NANI KASEMA USAWA MGUMU… TAJIRI AMWAGA FEDHA UKUMBINI

WEWE endelea kulialia, oooh usawa mgumu, vyuma vimekaza! Wenye shughuli zao wanapata fedha hadi za kumwaga ukumbini na kuwashughulisha watu kuziokota mpaka jasho kuwatoka. Ijumaa Wikienda limejionea kwa macho yake.

MZEE WA MWANZA NOMA

Usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita, tajiri mmoja aliyejulikana kwa jina la Mzee wa Mwanza aliwaacha watu midomo wazi baada kumwaga noti za elfu kumikumi ndani ya Ukumbi wa Next Door Arena uliopo Masaki jijini Dar kiasi cha ‘kuchafua’ sakafu.

Ukiuliza kulikuwa na nini ndani ya ukumbi huo siku hiyo hadi tajiri huyo kufanya kufuru hiyo? Jibu ni kwamba ilikuwa ni bethidei ya mwanamuziki wa Bongo Fleva, Faustina Charles maarufu kama Nandy.

JOKATE NDANI

Mbali na sherehe hiyo iliyohudhuriwa na mastaa kibao wa Bongo sambamba na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo, pia kulifanyika uzinduzi wa albam mpya ya Nandy iitwayo The African Princes. Wakati hayo yote yakiendelea hakukuonekana kama ndani ya ukumbi huo kulikuwa na tajiri mwenye fedha chafu hadi pale albam ilipoanza kunadiwa ambapo baadhi ya mastaa na watu maarufu walijitokeza kuinunua.

Miongoni mwao alikuwa ni Kajala Masanja aliyeinunua kwa shilingi laki mbili, Jacquiline Wolper, laki mbili pia na Aunty Ezekiel alijitwalia kwa kiasi cha laki na nusu. Wengine ni Daktari Elizabeth Kililia aliinunua kwa shilingi milioni moja na Kiongozi wa B-Band, Banana Zorro aliinunua kwa shilingi laki mbili.

PETIT MAN KULIKONI?

Wakati zoezi la kuinadi likiendelea ndipo mnadishaji aliyetajwa kwa jina la MC Pilau alimgeukia Ahmed Hashim ‘Petit Man’ na kumwambia kulikoni mbona hajipigipigi mfuko kuunga mkono shughuli?

Mara baada ya kutajwa, Petit Man alikamata kipaza sauti na kusema yeye amemsaidia sana msanii Nandy na kwamba muda mfupi ujao angepandisha kampani yake ikiongozwa na Mzee wa Mwanza. Awali ilionekana kama anafanya usanii, hata pale alipotupatupa vinoti vichache vya elfu kumi watu hawakumwelewa sana hadi pale kampani yake iliyokuwa chini ya tajiri huyo ilipoingia.

MZEE WA MWANZA SASA

Ilikuwa kama mkimbia mbio ndefu asiyeanza mashindano kwa mbwembwe, Mzee wa Mwanza alianza kumwaga fedha ukumbini hapo huku watu wakiokota na kuzihifadhi kwenye mkoba kama watu wasemao enzi za kuchafua sakafu zilikuwa zimepita.

Zitaishia hapa, zitaishia hapa! Waliowaza hivyo walikuwa wanajidanganya kwani Mzee wa Mwanza alizidi kutandaza fedha kwenye sakafu kiasi kwamba mkoba uliokuwa ukitumika kuhifadhi noti hizo nyekundu uliishiwa nafasi.

RANGI NYEKUNDU

Hata pale walipoongezeka waokotaji, mvua ya fedha kutoka kwa Mzee wa Mwanza haikukatika; ukumbi ukapendeza kwa rangi nyekundu huku shangwe na vifijo vikitawala miongoni mwa waalikwa.

MZEE WA MWANZA NI NANI?

Hapo sasa maswali yakawa; “Ni nani huyu, nani huyu?” Wenye kumjua wakasema anaitwa Mzee wa Mwanza, tajiri anayemilimiki migodi ya dhahabu kutoka Kanda ya Ziwa. Pengine kivutio kilikuwa ni pale wengi walipomtazama; hakuonekana kuwa ni mzee sawa na jina lake, pengine uzee ulitokana na kuwa na ‘fedha chafu’ kama wasemavyo watoto wa mjini.

MASTAA WAMTAMANI

Kufuatia kuonesha jeuri hiyo ya fedha, tajiri huyo ghafla aligeuka kuwa kipusa cha thamani ambacho baadhi ya mastaa wa kike walitamani kukipata kwa gharama yoyote. Vitendo vya kunong’onezana miongoni mwa mastaa havikupungua huku macho hayo yakiekea mahali alipoketi tajiri huyo ambapo ishara ya mwili ilionesha kama watu wasemao: “Ukimpata huyu, mjini unaishi kwa raha.”

Katika pitapita yake ukumbini mle Ijumaa Wikienda liliwasikia baadhi ya mastaa wakimhusisha tajiri huyo kuwa na uhusiano wa kimapenzi na msanii mmoja wa Bongo Muvi (jina kapuni) na kwamba ndiye aliyekuwa anampa jeuri ya fedha katika siku za hivi karibuni.

Ijumaa Wikienda lilipojaribu kumfikia tajiri huyo ukumbini humo kwa lengo la kumuuliza juu ya jeuri hiyo ya fedha wapambe wake walikuwa nuksi mara elfu; walimlinda kwa nguvu zote. Mwisho wa picha shughuli ya Nandy ilimalizika na kila mmoja kushika hamsini zake, huku Ijumaa Wikienda likibaki na sintofahamu kama kweli tajiri huyo ni mfanyabiashara wa madini au kuna shughuli nyingine pia anafanya.

JIONEE KWENYE VIDEO HII MCHEZO ULIVYOKUWA 

Loading...

Toa comment