The House of Favourite Newspapers

Mwili wa Dada’ke Ndugai Waagwa Dodoma

0

 

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, jana (Jumatatu, Januari 25, 2021) alishiriki mazishi ya dada wa Spika wa Bunge, Job Ndugai, aitwaye Mary Ndugai, aliyefariki dunia Januari 23, 2021, wilayani Mpwapwa, Dodoma. Mazishi hayo yalifanyika katika makaburi ya Ving’awe wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma.

 

 

Akizungumza baada ibada ya kumuombea marehemu Mary iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania jimbo la Mpwapwa, Majaliwa aliwaomba wafiwa wawe na subira na utulivu katika kipindi hiki kigumu.

 

 

“Nimekuja kuungana nanyi kwa niaba ya Mheshimiwa  Rais Dkt. John Pombe Magufuli na Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan kutoa pole kwa Mheshimiwa Spika Job Ndugai kufuatia msiba mzito wa kuondokewa na dada yake mpendwa Mary,” alisema.

 

 

Aliongeza kwamba msiba huo ni mzito na jukumu kubwa ni kumuomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu pahali pema, hivyo amewaomba watoto wa marehemu, ndugu na jamaa wawe watulivu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.

 

 

Ndugai aliwashukuru viongozi wa dini, serikali na waombolezaji kwa kujitokeza na kuifariji familia kufuatia msiba huo. Pia aliwashukuru madaktari na wauguzi wa Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa ambako marehemu alikuwa akitibiwa.

 

Leave A Reply