The House of Favourite Newspapers

Nabi Aiongoza Yanga Kininja Dhidi ya Azam leo, Dube Tishio Kwake

0

REKODI zinaonesha kwamba, Oktoba 15, 2008, ilikuwa mara ya kwanza Yanga kukutana na Azam kwenye Ligi Kuu Bara ambapo matokeo ya mchezo huo, Yanga iliikaribisha vizuri Azam kwenye michuano hiyo kwa kuichapa mabao 3-1.

 

Huo ndiyo ulikuwa msimu wa kwanza kwa Azam kucheza Ligi Kuu Bara. Leo Jumapili, timu hizo zinakutana tena Uwanja wa Mkapa, Dar, ukiwa ni mchezo wa 26 ndani ya ligi hiyo.

 

Safari hii ushindani unatarajiwa kuwa mkubwa zaidi kutokana na nafasi za timu hizo kuelekea mechi za mwisho za kumalizia msimu huu wa 2020/21.Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Azam Complex, Dar, Yanga ilishinda 1-0, mfungaji akiwa Deus Kaseke dakika ya 48.

Wakati ule, Benchi la Ufundi la Yanga liliongozwa na Cedric Kaze raia wa Burundi, huku lile la Azam likiongozwa na Mromania, Aristica Cioaba.

 

Katika mchezo wa leo, makocha hao wote hawapo baada ya kutimuliwa.Kauli ya pisha njia itatumiwa na kila upande kwani Yanga yenye pointi 57, itataka kushinda mchezo wa leo ili kurudi kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo, huku Azam yenyewe ikitaka ushindi kwa namna mbili; kupunguza wigo wa pointi dhidi ya Yanga na kulipiza kisasi kutokana na kupoteza mchezo wa kwanza nyumbani.Katika mechi 25 zilizopita baina ya timu hizo kwenye Ligi Kuu Bara, Yanga imeshinda tisa, Azam nane na sare nane.

 

KAULI ZA MAKOCHA

Kocha wa Makipa wa Yanga, Razak Siwa, amesema: “Ni mechi ya ushindani ukizingatia wapinzani wetu Azam FC wanahitaji kulipa kisasi, sisi pia tunahitaji kupata pointi tatu.“Wachezaji wapo fi ti, lakini tunaweza kumkosa Tuisila Kisinda.

 

Kocha Msaidizi wa Azam, Vivier Bahati, alisema: “Mechi ya kwanza tulipoteza nyumbani, sasa hatutakubali kupoteza tena, tutacheza kwa kuiheshimu Yanga na tutaingia kwa kutafuta matokeo mazuri.

NABI KUIONGOZA YANGA KININJA

Kuna uwezekano mdogo wa Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi kukaa kwenye benchi la ufundi la timu hiyo leo, hii inatokana na ishu ya vibali vyake vya kazi hadi jana jioni vilikuwa vinashughulikiwa na bado havikukamilika.

Nabi aliyejiunga na Yanga hivi karibuni kwa mkataba wa mwaka mmoja na nusu akichukua mikoba ya Cedric Kaze raia wa Burundi, Alhamisi ya wiki hii alianza kuinoa timu hiyo mazoezini, lakini uhakika wa kukaa benchi leo ni mdogo.

Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Haji Mfi kirwa, ameliambia Spoti Xtra kuwa walichokifanya ni kuanza kazi kwa kocha huyo wakati wakiwa wanashughulia mambo mengine ya msingi kuelekea katika mchezo wa leo Jumapili.

 

“Kocha yupo kambini na ameanza kazi kwa ajili ya mchezo wetu dhidi ya Azam, kuhusu mambo mengine kwamba atakaa benchi au la, yatajulikana siku ya mchezo.

 

“Lakini jambo kubwa ni kwamba yeye ndiye ataiongoza timu katika mchezo huo, sasa kama atakuwa kwenye benchi au jukwaani itafahamika kwa kuwa bado kuna mambo ya msingi ambayo yanahusisha nchi tunaendelea kuyapigania ili kuona kila kitu kinakuwa sawa.”

MWAMBUSI AREJEA

Kaimu Kocha Mkuu wa Yanga, Juma Mwambusi, jana Jumamosi alirudi kambini na leo Jumapili atakuwa kwenye benchi la ufundi la timu hiyo kucheza dhidi ya Azam.Mwambusi aliondoka mara moja kambini akienda Mbeya kuhani msiba wa ndugu yake uliyotokea Alhamisi wiki hii.

 

Akizungumza na Spoti Xtra, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Yanga, Hassan Bumbuli, amesema: “Naomba mashabiki na wapenzi wetu wafahamu kuwa, bado benchi lipo chini ya Mwambusi, ingawa kwa takribani siku mbili aliondoka kambini na kwenda Mbeya kuhani msiba wa ndugu yake, hivyo akaiacha timu chini ya kocha wetu mpya Nasreddine Nabi.

 

 

“Kutokana na Nabi ishu za vibali kutokaa sawa, hivyo Mwambusi ataongoza benchi hadi pale kibali cha kocha kitakapopatikana.”

Leave A Reply