The House of Favourite Newspapers

Kocha wa Yanga Atamba “Simba Wametufunga, Lakini Ubingwa Wasahau”

0
Kocha Mkuu wa Yanga, Mtunisia, Nasreddine Nabi akiongea jambo baada ya mechi dhidi ya Simba.

KOCHA Mkuu wa Yanga, Mtunisia, Nasreddine Nabi, amekubali kufungwa dhidi ya Simba katika Kariakoo Dabi, lakini amesisitiza hawatakubali kuuachia ubingwa wa Ligi Kuu Bara uende Simba.

Kauli hiyo aliitoa mara baada ya Yanga, juzi kufungwa mabao 2-0 dhidi Simba katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.

Katika mchezo huo, mabao ya Simba yalifungwa na Hennock Inonga na Kibu Denis ambayo yamewafanya wafikishe pointi 63, huku Yanga wakibakiwa na 68.

Akizungumza na Spoti Xtra, Nabi alisema mashabiki waondoe hofu ya kupoteza ubingwa wa ligi baada ya kufungwa dhidi ya Simba.

Nabi alisema anafahamu walipokosea na kusababisha wapoteze katika mchezo huo, hivyo anakwenda marekebisho upungufu uliojitokeza ili wafanye vizuri.

Aliongeza kuwa, hakuna kitakachowazuia kuutetea ubingwa huo wa ligi, kikubwa mashabiki wasikatishwe tamaa na matokeo hayo waliyoyapata na badala yake waendelee kujitokeza uwanjani kuwasapoti wachezaji wao.

“Niwaombe radhi mashabiki wa Yanga kwa matokeo haya mabaya tuliyoyapata dhidi ya Simba, ni matokeo mabaya na kuumiza kwao, kwetu benchi la ufundi na wachezaji.

“Lakini matokeo haya mabaya yasiwaogopeshe juu ya ubingwa kwani tutautetea msimu huu, hatutaruhusu uende kwingine.

“Matokeo katika dabi yasiwakimbize uwanjani, badala yake waendelee kuitokeza ili wachezaji wapate nguvu ya kupambania malengo,” alisema Nabi.

Yanga imebakiwa na mechi nne kumaliza msimu huu ndani ya Ligi Kuu Bara ambazo ni dhidi ya Singida Big Stars (ugenini), Dodoma Jiji (nyumbani), Mbeya City (ugenini) na Tanzania Prisons (nyumbani).

Katika mechi hizo nne, Yanga inatakiwa kukusanya pointi 10 tu kati ya 12 ili kujihakikishia ubingwa na pointi 78, wakati wenzao Simba nao wakipigia hesabu pointi 12 katika mechi nne zilizosalia ili wafikishe 77.

Mechi za Simba zilizosalia ni dhidi ya Namungo (ugenini), Ruvu (nyumbani), Polisi Tanzania (nyumbani) na Coastal Union (nyumbani).

Leave A Reply