.”

Gari zote mbili za polisi pamoja na gari la tatu la mzee Makang’ako zilikuwa zikienda kwa mwendo wa kasi kuelekea kwa yule mama mkatili na zote ziliwasha taa za mbele japokuwa ilikuwa ni mchana kweupee.

Pale tulipokuwa tukikuta msongamano wa magari lile gari lililokuwa mbele lilikuwa likipiga king’ora na tukawa tunapishwa.

Tulifika katika geti la yule mwanamke na polisi wakashuka huku wakiwa na silaha zao. Sisi tuliambiwa tusishuke mpaka kwanza polisi wapate uthibitisho kwamba yupo.

Je, watamkuta huyo mwanamke aliyemfanya kaka yao zezeta? Fuatilia Jumanne ijayo.

Leave A Reply