The House of Favourite Newspapers

Nabi Atua na Mzuka Kama Wote Yanga SC

0

KOCHA Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, juzi alfajiri alishuka kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam na haraka akawataka wachezaji wote kuingia kambini kuanza mikakati ya mchezo dhidi ya Coastal Union.

 

Timu hizo zinatarajiwa kuvaana keshokutwa Jumapili saa kumi kamili jioni kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Yanga wataingia kambini wakiwa na hasira za kutolewa na Azam FC katika hatua ya nusu fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi.

 

Mmoja wa viongozi wa Benchi la Ufundi la timu hiyo, ameliambia Championi Ijumaa kuwa kocha amechukizwa na viwango vya wachezaji wake walivyovionyesha katika Mapinduzi, hivyo haraka amewaita wachezaji hao kambini.

Kiongozi huyo alisema timu hiyo kabla ya kocha Nabi kurejea nchini ilikuwa ikifanya mazoezi asubuhi kwenda na kurudi nyumbani kwenye Uwanja wa Avic Town, Kigamboni nje kidogo ya Dar.

 

Aliongeza kuwa baada ya kocha huyo kutua kwenye Uwanja wa Ndege haraka alitoa maagizo kwa uongozi kuwazuia wachezaji kurejea majumbani kwao baada ya mazoezi ya asubuhi na badala yake kuendelea kukaa kambini hapo.

“Nabi tayari yupo nchini tangu alfajiri ya leo (juzi) baada ya kutoka katika mapumziko yake ya siku saba huko Ubelgiji ilipokuwepo familia.

 

“Mara baada ya kushuka katika uwanja wa ndege huo, aliwapa taarifa viongozi wenzake wa benchi la ufundi kuwazuia wachezaji hao kurejea majumbani kwao mara baada ya mazoezi ya asubuhi kumalizika.

 

“Kocha amepanga kuwaongezea program ya mazoezi ya jioni ndani ya siku hizi mbili kuanzia leo (juzi) Alhamisi katika kujiandaa na mchezo dhidi ya Coastal Union tutakaoucheza Jumapili,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Alipotafutwa Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela alikiri kocha huyo kurejea na kusema: “Timu tayari ipo kambini pamoja na kocha Nabi katika kujiandaa na mchezo wetu wa ligi dhidi ya Coastal na kikubwa tunazihitaji pointi tatu ili tuendelee kukaa kileleni.”

Wilbert Molandi, Dar es Salaam

Leave A Reply