The House of Favourite Newspapers

Mwanamke Jini Alivyonipenda na Kunipeleka Ujinini! – Sehemu ya 1

0

NAITWA Omar Ibrahim Msangi.  Nilikuwa ndiyo kwanza nitimize umri wa miaka thelathini.  Masomo niliyochukua yalikuwa ni ufundi wa kompyuta na nilikuwa nimeajiriwa na kampuni binafsi iliyokuwa  ikishughulika na uuzaji wa aina zote za kompyuta na utengenezaji.  Mimi nilikuwa upande wa ufundi na nilikuwa fundi mkuu.

 

Hii kampuni ilikuwa ya mfanyabiashara mmoja mwenye asili ya Kiasia.  Mtoto wake mmoja nilisoma naye. Baada ya kumaliza masomo yake akaenda Ulaya.  Yeye ndiye aliyefanya mpango wa mimi kuajiriwa na kampuni ya baba yake kwa sababu alikuwa akiujua utaalam wangu.

Sisi tulizaliwa wawili tu, mimi na mdogo wangu wa kike aliyekuwa akiitwa Farida.  Yeye alisomea uuguzi, akapata ajira kwenye hospitali binafsi.  Wazazi wetu walikuwa marehemu.  Alitangulia kufa baba kisha akafuatia mama.

 

Nataka nieleze kitu kimoja kuhusu baba yangu.  Wakati wa uhai wake alikuwa akivaa pete ambayo sikuweza kujua ilikuwa na madini gani lakini ilikuwa na kito cha feruzi.  Siku alipokufa nilikuwa naye.  Dakika chache kabla ya kuaga dunia alivua ile pete akanivisha mimi.

Baada ya marehemu baba kunivalisha ile pete haukupita muda mrefu akaaga dunia.  Mpaka hii leo pete hiyo iko kidoleni kwangu.

Kwa vile wazazi wetu walipokufa nilikuwa nimeshanza kazi, nikabaki na mdogo wangu ambaye alikuwa bado anasoma.  Na yeye alipomaliza masomo yake nikamtafutia kazi na kufanikiwa kumpatia nafasi katika hospitali moja iliyokuwa inamilikiwa na kanisa.

 

Mwanzo tulikuwa tukiishi pamoja nyumbani kwetu Chuda mkoani Tanga.  Lakini alipopata kazi Farida alijitenga.  Alitafuta nyumba ya kupangisha akafanikiwa kupata nyumba moja ya Msajili wa Majumba eneo la Chumbageni.

Miezi miwili tu baada ya Farida kuhamia Chumbageni nilipokea barua mbili za posa yake.  Barua iliyowasilishwa kwanza ilitoka kwa daktari mmoja ambaye Farida alikuwa akifanya naye kazi.  Barua ya pili ilitoka kwa kijana mmoja aliyekuwa akiishi maeneo ya Nguvumali.

Farida mwenyewe aliniambia alikuwa  amempenda yule daktari.  Yule kijana mwingine alikuwa na pesa.  Tatizo lake alikuwa akifanya biashara ya madawa ya kulevya.

 

Nikaikataa posa ya kijana huyo na kuikubali posa ya daktari kutokana na uchaguzi wa Farida mwenyewe.

Baada ya kujibu ile barua ya daktari, taratibu nyingine zikafuata ikiwemo kutolewa mahari ya Farida mwenyewe. 

Nakumbuka ulikuwe ni mwezi wa pili na ndoa ya Farida ilipangwa ifanyike mwezi wa tano.

Wakati Farida yuko kwenye maandalizi ya ndoa yake, kwa upande  wangu kulikuwa na msichana wangu ambaye nilipanga kuja kuoana naye baada ya Farida kuolewa.  Alikuwa anaitwa Mishi.

Siku moja likatokea tukio ambalo liliniumza sana.  Ilikuwa siku ya Jumapili ambayo siendi kazini.  Niliamka asubuhi na kuanza kufua nguo zangu, ghafla simu yangu niliyokuwa nimeiweka pembeni ilitoa mlio wa kupokea meseji.

 

Nikaichukua na kuifungua meseji iliyoingia.  Ilikuwa inatoka kwa Farida.  Iliandikwa hivi: OMAR NJOO HARAKA NYUMBANI.

Ile meseji kidogo ilinishtua, nikajiuliza Farida amepatwa na nini.  Lakini sikupata jibu.  Jambo lingine lililonitia shaka ni jinsi Farida alivyonitaja kwa jina langu.  Mara nyingi Farida huniita kaka na si Omar.

Nikaona nimpigie ili nijue kulikoni.  Nilipiga simu yake mara mbili lakini simu ilikuwa ikiita tu bila kupokelewa, jambo ambalo lilizidi kunitia wasiwasi.

 

Nikaacha kufua nikaondoka nyumbani na kwenda kupanda bodaboda iliyonifikisha katika nyumba aliyokuwa anaishi huko Chumbageni.  Ilikuwa nyumba ya vyumba sita lakini iligawanywa katika pande mbili.  Kila upande ulikuwa na vyumba vitatu na ulikuwa ukijitegemea.

Farida alikuwa amepangisha upande mmoja na upande mwingine ulikuwa na mpangaji mwenzake.  Kila upande ulikuwa na mlango wake.

 

Nikabisha mlango wa Farida.  Sikupata jibu.  Nikaona niufungue niingie ndani.  Nilipoingia sikuamini macho yangu kwa kile nilichokiona sebuleni.

Farida alikuwa amelala chini kwenye dimbwi la damu mbichi.  Alikuwa amelala kichalichali huku kisu chenye mpini wa nchi nne kikiwa kimezama kwenye kifua chake. 

Macho yakeyalikuwa wazi lakini yalionyesha kutoona chochote.  Yalinidhihirishia wazi kuwa mdogo wangu alikuwa ameshakufa.

 

Huku mwili wangu ukitetemeka nilijaribu kumuita mara mbili.

“Farida!  Farida!”

Farida alikuwa kimya.  Nikachutama na kumtazama vizuri huku nikijiuliza.  Farida amepatwa na nini.  Ni dhahiri kuwa kuna mtu aliyeingia na kumchoma kisu.

Nikahisi labda palitokea wizi.  Wazo kwamba kuliingia wezi lilinifanya niyazungushe macho yangu pale sebuleni.  Lakini niliona kila kitu kilikuwa sawa.  TV ilikuwepo, sabuufa ilikuwepo pamoja na vitu vingine ambavyo kama kuliingia mwizi lazima angevichukua.

 

Nilijiambia hakukuingia wezi, aliyeingia alikuwa muuaji.  Nikasimama na kutoa simu yangu.  Nikawapigia polisi.

Haukupita muda mrefu polisi wakafika.  Wao pia walipomuona Farida walishtuka.

“Nini kimetokea?” polisi mmoja akaniuliza.

Nikamweleza kwamba yule alikuwa mdogo wangu tumbo moja na mimi.  Nikaendelea kuwaeleza jinsi nilivyotumiwa ile meseji na nilivyofika pale nyumbani na kukuta amechomwa kisu.

 

Je, nani amemuua Farida na kwa sababu gani?  Utapata jibu la swali hilo Jumatatu hapahapa.

Mtunzi: Faki A. Faki

Magufuli Awataka Wananchi Kutumia Fursa ya Bomba la Mafuta Kujenga Maisha

Leave A Reply