The House of Favourite Newspapers

Mwanamke alivyomfanya zezeta kaka yangu -36

0

ILIPOISHIA
Hata hivyo, baada ya sekunde chache aliwaamuru wale askari aliokuwanao ndani wamtoe nje, wakamtoa.
“Huyu ndiye ndugu yenu?” aliuliza yule mganga.
“Dah kaka Edgar,” nilisema huku nikimkimbilia na kwenda kumkumbatia. Alikuwa amedhoofu na hakika hakuwa na siha njema, mwili wote uliporomoka akabaki mifupa mitupu.
Je, nini kitatokea? SONGA NAYO:
Nililia sana huku nikiwa nimemkumbatia kaka lakini yeye alikuwa haoneshi kunijali ni wazi alikuwa zezeta, hakuwa na uwezo wa kusema lolote japokuwa alikuwa akiniangalia na mbaya zaidi alikuwa akitokwa na udenda kwani hata fulana nyeusi aliyokuwa ameivaa ililowa kifuani.
“Kaka Edgar, kaka Edgar,” niliita huku nikitokwa na machozi lakini yeye akawa ananikodolea macho kama vile alikuwa hasikii kama anaitwa.
Nilipandwa na kisirani sana kuona kaka yangu ambaye wiki mbili au tatu zilizopita nilimuacha akiwa anaweza kutembea japo kwa kujikongoja, leo hawezi hata kututambua sisi ndugu zake.
Kaka Ipacho Mavaka naye alionekana kupandwa na hasira kwani alikunja sura huku jasho likimtiririka kwenye paji la uso wake.
Nilimuangalia yule mwanamke aliyemfanya zezeta kaka yangu, nikamfuata alipokuwa amesimama, ilibidi akimbie kwani alijua kwamba nitaweza kumuumiza kwa hasira.
Nilipomuona anakimbia nami nikawa namkimbiza mle ndani ya ua wa nyumba yake. Alijikwaa akaanguka kabla ya kulifikia geti kubwa jeusi. Nilimuwahi, nikamshika kisha kumpiga vibao viwili vitatu mashavuni. Mbwa wake alikuwa anabweka, bahati ni kwamba alikuwa amefungwa mnyororo.
Nilishtukia askari mmoja akiwa ananishika shati:
“Hapana usifanye hivyo, kumpiga mhalifu ni kuvunja sheria za nchi, unaweza kufunguliwa mashtaka,” alisema askari huyo aliyekuwa nyuma yangu.
“Wewe mwanamke ni katili sana, kweli unatudanganya kwa kutupigia simu kwamba kaka yetu ni mgonjwa, baadaye ukasema amefariki dunia kumbe umemfanya msukule, umemfanya zezeta? Shetani mkubwa wewe,” nilifoka.
Pale kwenye geti la nyumba yake kulijaa watu na walijazana kutokana na kuyaona magari mawili ya polisi.
“Koplo Fidea! Mchukue huyo mama, mfunge pingu kisha muingize kwenye gari.” Ilikuwa ni amri ya Inspekta Ben Matwanga.
Haikuchukua dakika mbili, tayari mwanamke yule mkatili alikuwa amefungwa pingu na kutupwa nyuma ya Defenda ya polisi pamoja na wale watu, yaani kaka yangu na yule mtu mwingine ambaye hatukuwa tunamjua.
Nilishangaa sana nilipowaona waandishi wa habari hasa wa MBC TV, kituo cha televisheni kinachoangaliwa na watu wengi pale Lilongwe wakiwa wamefika.
Waandishi hao walikuja moja kwa moja kwangu kutaka kuhojiana nami na kamera zao za kurekodi zikiwa begani.
“Haloo, tunaomba kuongea na wewe dakika chache,” alisema kijana mmoja ambaye alikuwa amevaa kizibao kilichoandikwa MBC TV TEAM.
“Kuhusu nini?” nilimuuliza.
“Kuhusu tukio hili la kustaajabisha.”
“Lipo chini ya polisi, ungezungumza na kamanda pale,” nilisema huku nikimuelekeza kwa Inspekta Ben Matwanga.
“Lakini tumeambiwa wewe ndiye mhusika mkuu.”
“Hapana, mhusika mkuu ni kamanda wa polisi. Tumekuja hapa kwa amri yake.”
“Sawa, lakini watu wanasema mmoja wa wale watu waliodhoofu ni ndugu yako na ndiyo maana tukaamua kukufuata ili tujue historia nzima ya tukio hili tafadhali.”
“Unitafute kwa wakati wako, sehemu nyingine na siyo hapa. Hapa mamlaka yake ni ya polisi kama nilivyokufahamisha,” nilizidi kusimamia msimamo wangu.
Yule kijana alipoona amegonga mwamba alikwenda kwa Inspekta Ben lakini hata kabla ya kumuuliza chochote alikuwa ameshapanda gari la polisi nalo likaanza kuondoka.
Sisi kwa kuwa tulikuwa na gari dogo ambalo lilikuwa likiendeshwa na mwenyeji wetu, Bwana Makang’ako, tulipanda mle na msafara wa magari matatu ukaanza. Mbele kulikuwa na gari lililokuwa na mtuhumiwa na kaka na yule mtu na polisi wenye silaha.
Katikati kulikuwa na gari ambalo alipanda kamanda wa polisi na askari wengine wenye silaha na taratibu magari hayo yakaanza kutoka ndani ya geti la nyumba ya yule mwanamke aliyemfanya kaka yangu zezeta.
Nje ya geti kulikuwa na watu wengi ambao walikuwa na shauku kubwa ya kujua nini kimetokea katika nyumba ile.
“Kuna maiti zimekutwa kwenye banda,” alisikika mtu mmoja akisema, nilijua kuwa kwenye tukio kama hilo watu kama hao ambao hujitungia maneno huwa hawakosi.
Gari letu kwa kuwa lilikuwa la mwisho kutoka katika geti la yule mama na kwa kuwa getini watu walijaa mno, niliweza kusikia maneno mengi ya watu tofauti.
“Hapana, mle kwenye gari kuna misukule wanne,” nilisikia mtu mwingine akisema. Nikajiambia kimoyomoyo kwamba huyo kapatia lakini amekosea idadi ya misukule kwani siyo wanne kama anavyowaambia wenzake.
Msafara huo ulianza kuongeza mwendo, mara simu ya Bwana Makang’ako ikaita;
“Ni Inspekta Ben Matwanga, sijui anasemaje,” akasema.
“Pokea usikie,” akasema kaka Ipacho.
Simu yake akabonyeza sehemu tukawa tunasikia wote:
“Halooo, tunaelekea hospitali moja kwa moja.”
“Sawa, ngoja niwaulize ndugu zake tuwapeleke hospitali gani,” alituuliza lakini Bwana Makang’ako akasema tuwapeleke Hospitali ya Misheni ya Malamulo kwani ina ubora wa hali ya juu.
Niliwaza na kujiona sina fedha za kutosha nikajisemea moyoni kwamba nisijifanye mjanja halafu baadaye nikwame.
“Mzee huko mbona fedha hatuna?” nilisema huku nikimuangalia kaka Ipacho.
“Hilo siyo tatizo. Nitalipa mimi hata kama tutadaiwa shilingi milioni kumi,” alijibu.
Nilifarijika na moyo wa huruma aliouonesha Bwana Makang’ako. Wakati nawaza hilo naye akadakia.
“Unajua hospitali ya kulipia ni bora na huyu mama anajulikana sana, anaweza kucheza mchezo tukampoteza ndugu yetu, fedha ni nini bwana, huwa zinatafutwa na kutumika, roho utaipata wapi ikipotea?”
“Kweli mzee, nakushukuru sana.”
Usikose kusoma muendelezo wa simulizi hii wiki ijayo.

Leave A Reply