The House of Favourite Newspapers

Mwigulu atoa tamko Bashe…

0

Na Mwandishi Wetu GPL/ Uwazi

D ODOMA: Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba jana alitoa tamko kufuatia madai ya Mbunge wa Nzega Mjini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Hussein Mohamed Bashe kuomba mwongozo wa Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson akitaka kuahirishwa kwa shughuli za kawaida za bunge ili kutoa nafasi kwa wabunge kujadili matukio ya utekaji watu yanayoendelea nchini kwa sasa akidai kuwa, na yeye ni mmoja wa walengwa wa kutekwa.

Bashe (pichani) alisema kuwa, ametumiwa ujumbe wa vitisho na watu wasiojulikana wakisema kuwa watamfanyia kitu kibaya popote pale alipo.

Bashe ambaye yupo kwenye vikao vya bunge vinavyoendelea mjini Dodoma, jana aliandika kupitia akaunti zake za Mitandao ya Twitter na Instagram:

“Kuna watu wamenitumia ujumbe kwamba mimi ni kati ya watu 11 waliopo hatarini kufanyiwa vitu vibaya popote pale tulipo.

“Bunge na serikali haviwezi kulifumbia macho jambo hili haramu wakati Watanzania wanatekwa na watu wasiojulikana.”

Kufuatia vitisho hivyo, Bashe alilitaka bunge na serikali kutofumbia macho vitendo hivyo vya wananchi kutekwa na watu wasiojulikana.

Baada ya maelezo hayo ya Bashe, Uwazi lilizungumza na Waziri Mchemba kuhusu kauli hiyo ambapo alisema:

“Mimi nimemsikia, sijapata fursa ya kumuuliza, lakini serikali tutapambana na watekaji wote wanaotaka kuichafua serikali ya awamu ya tano.

Nia ya serikali ni kutaka watu wake waishi kwa amani katika nchi yao.”

Hivi karibuni kumekuwa na malalamiko ya Watanzania kutokana na watu kutekwa ambapo msanii Ibrahim Musa ‘Roma Mkatoliki’ na wenzake watatu na Msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Ben Saanane imedaiwa walitekwa na watu wasiojulikana.

Hata hivyo, wakati Roma na wenzake walipatikana Jumamosi iliyopita, Ben Saanane hajaonekana tangu Novemba 8, mwaka jana na haijulikani alipo licha ya kupigwa kelele na taasisi na watu mbalimbali kuhimiza vyombo vya dola vimtafute.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba alipoulizwa juu ya matukio hayo ya

utekaji alisema; “Tutahakikisha watekaji wote wanatiwa mbaroni.”

Naye Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe alisema jana kwamba, ameelekeza upelelezi juu ya tukio la kutekwa kwa Roma na wenzake ambao unafanyika kwa umakini mkubwa.

Leave A Reply